Una haja ya kujifunza tabia mpya katika maisha yako

Muktasari:

Unapoongezea tabia nzuri ni lazima utambue haziwezi kuwa tabia zako kwa kuziandika tu katika orodha. Katika zoezi hili watu wangi wenye akili timamu hupendelea kuwa na tabia nzuri nyingi zaidi. Ni watu wachache tu ambao huweza kufikiria kuongeza tabia zisizofaa.

Je, unaweza kuandika orodha ya tabia zako zote? Kama unaweza kuziandika zitenge katika makundi mawili. Kundi moja liwe la zile ambazo zinakusaidia na zenye manufaa hata kwa watu wengine na kundi la pili ni zile ambazo hazina maana na hata zinawaudhi watu wengine. Kama utafanya zoezi hili kwa uaminifu huku ukiamini hakuna atakayeiona orodha yako kuna mambo mawili ambayo huenda ukafikiria kuyafanya. Kwanza utasikitika kugundua kuwa baadhi ya tabia zako mbaya ni zile ambazo ungependelea kuziacha haraka ili kuboresha utu wako. Jambo la pili ambalo litakujia katika fikara zako ni kuongeza orodha ya tabia zako nzuri.

Unapoongezea tabia nzuri ni lazima utambue haziwezi kuwa tabia zako kwa kuziandika tu katika orodha. Katika zoezi hili watu wangi wenye akili timamu hupendelea kuwa na tabia nzuri nyingi zaidi. Ni watu wachache tu ambao huweza kufikiria kuongeza tabia zisizofaa.

Lakini unapopata mawazo ya kuongeza tabia nzuri ina maana unatambua umuhimu wa tabia katika maisha yako ya kila siku. Hebu fikiria baadhia ya tabia ulizonazo. Asubuhi unaamka mapema, unaoga na kupiga mswaki na kuvaa nguo na viatu. Pengine kabla ya kutoka kitandani unaweza kufungua redio au televisheni ili kupata taarifa za habari. Baada ya kujitayarisha, unajipatia kifungua kinywa na kuondoka nyumbani kuelekea kazini. Hizi ni baadhi ya tabia ulizojizoeza tangu ulipokuwa mtoto.

Mtu ana tabia kama hizi tulizozitaja na nyingine nyingi ambazo zote kwa pamoja hufanya maisha yake kuwa mazuri na ya furaha. Kwa kawaida mtu hujikuta ana tabia nyingi za utaratibu wa maisha ambazo zimemwingia au kumvaa zenyewe na pengine bila kufanya juhudi ya kuzipata ama kuzifikiria. Tabia hizo zinaweza kuwa kama vile ucheshi na kuzungumza vyema na watu, kuheshimu wanaokuzidi umri na kustahi wadogo, ukarimu na huruma kwa watu, uadilifu, staha, uaminifu na nyingine nyingi. Jambo muhimu katika maisha ni kuzidumisha na kuziboresha zaidi.

Kudhibiti mfumo wa kupata tabia

Tukumbuke kuwa kwa kufanya mazoea fulani tunaweza kustukia tumebadili baadhi ya tabia. Inabidi tuwe makini kuepuka kujifunza tabia mbaya. Hii ni kwa sababu tabia mbaya hutupotezea wakati na kutufanya tushindwe kupata mafanikio katika maisha. Aidha ni dhahiri kuwa zipo tabia zinazoboresha mienendo yetu na kutufanya tupate mafanikio makubwa katika maisha.

Kumbuka kuwa kwa vile umekwisha kuwa mtu mzima juhudi za kuunda tabia mpya ambazo zitafanya maisha yako yawe mepesi zinakutegemea wewe mwenyewe. Ulipokuwa ungali mdogo misuli na mfumo wako wa neva za hisia ulikuwa haujakomaa kiasi cha kukuwezesha kukabiliana na mazingira na kujenga tabia zote ambazo ni muhimu kwa maisha yako. Wakati ule kila hatua ya mendeleo ya kupata tabia mpya ilitegemea mafunzo kutoka kwa wazazi, walimu na watu wengine walio kuzidi umri.

Kwa kuwa sasa umekua, wewe mwenyewe unaweza kufahamu sababu za kujenga tabia mpya. Ili kuunda tabia mpya unahitaji kuwa na dhamira na utashi wa dhati. Licha ya utashi mkubwa jambo la pili ni kuandaa utaratibu thabiti utakaokufanya uitende tabia hiyo mara kwa mara ili kuweza kujenga mazoea na kujiridhisha kuwa unachokifanya kitasaidia kuimarisha hiyo tabia mpya.

Kanuni za kujifunza tabia mpya

Kujenga tabia mpya na kujifunza kitu kipya kunafanana sana. Maana ya kujifunza ni nini? Kujifunza ni kujipatia mwelekeo fulani kikamilifu katika mfumo wa neva ya ufahamu. Hivyo, kujipatia tabia mpya ni kujifunza kwa kufuata kanuni kuu mbili zifuatazo.

(a) Kwanza kuwa na matakwa thabiti ya kujifunza

(b) Pili kuandaa mpango au utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara ya kutenda tabia hiyo hadi uimudu kuitekeleza kwa usahihi.

Hebu tutumie mfano ufuatao

Kulikuwa na mtu aliyekuwa akifanya kazi katika mji na akiishi katika kijiji cha mbali. Hivyo, kila siku asubuhi alikuwa akiondoka nyumbani na kutembea kuelekea kazini. Na jioni vivyo hivyo akipata taabu kwa kutembea kurudi nyumbani. Alikuwa anachelewa kufika kazini asubuhi na jioni pia alichelewa kurudi nyumbani.

Wakati huo huo kulikuwa na jirani yake aliyekuwa akitumia baiskeli kwenda kazini na kurudi nyumbani. Jambo hili lilimfanya yule jirani yake ajiulize afanye nini kwa kuwa hakuwa akijua kuendesha baiskeli. Hata hivyo alikiri moyoni kuwa ingekuwa vyema kiasi gani kama angeweza kwenda na kurudi kazini kwa baiskeli kama mwenzake.

Kama ungekuwa wewe ungefanya nini ? hapana shaka ungeamua kufanya kama jirani yake kutumia baiskeli. Hivyo utakuwa na budi kujifunza kuendesha baiskeli. Hii ni hatua ya kujifunza tabia mpya ya kuendesha baiskeli hatua ya kwanza katika dhamira ya kujitunza tabia hii mpya itakuwa kujizatiti katika utashi wako. Hatua ya pili utaanza kujifunza jinsi ya kukaa juu ya baiskeli kwa uwiano wa uzito ulio sawa ili usiegemee upande mmoja na kukufanya ukaanguka. Kisha kuanza kujifunza kuendesha baiskeli.

Hatua ya tatu itakuwa kutambua kuwa ili uweze kuendesha baiskeli huna budi kufanya mazoezi. Hivyo, utalazimika kupanga muda na kufanya mazoezi kwa usahihi ili kuuzoesha mfumo wako wa neva uwe umejifunza na kukuwezesha kuimudu hii tabia mpya.

Utaweza kujifunza tabia mpya kwa kufuata hatua kama hizi

Kanuni za kuacha tabia mbaya

Kama vile mtu anavyoweza kujifunza tabia mpya pia kuna njia ya kupangua na kutupilia mbali tabia usiyoipenda. Hapana shaka unaelewa jinsi mtu anavyosahau haraka jambo analolijua anapoacha kabisa kulitenda kwa muda. Hii ndiyo njia unayoweza kuitumia ili kuacha tabia ambayo hupendi kuendelea nayo. Tunaposema tabia mbaya tuna maana ule mwenendo ulio nao unaoudhi watu wengine na kuwafanya wapoteze imani na upendo kwako au ile tabia ambayo inaweza hata kuathiri afya yako.

Unapokusudia kuiacha tabia mbaya unaweza kufuata hatua zifuatazo:-

(a) Kwanza uwe na nia na utashi thabiti wa kuicha kabisa tabia hiyo

(b) Uyakinie katika nafsi yako na ujiridhishe kikamilifu na uamuzi wako wa kwa nini umeamua kuiacha hiyo tabia.

(c) Fanya mazoezi ya kuacha kuifanya hiyo tabia hadi utakapohakikisha imetoka kabisa katika mfumo wako wa neva.

Hitimisho

Tabia ndiyo inayomtofautisha binadamu na mnyama. Hivyo, kadri mtu anavyokuwa na tabia njema ndivyo kadri anavyouimarisha ubinadamu wake. Kila mmoja wetu anawajibika kuhakikisha anaimarisha utu wake kwa kuongeza tabia bora na kuacha tabia mbaya kama makala hii ilivyotufunza.