Umuhimu wa uzalendo, maadili

Muktasari:

  • Kauli hii inasikika kutoka kwa viongozi na hata wasanii, wakiwemo walio mstari wa mbele kupotosha maadili na utamaduni wetu na kuona mwanamume kusuka nywele au kuvaa hereni ni uzalendo wa kuendeleza utamaduni wa Watanzania.

Siku hizi kila wakati unasikia Watazania, Bara na Visiwani, wakikumbushana umuhimu wa kuweka mbele uzalendo.

Kauli hii inasikika kutoka kwa viongozi na hata wasanii, wakiwemo walio mstari wa mbele kupotosha maadili na utamaduni wetu na kuona mwanamume kusuka nywele au kuvaa hereni ni uzalendo wa kuendeleza utamaduni wa Watanzania.

Wapo ambao, labda kwa kuwa wazalendo zaidi kuliko watu wengine hapa nchini, hunukuu kauli maarufu ya Rais wa zamani wa Marekani, John Kennedy ya Fikiria nini utaifanyia nchi yako na sio nchi yako itakufanyia nini (Think what you can do for your country and not what your country can do for you).

Hawa watu wanaomnukuu Kennedy nadhani wangeonyesha dalili za uzalendo, kama wangenukuu misemo mingi ya hapa kwetu inayosisitiza umuhimu wa uzalendo badala ya kutupeleka Marekani.

Kwa mfano, kwa nini wasitukumbushe usemi maarufu wa Waswahili wa MTU KWAO na badala wake watuambie Kennedy aliwaambia nini Wamarekani?

Hivi karibuni kumekuwapo kampeni maalum ya kushajiisha Watanzania kuwa wazalendo na kuwataka waipende nchi yao. Hili ni jambo zuri na linalofaa kupongezwa.

Nilifurahi hata kumsikia Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, hivi karibuni naye akiwakumbusha Wazanzibari umuhimu wa kuweka uzalendo mbele.

Dk Shein aliwataka Watanzania kutathmini uzalendo wao ambao alisema umeshuka kwa kasi na hili sio jambo zuri kwa taifa.

Kwa maneno yaliozoeleka kusikika kutoka kwa wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ninamuunga mkono Dk Shein mia juu ya mia.

Hapana ubishi kwamba uzalendo ni mhimili muhimu wa kujenga taifa imara, ndio maana hata katika wimbo wetu wa taifa tunasema wazi wazi …Tanzania…Tanzania nakupenda kwa moyo wangu wote.

Lakini, tusisahau kuwa uzalendo unakuja kwa mamo mengi. Mwananchi hujiona ni mwana wa nchi aliyozaliwa na kuwa na uzalendo anapoona kwa vitendo anathaminiwa, kuheshimiwa na kuenziwa kama mzalendo.

Inapotokea mtu anaona uzalendo wake umepuuzwa na hathaminiwi kama raia huona hana sababu ya kuonyesha uzalendo kwa sababu yeye hahesabiwi kama mzalendo na kwa kuwa ni hivyo kwa ini ajipakazie sifa asiyostahiki?

Nimesema hivi kwa sababu mbalimbali. Mngoni mwao ni ile ambayo nimeipigia kelele mara nyingi juu ya baadhi (kama sio wengi) ya watu wa Zanzibar kuona au kuhisi uzalendo wao hauthaminiwi na wananyimwa haki za kiraia.

Kwa mfano, mpaka leo wapo mamia ya watu wamenyimwa haki ya kiraia ya kuwa na kadi ya utambulisho wa kuwa ni Wazanzibari licha ya wao na wazazi wao kuzaliwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Ukichunguza utaona hii inatokana zaidi na mambo ya kisiasa. Kutokana na hali hii wanakosa haki yao ya kushiriki katika uchaguzi na hata kupata tabu, kukosa mambo mengi kama hati ya usafiri, leseni ya biashara na mambo mengine.

Hivyo, kweli mtu anayetendewa haya atakuelewa unapomtaka aonyeshe uzalendo wakati huo uzalendo wake hauthaminiwi?

Nalizungumzia hili sio kwa utani na ninaamini kama patafanyika mikutano kila wilaya ya kuwataka wajumuike watu walionyimwa kadi za utambulisho wa Mzanzibari na ya kupiga kura basi kila ukumbi utafurika watu.

Watu hawa wapo tu Visiwani, hawana mbele wala nyuma. Baadhi yao huhangaika wanapotaka tiketi ya kusafiri kati ya Unguja na Pemba au kwenda Dar es Salaam kwa vile hawana vitambulisho.

Ni kawaida kuona watu hawa wanazungushwa kama pia, nenda huku nenda kule na mwisho wa siku wanakwenda kapa, yaani hawapatiwi vitambulisho.

Mimi binafsi ninawafahamu watu wengi wa aina hii na nimelisema hili mara kwa mara na kuahidiwa litafanyiwa kazi, lakini sioni chapati wala mandazi.

Niliwahi kulizungumzia katika mkutano wa waandishi wa habari alioufanya Ras Shein hapo Ikulu ya Zanzibar, lakini limebaki kufumbiwa macho kama vile halipo na sababu sio nyengine isipokuwa siasa ndio imewekwa mbele na kusahau haki za raia.

Wakati mmoja nilikwenda Idara ya Uhamiaji na hapo ndipo nikaona maajabu. Mama mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 alikuwa anataka kupewa hati mpya ya usafiri ambayo kwake ni ya tatu au ya nne ili aende Makah kufanya ibada ya hijja.

Alichotakiwa ni kutafuta watu waliomjua baba yake ambaye alikufa zaidi ya miaka 10 iliyopita akiwa na miaka 90 ili kuthibitisha huyo baba yake alizaliwa Zanzibar.

Haya ni maajabu kwa sababu kila aliyemjua baba wa huyo mama alizaliwa Zanzibar, alikuwa ameshatangulia mbele ya haki na hata mwili wake huko kaburini ulishageuka udongo.

Ama ingekuwapo teknolojia ya kuzungumza na maiti kaburini hilo lingewezekana, lakini kwa ufahamu wangu bado teknolojia hio haijavumbuliwa.

Sasa unapokihangaisha kizee kama huyu kupata hati ya usafiri ili kwenda Makkah kumuabudu Mola wake, kweli atakuwa na imani kwamba kuzaliwa kwake Visiwani kunathaminiwa na kuheshimiwa?

Kwa kauli na vitendo vinavyofanywa na watumishi wachache wa Serikali ndio vinavyopelekea watu kuona uzalendo hauna maana yoyote kwao.

Vile vile, nataka niweke bayana kwamba yapo malalamiko mengi Zanzibar ambayo hayafai kupuuzwa ya kuwepo upendeleo na wengine wanasema ni ubaguzi katika kupata ajira serikalini.

Nimesikia watu wengi wakilalamika na tumeambiwa lisemwalo lipo na kama halipo lisingezungumzwa, kwamba ni akina fulani tu, yaani Ibni Kininana na Ibni Khuzaymat ndio wanapewa umuhimu katika kupatiwa ajira na hata nafasi za masomo. Kwa lugha nyengue wapo wanaoitwa wenzetu na wapo wanaotajika kuwa sio wenzetu.

Kwa Zanzibar, hata uwe na moyo sugu wa kutumikia ndugu zako, lakini ukiwekwa katika orodha ya huyu si mwenzetu elimu yako na juhudi zako za kusaidia wenzako hazithaminiwi na utatengwa.

Huu ndo ukweli na wnaaoununa wanune, shauri yao.

Nimeyasema haya mara nyingi na nitasema kwa sababu inaumiza na zaidi utaona waliokuja Zanzibar kwa mbeleko au mbio za mwenge ndio mashabiki wakubwa wa kuendeleza mwenendo huu.

Bila ya kutafunia maneno nataka nieleze wazi kwamba zipo hisia miongoni mwa watu wengi wa kisiwa cha Pemba kwamba wanatengwa. Hili halifai kupuuzwa na Serikali na ni bora litafutiwe muarubaini wa kulitibu kwani hasara na madhara yake ni makubwa kwa siku za baadaye.

Wazanzibari lazima waachane na tabia ya mimi Mtumbatu, wewe Mmakunduchi, huyu Mwarabu, yule Mzaramo,, yule Mmakonde, huyu Mngazija na yule Mpemba ndio wataweza kusonga mbele na kujipatia maelewano na maendeleo.

Vinginevyo wataendelea kuwa na misuguano isiyo na maana kwao na vizazi vijavyo. Tujifunze kutokana na makosa tulioyatenda na yaliowakuta wenzetu waiojigawa katika makundi ya raia daraja la kwanza na raia daraja la pili. TUTUPIE MCHO NCHI JIRANI.

Dhana ya mtu kwao huwa ya kweli kila mtu anapoona na kuamini anaheshimika na kuthaminiwa kwao na sio mpaka anapoondoka kwao na kwenda kwengine.