Utampenda tu, Kichuya huyu huyu

Muktasari:

  • Simba na Yanga zinapocheza, Kichuya hawaachi Yanga salama hata mara moja. Kati ya mabao yatakayofungwa, lake moja halikosekani.

Katika siku za karibuni, inawezekana kabisa kwenye mechi ya mahasimu, Yanga hawapati usingizi wakisikia jina la Shiza Kichuya limo kwenye listi wanaoanza. Ndiyo, hata ukiguna.

Simba na Yanga zinapocheza, Kichuya hawaachi Yanga salama hata mara moja. Kati ya mabao yatakayofungwa, lake moja halikosekani.

Ni katika Kombe la Mapinduzi tu hakuwafunga. Simba ilishinda mikwaju ya penalti 4-2 zilizowekwa kimiani na Jonas Mkude, Kipa Daniel Agyei, Muzamil Yasin na Bokungu wakati ile iliyopigwa na Mwanjali iliokolewa na kipa wa Yanga, Munishi.

Mechi hiyo ilikuwa ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, ilipigwa Januari 8.

Nyuma kidogo, Oktoba Mosi 2016, Simba ilitoka sare ya 1-1 na Yanga ambayo iliongoza hadi dakika ya 87, Kichuya akachonga kona iliyokwenda moja kwa moja kimiani.

Februari 25, Simba iliichapa Yanga mabao 2-1, moja Laudit Mavugo na lingine la ushindi kapiga Kichuya.

Ikaja Ngao ya Jamii, Agosti 23, kama miezi sita hivi baada ya pambano ya Februari. Mechi hii ya kukunjua pazi la Ligi Kuu. Simba ilishinda mikwaju ya penalti 5-4.

Walofunga ni; Method Mwanjale, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim ‘Mo’ walifunga wakati Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ mkwaju wake wa penati ukidakwa na golikipa wa Yanga.

Si umeona hapo, Kichuya hakuwaacha salama Yanga, alitupia penalti yake.

Haya, juzi tu hapa, Oktoba 28, mechi ya Ligi Kuu, Simba ilianza kufunga, na aliyetupia ni huyo huyo japo bao lake halikudumu, Obrey Chirwa akalichomoa kama dakika tatu hivi baadaye. Unaweza kusema ni mbaya wa Yanga.

Jina la winga huyo wa Simba, lilipata umarufu muda mfupi baada ya kutua Msimbazi msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar.

Alifanya mambo si ya kawaida hata akatupiwa jicho na wadau wa soka nchini kwani alifunga zaidi ya magoli 10, katika msimu wake wa kwanza tu.

Mechi mbili za watani wao Yanga, mzunguko wa kwanza na wa pili zilimpa ufalme baada ya kufunga magoli mawili ya kihistoria katika mechi zote mbili.

Spoti Mikiki, imefanya mahojiano maalumu na winga huyo, amezungumzia maisha yake kwa mwaka huu baada ya ongezeko la mastaa wapya ndani ya kikosi cha Simba ambao majina yao yamekuwa yakitajwa kila inapoitwa leo na wadau wa soka ndani na nje ya nchi.

Simba aliyoingia na hii

“Ingizo jipya la wachezaji wazoefu ndani ya Simba, limeibua changamoto ya mimi kujituma kwa bidii kuhakikisha uwezo wangu haushuki bali unaongezeka na kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa msimu uliopita.”

Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima ni kati ya wachezaji ambao Kichuya anakiri wana uzoefu wa juu ambao unamfanya akili yake iwaze kwa mapana kutambua majukumu yake kwa kina.

“Wachezaji wote Simba ni wazuri, lakini angalia wanaotajwa na mashabiki mara kwa mara, unakuta ni Okwi na Niyonzima, kutajwa kwao ni somo kwangu kwamba wana kitu cha ziada kinachoonekana machoni kwao, lazima nijue kocha anataka nini kwangu ndipo naweza kufika mbali,” anasema.

Anafafanua kwamba hana maana ya kuwaogopa bali anaheshimu uzoefu walionao tofauti na mchezaji ambaye ana hamu na kutoka ili afikie mafanikio yao.

“Kila msimu una utofauti na ndiyo maana usajili wa msimu huu una wachezaji tofauti na mwaka jana, hilo linatosha na ninatakiwa kuwa mjanja wa kusoma nyakati na kuendana nazo ili nisiachwe na ushindani wa kazi bora,”anasema.

Mpenda kuthubutu

“Huwa sijifikirii mara mbili, mimi napenda kujaribu nione kama ninaweza na ndiyo maana ninakuwa na hatua kila ninapocheza.

“Natumia fursa ya kujifunza kwa mchezaji aliyekaribu yangu, nikiamini nitapata hatua moja mbele, uwepo wangu Simba najituma ili nijifunze kitu kitakachonipa hatua moja mbele,”

“Siogopi kumfuata mchezaji na kumuuliza siri ya mafanikio yake ili nijifunze, unaambiwa uoga wako ndiyo umaskini wako,” anasema.

Utajiri wake

Anaweka wazi kwamba licha ya jina lake kujulikana na wadau mbalimbali nchini, lakini bado maisha yake ni ya kawaida tofauti na wadau wanavyomchukulia, kumuona ni mtu ambaye ana maisha ya kifahari.

“Ufahari wangu ni uwanjani, siwezi kusema sina hatua ila ni ndogo siwezi kujifananisha na hao wanaomiliki magari ya kifahari na majumba makubwa, bado nina safari ya kusaka mafanikio, ninaamini ipo siku moja nitafanikiwa,” anasema.

Jamii yake

“Ninaishi maeneo ya Mabibo, awali majirani zangu walikuwa wananitarajia kuwa mtu wa bata, ajabu wanaona nikitoka uwanjani ama mazoezi napitiliza kulala, kuniona ni wakati wa kula, iliwapa shida awali ila kwa sasa wananiona kawaida tu,” anasema.

“Watu wengi wanashindwa kufanikiwa na wanaishi maisha ya kuigiza kwa kupenda sifa yaani kuwa mjuaji wa kila kitu kisa wanafahamika.”

“Ustaa wangu mwisho uwanjani,nikirejea kitaa ni maisha ya kawaida,” anasema

Taifa Stars

Tangu ajiunge na Simba, amekuwa bandika bandua kwenye kikosi cha Taifa Stars na kumemsaidia kuwa na mtazamo wa kuwa mchezaji wa kimataifa.

”Nikiwa Stars, nakutana na timu za nchi tofauti na wanaocheza klabu tofauti, naona jinsi ambavyo wanaishi na namna ambavyo soka limewalipa na kuwa watu wa heshima”

“Unapojichanganya na watu ndivyo unavyozidi kupanuka kiakili ndiyo maana ninasema kwa sasa ninaanza kutazama ndoto zangu kuwa mchezaji wa kimataifa.”