UCHAMBUZI: Usaliti CCM haukuanza mwaka 2015

Muktasari:

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulifanya mabadiliko ya 16 ya katiba ya chama hicho na pia uliondoka na makada 12 waliodaiwa wasaliti kutokana makovu ya uteuzi wa mgombea wa urais 2015.

Mkutano Mkuu maalumu wa CCM uliomalizika kwa kishindo hivi karibuni uliacha alama nyingi, mojawapi ni kuanza kuwaadhibu wanaodaiwa wasaliti.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulifanya mabadiliko ya 16 ya katiba ya chama hicho na pia uliondoka na makada 12 waliodaiwa wasaliti kutokana makovu ya uteuzi wa mgombea wa urais 2015.

Si vigogo hao 12 pekee waliotimuliwa, bali katika mikoa yote timuatimua imefanyika na sasa inaelekea Zanzibar. Hivi karibuni hapa Arusha wana-CCM 1,520 walivuliwa uanachama, jambo ambalo halikuwahi kudhaniwa.

Ni ukweli, usaliti ni moja ya dhambi kubwa yenye madhara makubwa katika kundi la watu wanaofanya kazi pamoja.

Hata hivyo, katika siasa zetu hapa nchini usaliti umekuwa ukitafsiriwa katika namna mbalimbali, wapo wanaoitwa wasaliti kwa kuwapenda viongozi fulani ndani au nje ya vyama, wengine kwa kununuliwa na wengine na hata kwa kusimamia kutovunjwa katiba za vyama vyao.

Kutokana na tafsiri hizo, hata adhabu ya usaliti zimekuwa zinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.

Ni dhahiri usaliti unaodaiwa na CCM sasa ni mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2015 ndani ya chama hicho. Hivi nani asiyejua kuwa Edward Lowassa kabla ya kuhamia upinzani alikuwa na wafuasi wengi hasa baada ya kuishi ndani ya CCM kwa zaidi ya miaka 50.

Lowassa alikuwa na marafiki tangu shule za msingi, sekondari, chuo kikuu, jeshini, bungeni na hadi serikalini, hivyo kwa ushawishi wake, haikuwa rahisi na haitakuwa hivyo kwa watu wote kumtupa.

Mbali na CCM, karibu vyama vyote vimewahi kukumbwa na migogoro iliyohusiana na usaliti, tuliona Chadema na Zitto Kabwe na hata CUF na akina Hamad Rashid.

Wote waliofukuzwa katika vyama vya upinzani, wamekuwa wakihusishwa na kutumiwa na CCM na dola kuhujumu harakati za upinzani au viongozi wa vyama husika.

Safari hii, mambo yamegeuka, chama tawala kinawang’oa viongozi na wanachama kibao kwa usaliti na kuunga mkono upinzani.

Hata hivyo, ukifuatilia mwenendo wa chama hicho tawala, utabaini kuwa usaliti ndani yake haujaanza mwaka 2015, umeanza muda mrefu pale viongozi walipoamua kuachana na katiba yao na kanuni zake na kujiundia taratibu mbadala za kuendesha mambo kwa manufaa yao.

Viongozi walijiwekea taratibu za kupatikana viongozi kinyume na maelekezo ya CCM, waliunda mitandao imara nje ya chama hicho na hadi kufikia viongozi kuwa na nguvu zaidi ya chama.

Kila ulipofika mkutano mkuu, mapendekezo mapya yaliibuliwa, uteuzi wa viongozi wa ngazi ya taifa, mikoa na wilaya haukufuata tena taratibu za chama hicho na hivyo kuwa na viongozi wanaoheshimu waliowateua badala ya kuheshimu chama hicho.

Hakika wengi wanaamini CCM ya Mwalimu Julius Nyerere siyo hii CCM ya leo, hivyo kuna ulazima wa kuhoji uadilifu wa viongozi wa sasa na waliopita ndani ya chama unaowapa mamlaka ya kuwatuhumu wengine kwa usaliti.

Kwa hali ilivyo sasa, kinachofanyika si kuwaondoa wasaliti wa CCM bali kuondoa waliokuwa kambi ya Lowassa ndani ya CCM, ilhali wasaliti wakubwa wakingalipo.

Katika uchaguzi uliopita kabla ya uteuzi wa mwisho ilikuwa vipande vipande. Hivi nani ndani ya CCM ambaye anaweza kusema hakuwa na kambi.

Hivyo itoshe kusema usaliti ndani ya CCM haukuanza mwaka 2015 baada ya Lowassa kuhama bali ulianza zaidi ya miaka 20 iliyopita hasa baada ya mwalimu kungatuka.

0754296503