Umuhimu wa mkulima kuwa na mpango kazi

Muktasari:

Ni sawa na siwezi kukataa kuwa kilimo kinalipa. Kikubwa hapa napenda kuweka sawa kuwa utakaposikia kuwa mwenzio kufanikiwa kutokana na zao fulani sio kweli kuwa na wewe hutofanikiwa.

Wakulima wengi tumekuwa tukilima kwa kusikia tu kwa wenzetu kuwa kilimo kinalipa.

Ni sawa na siwezi kukataa kuwa kilimo kinalipa. Kikubwa hapa napenda kuweka sawa kuwa utakaposikia kuwa mwenzio kufanikiwa kutokana na zao fulani sio kweli kuwa na wewe hutofanikiwa.

Utafanikiwa ikiwa utaangalia mambo muhimu hasa kwa mazingira yako. Fanya utafiti ili ujue kama nawe utapata mafanikio kama wenzako au la.

Unaposikia mafanikio ya mwenzako, wewe jiulize maswali haya: amevuna kiasi gani? shamba lake lina ukubwa upi?, amevuna mazao kiasi gani na yenye uzito gani?, ameuza kwa bei gani?, amelima lini na kuvuna lini (kulima kwa msimu). Mwisho amekumbana na changamoto zipi?

Katika makala ya leo, nataka kuwafundisha kuhusu mpango kazi katika kilimo. Huu unaweza kuandaliwa na wakulima au hata kwa kuwatumia wataalamu.

Mpango kazi ni neno pana likiwa na maana ya kitu au mwongozo wa kimaandishi ambao huandikwa kwa malengo ya kumpa mhusika muongozo jinsi gani anaweza kufanya mradi wake kwa uhakika na kwa ufanisi.

Umuhimu wa mpango kazi

1.Humpa mkulima muongozo sahihi wa jinsi ya kuanza kilimo chake, kwa muda maalumu kuendana na soko. 2. Humsaidia mkulima kupata mkopo wa kilimo

3.Humsaidia mkulima kujua gharama muhimu za kilimo chake pamoja na faida, hivyo kabla hajalima hujitambua mapema na hatimaye kufanya maamuzi sahihi.

4.Humsaidia kuweka kumbukumbu ya mambo muhimu katika kilimo, hivyo kurahisisha wengine kuja kufanya kilimo kwa muongozo huohuo.

5.Humwepusha mkulima kukwama njiani kwa gharama kuzidi, hii hutokana na kwamba mpango kazi unahusisha gharama za ziada kwa mambo yasiyotegemewa.

6.Ni njia ya kisasa ambayo humfanya mkulima kuonekana kilimo chake au biashara yake ni ya kisasa na iliyopangiliwa.

7.Humsaidia mkulima kujiandaa na dharura ambazo zinaweza kutokea kama kukosa soko, kuharibikiwa vifaa, Lakini pia humsaidia mkulima kujua uhalisia wa mradi wake katika mazingira yake.

Sehemu za mpango kazi

Huwa na utangulizi muhimu, uongozi au menejimenti ya shamba, masoko na bei ya kuuza bidhaa, maelezo ya bidhaa husika na uzalishaji wake kwa ekari, gharama kwa ekari na mauzo, vitu hatarishi na jinsi ya kujikinga navyo. Mambo haya huandikwa kwa ufupi sana katika utangulizi kisha kuelezwa kwa undani katika sehemu husika. Kwa ufupi sana huwa na mambo yafuatayo:-

1.Utangulizi mdogo wa mmiliki wa shamba, eneo la shamba lake lilipo, ukubwa wa shamba na zao analohitaji kulilima. Historia ya shamba kwa ufupi na umiliki halali wa shamba.

2.Malengo ya zao hilo kulimwa, kinachotegemewa kupatikana, bei husika ya kuuzia na walengwa wa kununua mazao hayo.

3.Faida inayotegemewa kupatikana, je, huo mradi unalipa? Hapa ili upate mkopo ni lazima mradi huu uwe na faida.

4.Miaka ya utendaji ya mradi huo.

5. Uongozi wa mradi huo, idadi ya wafanyazi, kiasi cha fedha utakachowalipa.

6.Washindani wako ni nani na upungufu wao. Weka pia uwezo na upungufu wako, lengo likiwa kujua namna ya kuzalisha bidhaa bora.

7.Kipengele cha kuonyesha faida na hasara ya mradi. Hapa kila zao litawekewa gharama halisi mwanzo mpaka kuvuna na kisha gharama kwa ajili ya vitu vya dharura. Kisha mavuno pamoja na fedha itayohitajika.

0713593894