Unaambiwa usajili wa Sh1.3bil umelipa Msimbazi

Muktasari:

  • Ubora wa kikosi cha wekundu hao wa Msimbazi umetokana na nguvu kubwa ya fedha zilizowekezwa kwenye usajili wa kikosi chao chenye thamani ya Sh1.3bilioni.

Baada ya misimu minne bila kutwaa ubingwa hatimaye Simba imetawazwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2017/2018.

Ubora wa kikosi cha wekundu hao wa Msimbazi umetokana na nguvu kubwa ya fedha zilizowekezwa kwenye usajili wa kikosi chao chenye thamani ya Sh1.3bilioni.

Mwanzoni mwa msimu huu, Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alielezea mchakato mzima kwenye mkutano wa kawaida wa kila mwaka wa wanachama uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Alisema kwamba wamesajili kikosi madhubuti kwa gharama kubwa, lengo likiwa ni kurejesha heshima ya klabu yao huku akitoa mchanganuo kuwa wachezaji wa kigeni pekee wamewagharimu Sh679milioni. Hapo ni kabla ya Ahsante Kwasi kusajiliwa.

Wachezaji walioigharimu Simba fedha hizo ni kipa Aishi Manula aliyesajiliwa kutoka Azam kwa lengo la kuchukua mikoba ya Daniel Agyei ambaye alionekana kutofanya vizuri na Peter Manyika ambaye naye alitimkia Singida United na Simba ilipoamua kumsajili, Emmanuel Mseja kutoka Mbao FC na kumpa mkataba wa miaka miwili ili kuziba nafasi ya Manyika.

Hata hivyo, Simba iliongeza nguvu kwenye eneo hilo kwa kumsajili kipa bora wa kombe la Cosafa 2017, Said Mohamed ‘Nduda’ aliyetokea Mtibwa Sugar.

Shomary Kapombe ambaye amehusika kwa kiasi kikubwa na mafanikio ya Simba kwa kucheza kama beki na wakati huo ni winga alitua ndani ya klabu hiyo kutoka Azam akiwa majeruhi kabla ya hali yake kutengemaa.

Usajili mwingine ambao Simba iliufanya kwenye dirisha kubwa ni kumnasa beki wa kushoto wa Mbao, Jamal Mwambeleko ambaye alitua kama msaidizi wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Lakini mambo yaliwaendea kombo mabeki wote hao wa kushoto pale ambapo Asante Kwasi kutoka Lipuli alipotua ndani ya klabu hiyo kwenye dirisha dogo na kufiti kwenye mfumo wa kisasa wa benchi la ufundi la timu hiyo.

Kiraka Erasto Nyoni ambaye alikuwa akitizamwa kama mkongwe ambaye hatoweza purukushani na vijana alisajiliwa Simba akitokea Azam na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi hicho kwa kucheza kama beki wa kulia na kushoto kabla ya kutumika kwenye nafasi ya beki wa kati.

Simba ilihitaji kujenga eneo lake la ulinzi ambalo liliondokewa na Abdi Banda ambaye alitimkia Afrika Kusini kwenye klabu ya Baroka inayoshiriki ligi kuu nchini humo.

Kujenga kwao eneo la ulinzi mbali na kumchukua Erasto pia ilimsajili Salum Mbonde na Ally Shomary wote kutoka Mtibwa Sugar.

Ukiachilia mbali walinzi hao wawili ambao hawajawa na msimu mzuri pia Simba ilitumia mwanya wa kushuka daraja kwa Toto Africans ya Mwanza kwa kumsajili, Yusuph Mlipili ambaye amefanya vizuri kwenye eneo la beki wa kati.

Simba walipoondokewa na mshambuliaji wao, Ibrahim Ajib kwa kuhamia Yanga, ilifanya usajili uliozua mijadala mingi nchini kwa wapenda soka kwa kumnasa, Haruna Niyonzima kutoka Yanga.

Hata hivyo, Mnyarwanda huyo alikuwa akisumbuliwa na majeraha yaliyomfanya kwenda nchini India kufanyiwa matibabu ya kawaida japo awali alitajwa kwenda na hakufanyiwa upasuaji.

Nyota mwingine ambaye Simba ilimsajili ni mshambuliaji kinda, Nicholas Gyan kutoka Ebusua Dwarfs ya Ghana ambaye alianza kwa kusuasua ndani ya kikosi hicho kabla ya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Simba msimu huu kwa kutumika kwenye nafasi tofauti.

John Bocco naye alikuwa ingizo jipya ndani ya klabu ya Simba akitokea Azam ambayo iligoma kumuongezea mkataba, kutokana na mahitaji ya wekundu hao wa msimbazi mshambuliaji huyo ameitendea haki jezi nyekundu kwa kufunga mabao 14.

Wakati Bocco akifunga idadi hiyo ya mabao pia pacha wake anayecheza naye kwenye safu ya ushambuliaji, Mganda Emmanuel Okwi ambaye na yeye alisajiliwa kipindi hicho akitokea SC Villa amefunga mabao 20 na sasa ndiyo mabingwa Bara.