Umuhimu wa sanaa katika elimu ya awali

Muktasari:

  • Wakoloni walipokuja pia waliheshimu sanaa katika elimu, shule zao zilikuwa na somo la sanaa(shule zote za wazungu na wahindi na chache za waafrika) na ni uelewa huu wa sanaa ukiongozwa na Baba wa Taifa , Mwalimu Nyerere ulisaidia kuanzisha Taasisi, mifumo na ujenzi wa sekta hii baada ya nchi yetu kupata Uhuru. Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka kuwa utamaduni ni roho ya Taifa. Je aliona nini ambacho hatukioni?

Kumekuwa na hoja mbalimbali juu ya umuhimu wa kufundishwa sanaa katika shule hasa za msingi na sekondari (kwa makala hii nitaiita ya awali). Tanzania ndio mwanzo wa sanaa ulimwenguni kwani sanaa za mababu zetu za mapangoni zinadhaniwa kuwa za kale kuliko zote. Kulikoni vitukuu vya wabunifu, wagunduzi sanaa wa mwanzo duniani kutothamini urithi wao?

Wakoloni walipokuja pia waliheshimu sanaa katika elimu, shule zao zilikuwa na somo la sanaa(shule zote za wazungu na wahindi na chache za waafrika) na ni uelewa huu wa sanaa ukiongozwa na Baba wa Taifa , Mwalimu Nyerere ulisaidia kuanzisha Taasisi, mifumo na ujenzi wa sekta hii baada ya nchi yetu kupata Uhuru. Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka kuwa utamaduni ni roho ya Taifa. Je aliona nini ambacho hatukioni?

Kwa kuanzia yapo maeneo mawili hapa: elimu ya sanaa na sanaa katika elimu. Nianze na sanaa katika elimu. Sanaa ina maana kubwa katika masomo na fani zingine kama vile hesabu, jiografia, historia, sayansi na masomo mengine yote zikiwamo lugha kwani fasihi ni sanaa. Umuhimu wa elimu ya sanaa katika utabibu ni mkubwa na hata sanaa hutumika kama aina ya tiba (therapy).

Ili mtu awe daktari, katika masomo yake anakuwa amechora michoro mingi na kuisoma michoro mingi sana. Vivyo hivyo kwa wahandisi, wachora ramani za majengo, wajenzi, na hata wapishi! Naam, mahoteli na migahawa hutumia sana sanaa kuleta chakula kikiwa katika hali ya kupendeza machoni.

Kila bidhaa inayouzwa ulimwenguni sasa lazima isanifiwe vyema ili soko liikubali. Kwa hiyo eneo la biashara pia linatawaliwa na sanaa. Kwenye upande wa magazeti, televisheni, redio, na machapisho mbalimbali ndio usiseme; sanaa inatumika si haba. Huu ndio mchango wa sanaa katika fani zingine, ni mchango usiokwepeka. Kwa maana hiyo habari ya Tanzania ya viwanda itakufa asubuhi kama sanaa haitopewa umuhimu wake.

Hebu sasa tuangalie elimu ya sanaa. Mwanasayansi maarufu, hayati Albert Einstein aliwahi kusema “mawazo bunifu ni muhimu kuliko elimu”. Binadamu anavutika na sanaa apende asipende sababu yeye mwenyewe ni sehemu ya sanaa ya uumbaji na. Hatua ya kwanza ya kuunda kitu kipya ni kubuni.

Kubuni ndio mwanzo wa utunzi na ugunduzi baadae ndipo hufuata uumbaji wa mawazo na vitendo. Sayansi ya ubunifu huitwa “innovation” na pale inapokuwa na matumizi halisi katika jamii hutambulika kama teknolojia. Upo ugunduzi ambao haujapata matumizi. Hivyo kitu cha kwanza kwenye mchango wa somo la sanaa ni kumpa mwanafunzi uwezo wa kupaa na mawazo yake na kuumba kimawazo.

Bila ubunifu watoto wetu watakuwa kama CD iliyonasa, wataimba nota moja ya sauti kutwa kucha wakisubiri kupewa nota nyingine kwa kukaririshwa. Katika nchi ya Finland watoto hawaanzishwi darasa la kwanza mpaka miaka saba, wao wanaamini kipindi hiki cha awali ndio cha kujenga ubunifu na kucheza. Nchi hii ndio inayoongoza katika elimu huko ulaya kwa miaka 16 sasa.

Eneo la pili linalopewa mchango mkubwa na sanaa katika makuzi ya mtoto ni uzingativu, umakinifu na urefu wa muda wa uzingatiaji. Mtu afanyaye sanaa hujenga uwezo wa kulenga mawazo katika eneo moja hata mara nyingine akasahau mambo yanayomzunguka, kwa kifupi uwezo wa kuzingatia humzamisha msanii ndani ya kazi yake na kumpa uwezo wa kuichambua vilivyo.

Uwezo huu wa uzingatiaji ukizoeleka huweza kutumika katika maeneo mengine ya masomo na maisha. Uzingativu ndio mwanzo wa maendeleo yoyote yale kwa sababu hapo tu ndio binadamu huweza kuwa na kina cha mawazo na kuweza kuchambua kitu kwa undani

Uvumilivu na nidhamu ni tunu kubwa ya mtu anaejifunza sanaa. Kwenye sanaa hakuna matokeo ya haraka haraka. Rangi za maji katika sanaa ya upakaji rangi huchukua muda fulani kukauka kabla ya kupaka nyingine. Kulichonga gogo au kujifunza ala za muziki nako kunahitaji uvumilivu na nidhamu kubwa. Bila nidhamu na uvumilivu sanaa haitoki na ikitoka inakuwa ndivyo sivyo.

Sanaa humfundisha mtoto kuwa na ung’ang’anizi (tenacity) na kunepa (resilience). Wanasanaa wengi hufanya sanaa zao kwa uvumilivu mkubwa wakisubiri matokeo, ukiwaangalia ni watu wenye kujibadili katika kila hali, ije mvua lije jua, vyuma kukaza ama kulainika. Bila sifa hii mambo mengi tunayofurahia duniani yasingekuwepo. Watu waliogundua vitu huwa na sifa hii ya ubishi.

Akili ya kawaida hutengeneza tafsiri lakini akili ya mwanasanaa hutengeneza dhahania ambayo ikiwasilishwa katika utendaji ndio inakuwa sanaa yenyewe. Uelewa wa maisha unakuwa finyu sana bila ya uelewa wa sanaa. Ulimwengu ni sanaa ya Muumba.

Ving’amuzi vya sanaa hiyo ni macho kuona, masikio kusikia, kuhisi, kunusa na ladha. Ving’amuzi hivi visipoamshwa kuanzia shuleni, uwezo wa kung’amua uzuri wa yanayoletwa mbele yetu katika maisha unadumaa bila kujali uwezo wako kimaisha.

Lakini sio kung’amua tu, bali kutafsiri kwa kumbukumbu za asili yako. Kwa maana hii inakuwa kichekesho kwa Mtanzania kutafsiri wimbo wa kizungu kwa vigezo na kumbukumbu za kizungu.

Mwandishi ni msanii na

mkurugenzi wa mipango wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania.