MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Utalijuaje shina la kitenzi katika Kiswahili?

Muktasari:

Kutokana na uhusiano wake na mzizi wa neno, baadhi ya wanafunzi huichanganya dhana hii na mzizi wa neno. Mzizi wa neno na shina la neno ni dhana mbili tofauti kiisimu ingawa zina uhusiano. Kuwapo kwa shina la kitenzi hutegemea mzizi wa neno kama tutakavyoona katika mjadala huu.

Mpenzi msomaji wa safu hii, baada ya kuangalia mada ndogo za mofimu na mzizi wa neno katika matoleo mawili yaliyopita, leo hii tuangalie dhana ya shina la neno.

Kutokana na uhusiano wake na mzizi wa neno, baadhi ya wanafunzi huichanganya dhana hii na mzizi wa neno. Mzizi wa neno na shina la neno ni dhana mbili tofauti kiisimu ingawa zina uhusiano. Kuwapo kwa shina la kitenzi hutegemea mzizi wa neno kama tutakavyoona katika mjadala huu.

Awali ya yote yafaa tuelewe maana ya dhana hii. Shina la kitenzi ni mzizi wa kitenzi uliofungiliwa irabu. Katika muktadha huu, tunapozungumzia mzizi, tunamaanisha mzizi asilia au mzizi wa mnyambuliko (rejelea darasa lililopita la mzizi wa kitenzi).

Kwa muhtasari, shina la kitenzi tunapata kwa kuunganisha mzizi wa kitenzi husika na irabu. Aidha, irabu inayotajwa hapa ni ‘a’ kwa vitenzi vile vyenye asili ya Kibantu. Kwa ufupi: Shina = mzizi + irabu (a).

Hebu tuangalie data ifuatayo:

Mzizi Shina

chez+a cheza

imb+a imba

ruk+a ruka

o+a oa

Katika data hiyo (juu), kwenye sehemu ya ‘mzizi’ tunaona mizizi ya vitenzi

(-chez-, -imb-, -ruk- na -o-) huku kwenye sehemu ya ‘shina’ tunaona mashina ya vitenzi ambayo yametokana na kuongezewa irabu ‘a’ na hivyo tukapata maneno kama yanavyoonekana yaani cheza, imba, ruka na oa (mashina).

Tuweke msisitizo kwamba, namna hii ya uundaji wa mashina ya vitenzi hufanyika katika maneno yenye asili ya Kibantu kama ilivyoelezwa hapo awali. Hii ni kwa sababu licha ya Kiswahili kuwa na msamiati mwingi utokanao na maneno ya lugha za Kibantu, Kiswahili kina msamiati wenye asili ya lugha za kigeni mathalani Kiarabu, Kiingereza na kadhalika.

Katika vitenzi vyenye asili ya lugha hizo za kigeni, ili kuweza kupata shina la kitenzi kanuni itumikayo ni tofauti.

Vitenzi vyenye asili ya kigeni ambavyo huishia na irabu a, e na u kama vile arifu, tafiti, sali na jibu (vyenye asili ya Kiarabu); shina halipatikani kwa kuongeza kiambishi ‘a’ katika mzizi wa neno. Katika uundaji wa shina la neno, kwa vitenzi vingi ya namna hiyo mashina hubakia kama namna vitenzi vyenyewe vilivyo.

Chunguza data hii:

Kitenzi Mzizi Shina

i) arifu -arif- arifu (arifa*)

ii) tafiti -tafit- tafiti (tafita*)

Lengo la data hii ni kuonyesha kuwa, vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya kigeni haviundi shina la mzizi wa kitenzi kwa kuongeza irabu ‘a’ mbele ya mzizi wa kitenzi kama vile vyenye asili ya Kibantu. Ikiwa vitafanya hivyo, havitaleta maana.

Kutoka katika data hiyo, rejelea maneno arifa* na tafita* (ambayo kwa kanuni tuliyokuwa nayo yangekuwa mashina yetu). Kwa hiyo, vitenzi hivyo (vya kigeni) vina ughairi.

Tuhitimishe mjadala huu kwa kusisitiza kuwa, ili kupata shina la neno katika kitenzi katika hali yoyote kilivyo, hatua ya kwanza tafuta mzizi na kisha ongeza irabu ‘a’ na kwa vile ambavyo vina asili ya kigeni, zingatia maelezo yaliyotolewa katika mjadala huu.