JICHO LA MWALIMU : Usimamizi katika sekta ya elimu si kukosoa pekee

Muktasari:

  • Usimamizi huhusisha kuonyesha njia, kufanya kwa vitendo na kuwa mbunifu katika kutekeleza malengo na maono ya shule kwa njia zisizodhalilisha wafanyakazi, wanafunzi, wazazi au walezi na jamii kwa jumla.

        Moja ya majukumu ya kiongozi katika sekta ya elimu, ni usimamizi wa karibu wa shule anayoiongoza.

Usimamizi huhusisha kuonyesha njia, kufanya kwa vitendo na kuwa mbunifu katika kutekeleza malengo na maono ya shule kwa njia zisizodhalilisha wafanyakazi, wanafunzi, wazazi au walezi na jamii kwa jumla.

Usimamizi mzuri huchangia kwa kiwango kikubwa katika kutimizwa kwa malengo na shabaha za elimu na shule kwa kusimamia miongozo, sera, taratibu na kanuni zilizotolewa na mamlaka zinazosimamia elimu.

Usimamizi katika ngazi ya shule huhusisha vitendo vya kiongozi wa shule kuwezesha kiuweledi walimu na wafanyakazi wasio walimu katika shule katika kutekeleza majukumu yao, kama vile inavyopaswa na kama inavyoelekezwa katika majukumu ya kiutendaji ya kila mmoja.

Ipo miongozo mbalimbali ambayo hutolewa na vyombo vinavyosimamia elimu katika kuwaongoza viongozi katika ngazi mbalimbali za elimu.

Kupitia usimamizi, kiongozi hutambua na kuwasaidia walimu wake kutokana na changamoto na matatizo yanayowakabili kitaalamu, kwa lengo la kuongeza ari na tija ili kukuza maendeleo ya kitaaluma na ujifunzaji au ufundishaji.

Ufuatiliaji huu unaambatana na tafiti kabla ya kufanya maamuzi yoyote yanayohusiana na tendo la ujifunzaji na ufundishaji.

Bila ya kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi au utafiti kujua ukweli wa mambo, kiongozi anaweza kufanya maaamuzi yasiyo sahihi hivyo kuleta migogoro na mifarakano. Hatua hizi huwa ni za kidemokrasia na siyo za kibaguzi kiasilia.

Kwa nini tunahitaji usimamizi bora?

Katika muktadha huu, mtu anaweza kujihoji kwa nini tunahitaji usimamizi bora katika shule zetu?

Umuhimu wa usimamizi bora katika shule na hata vyuo unajidhihirisha katika mambo yafuatayo:

Moja, kuhakikisha kwamba kila mwalimu anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Pia, mwalimu wa somo anafundisha kwa kufuata mitalaa iliyotolewa na mamlaka ya elimu.

Kwa mfano, katika ngazi ya familia, mama hutimiza wajibu wake wa majukumu ya kinamama katika muktadha wa utamaduni husika wa Kitanzania.

Wakati mwingine baba hufuatilia ili kuona kama kila kitu kinaenda na inapotokea kuna jambo halikwenda sawa, mama anaweza kuwatupia mzigo wa lawama wasaidizi wa kazi.

Mbili, kuhakikisha kwamba wafanyakazi (walimu) wanafanya kazi yao katika kiwango cha juu na kwa uweledi.

Tatu, usimamizi humwezesha mwalimu mkuu kutambua uwezo na vipawa mbalimbali walivyo navyo walimu au wafanyakazi wasio walimu. Kwa kutambua vipaji vyao, humpa nafasi kiongozi wa shule kupanga safu yake ya kumsaidia vizuri.

Pia, kukuza vipawa hivyo kwa kutoa fursa ya mazingira wezeshi kwa kuwalenga wanafunzi na malengo ya shule.

Nne, kutambua mwelekeo wa shule. Kwa kufuatilia kwa karibu, kiongozi wa shule anaweza kugundua mwelekeo wa shule yake kama ni sahihi na unaelekea kufikia malengo au la.

Ufuatiliaji unamwezesha kiongozi kuona maendeleo ya kitaaluma, kijamii, kiuhusiano na katika shughuli zilizo nje ya mtalaa.

Tano, kukuza kiwango cha kitaaluma cha walimu. Kiongozi anaweza kugundua upungufu wa walimu wake na kushirikina pamoja nao katika namna ya kuboresha changamoto hizo za ufundishaji.

Sita, kuweza kutambua walimu au watumishi ambao wanapaswa kupandishwa madaraja, vyeo, kuhamishwa au kusimamishwa au kufukuzwa.

Kwa kutambua uwezo wao na utendaji, anaweza kupanga namna ya kuwapa motisha wafanyakazi wake.

Usimamizi katika ngazi ya darasa huweza kufanywa na mwalimu mlezi wa darasa, mwalimu wa somo husika na hata mwalimu wa zamu kwa kuhakikisha anawafahamu wanafunzi wake na changamoto wanazokutana nazo ili waweze kuwasaidia.

Kiongozi wa shule asipofanya usimamizi wa karibu, anaweza kusababisha matatizo mengi baadaye ikiwao kushindwa kutumia rasilimali kikamilifu.

Zipo namna mbalimbali za ufuatiliaji na usimamizi. Kwa mfano, usimamizi wa ‘muendelezo’ au wa kila siku. Hii ni kuhakikisha shughuli zilizopangwa zinatekelezwa kama ipasavyo.

Ufuatiliaji huu kimsingi, unapaswa kufanyika kila siku hasa kunapokuwapo jambo fulani linalotekelezwa. Ufuatiliaji huu una umuhimu kwa ngazi ya shule na hata familia katika kupunguza matatizo kabla hayajakomaa na kuwa tatizo sugu.

Tumezoea kusubiri mwisho wa jambo na kuanza kutafuta sababu jambo hilo kuharibika, kumbe ingewezekana kama jambo hilo lingekuwa likifanyiwa tathmini wakati likiendelea.

Mwalimu asisubiri mpaka wanafunzi wamefanya mitihani yao ndiyo wafanye usimamizi na ufuatiliaji.

Pia, upo ufuatiliaji wa mwisho kwa ajili ya kufanya maamuzi. Katika ngazi ya shule, huu huhusisha kupandisha cheo, kupunguza cheo, motisha kwa kutoa zawadi ama adhabu.

Katika ngazi ya familia, ufuatiliaji na usimamizi wa namna hii unaweza kusababisha maamuzi ya wazazi au walezi kubadilisha shule ya watoto, baada ya kuona maendeleo katia shule hiyo siyo mazuri.

Hivyo, usimamizi katika ngazi ya elimu haushii tu kwa viongozi wa shule, wazazi na wadau wengine wa elimu katika kukosoa tu pale wanapoona kuna upungufu. Wanapaswa kutazama na kushauri kabla matatizo hayo hayajitokeza.

Katika ngazi ya familia, wazazi na walezi hawana budi kuwa mfano bora wa kuigwa katika malezi na makuzi ya watoto.

Aidha, wazazi wana wajibu wa kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu maendeleo yao ya kitaaluma, kimaadili, kimakuzi, kiroho na kitamaduni

Ufuatiliaji usiishie tu katika ukaguzi wa madftari au karatasi za mitihani kwa nia ya kukosoa tu.