JICHO LA MWALIMU : Umuhimu wa zana za kufundishia kwa mwalimu

Muktasari:

Hii ni kwa sababu ya mbinu na njia za ufundishaji za baadhi ya walimu kushindwa kuwagusa.

        Wakati mwingine baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kupata maarifa na ujuzi tarajiwa katika hatua fulani ya elimu.

Hii ni kwa sababu ya mbinu na njia za ufundishaji za baadhi ya walimu kushindwa kuwagusa.

Mathalani, maandalizi duni ya mwalimu kabla ya kufundisha na kutotumia zana mbalimbali za kujifunzia na kufundishia, zinaweza zikawa sababu mojawapo ya baadhi ya wanafunzi kushindwa kuelewa somo, hivyo kusababisha washindwe kufaulu majaribio na mitihani.

Zana za kufundishia na kujifunzia ni kitu chochote ambacho mwalimu hutayarisha, kwa lengo la kukitumia anapokuwa anafundisha ili kuinua kiwango cha uelewa na elimu kwa jumla.

Pia, zana za kujifunzia na kufundishia huwakilisha vifaa vyote ambavyo mwalimu hutayarisha na kutumia wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji, ili zimrahisishie ufundishaji wake na kuwafanya wanafunzi waelewe somo kirahisi zaidi.

Hivyo, zana za kufundishia na kujifunzia ni vifaa vinavyotumika katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji.

Makundi ya zana

Wataalamu wa saikolojia ya elimu na njia za ufundishaji, hugawa zana za kujifunzia na kufundishia katika makundi makubwa matano kama yanavyoainishwa hapo chini kwa kuzingatia umuhimu:

Moja, vitu halisi: Hivi ni bora kuliko zana nyingine kwa kutimiza lengo lake la kufundisha. Kwa mfano, vitu halisi vinaweza kuwa ni matunda, saa, simu, maji, chupa, samaki, mafuta na nyundo.

Mwalimu anapotumia vitu halisi katika somo lake, husababisha wanafunzi wake kujenga hali ya kuwa na uwezo wa kuchunguza, kuhoji (kudadisi), kugundua na kufurahia somo.

Zana zilizopo katika kundi hili la vitu halisi huzidi kuwapa fursa wanafunzi nafasi kubwa ya kujifunza kwa vitendo na kutumia milango mingi ya fahamu kwa wakati mmoja.

Mbili, zana bandia; wakati mwingine huitwa zana za maumbo au kwa lugha ya Kiingereza ‘model’ (modeli). Kundi hili la zana huchukua nafasi ya pili kwa ubora kutoka kundi la zana halisi.

Endapo hakuna uwezekano wa kupata kitu halisi, mwalimu anaweza kuchagua kutumia vitu bandia au vitu vilivyo mfano wa vitu halisi.

Kwa mfano; badala ya mwalimu kubeba kisu halisi au matunda halisi anaweza kuchukua kisu na matunda bandia (ya plastiki) yaliyotengenezwa mfano wa kitu halisi.

Faida za matumizi ya vitu au maumbo bandia huzidi zana za picha na chati kwa sababu vitu bandia hufanana na vitu halisi.

Tatu, runinga, video na sinema. Matumizi ya runinga, sinema na video kama zana za kujifunzia na kufundishia huwezesha wanafunzi kutazama na kuona vitu kama vilivyo katika uhalisia wake. Pia, wanafunzi huweza kuona na kusikia kinachofanyika katika picha jongefu.

Nne, picha na michoro: Kundi hili huwakilisha vifaa kama chati, grafu, ramani, mabango madogo na makubwa. Kundi hili la zana huzidiwa ubora na runinga kwa sababu huwawezesha wanafunzi kuona tu. Hivyo, zana hizi huhitaji uwezo wa uoni.

Tano, vinasa sauti, redio, cd na santuri. Kundi la zana hizi za kujifunzia na kufundishia humsaidia mwanafunzi kujifunza kwa kusikia.

Ni kazi ya mwalimu husika kutayarisha vipindi mbalimbali kwa kuvirekodi kupitia kinasa sauti. Zana hizi huweza pia kutumiwa na wanafunzi wanaosoma kwa njia ya masafa (learning distance).

Umuhimu wa kutumia zana

Matumizi ya zana za kujifunzia na kufundishia yana faida kwa pande zote mbili; humsaidia mwalimu kufikisha lengo au ujumbe kwa mwanafunzi.

Pia, mwalimu anapotumia zana, mwanafunzi hupata faida kwa kujifunza zaidi kwa kuona,kugusa, kuonja, kunusa, na kusikia (kwa kutumia milango yote ya fahamu)

Humsaidia kubadilisha mazingira ya kupatia maarifa na ujuzi; kumfanya afurahie somo hivyo kulipenda. Pia, kumpatia mwanafunzi maarifa na ujuzi kwa njia ya mkato na ujuzi wa maarifa hayo huwa vigumu kusahaulika upesi.

Kumuonyesha ukweli katika somo kwa sababu mwanafunzi huona vitu vya kweli au mifano yake; na kumsaidia kumfanya mwanafunzi ajifunze kwa njia ya kutenda na si kwa kusikiliza tu.

Sifa za zana zana za kufundishia

Zana zinazotumika kufundishia zinapaswa kuwa na uhusiano na mada inayofundishwa; nadhifu na zinazovutia; uhalisia; usahihi zisizoleta tafsiri mbaya kwa kundi fulani la imani ya dini; kubwa na zinazoweza kuonekana kwa darasa zima na zisizoleta madhara ya macho au masikio (zisiwe hatarishi). Pia, zana zinapaswa ziweze kuhamishika au kubebeeka kwa urahisi.

Umuhimu wa kuzijaribu zana kabla ya kutumika

Ni vizuri mwalimu akazijaribu zana au vielelezo vyake kabla ya kuvitumia darasani. Kwa kufanya hivyo, mwalimu hupata faida nyingi zikiwemo kuhakikisha kama zana/ vifaa hivyo vinafanya kazi kwa usahihi kama vilivyokusudiwa.

Kubaini kama kuna zana au vifaa vibovu ili viweze kutengenezwa au kutafuta vingine; kugundua udhaifu wa zana au vielelezo alivyopanga kuvitumia; kutambua haraka kama kuna madhara ya kiimani, yanayoweza kuletwa na vielelezo hivyo

Pia, kufahamu namna sahihi ya kutumia zana husika.

Matumizi ya zana au vifaa katika kujifunzia na kufundishia ni nyenzo muhimu kwa sababu husaidia katika ujenzi wa maana kwa kile mwanafunzi atakachojifunza. Vilevile, zana hurahisisha kazi ya mwalimu ya kufundisha.

Hivyo basi, zana za kujifunzia na kufundishia hupaswa zitumike kulingana na lengo la somo. Zitumike katika hatua yoyote ya somo kulingana na mpangilio wa mwalimu na lengo la zana husika.

Lengo hasa la kutumia zana katika kufundisha liwe kukuza na kuinua kiwango cha kujifunza cha mwanafunzi.

Ni vema na ni wajibu wa walimu kujifunza namna rahisi ya utengenezaji wa zana kwa kutumia malighafi zinaopatikana katika maeneo yao.