MAONI YA MHARIRI: Utaratibu wa kula kiapo uongezewe wigo

Picha na Ikulu

Muktasari:

Hao ni maofisa 25 ambao Rais aliwapandisha vyeo kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).

Juzi, Rais John Magufuli alishuhudia maofisa 58 kati ya 60 wa Jeshi la Polisi wakila kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma wakati wakiitoa mbele ya mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Umma, Jaji Salome Kaganda.

Hao ni maofisa 25 ambao Rais aliwapandisha vyeo kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).

Wengine 35 aliwapandisha kutoka cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).

Walifanya hivyo kwa kuzingatia misingi ya maadili iliyoainishwa katika Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, ambayo yanamtaka kila kiongozi wa umma kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kuhusu utendaji wa Serikali.

Kama ilivyokuwa kwa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, manaibu wao, wakuu wa wilaya na hivi karibuni, wakurugenzi watendaji wa majiji, manispaa, halmashauri na miji, makamanda hao katika kutimiza matakwa hayo ya kikatiba na kisheria waliahidi mambo 12 katika kutimiza wajibu huo;

Mosi, waliahidi kuwa wazalendo kwa nchi na utii kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pili, waliahidi kuwa waadilifu na mfano kwa watumishi wa umma na watu wengine katika kukuza na kusimamia maadili. Tatu, waliahidi kutotumia vyeo au wadhifa wao kwa masilahi binafsi, ya familia, ndugu au marafiki zao isipokuwa kwa masilahi ya umma. Nne, waliahidi kulinda na kutumia rasilimali za umma kwa masilahi ya umma. Tano, waliahidi kutekeleza majukumu yao na kufanya uamuzi kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa masilahi ya umma.

Ahadi ya sita ilikuwa ni kutoomba, kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa huku ya saba ikiwa ni kutoomba, kutoa wala kupokea zawadi au fadhila za kiuchumi au za kisiasa au kijamii zisizoruhusiwa na sheria.

Ahadi ya nane ni kutotoa shinikizo kinyume na sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji kazi za umma, hususan ajira, kupandisha cheo, kuchukua hatua za kinidhamu au kuingia mikataba mbalimbali.

Katika ahadi ya tisa walisema hawatatoa taarifa za siri za Serikali au za mteja kwa watu wasiohusika isipokuwa kwa masilahi ya umma. Ya 10 ni kutekeleza majukumu yao kwa kuepusha mgongano wa masilahi wa aina yoyote na endapo utatokea uamuzi wake, basi utazingatia masilahi ya umma.

Pia, waliahidi kutoa huduma bora kwa usawa kwa watu wote bila kujali misingi ya dini, siasa, kabila, udugu, ukanda, jinsia, urafiki au hali ya mtu katika ahadi ya kumi na moja na mwisho waliahidi kuepuka tabia ambayo inavunja heshima ya uongozi wa umma hata wanapokuwa nje ya mahali pa kazi au watakapoacha kazi.

Huu ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha watumishi wa umma hawapelekwi kuanza majukumu yao bila ya kula kiapo cha kuwafanya kuiheshimu kazi, masilahi mapana ya taifa na kutumikia wananchi.

Rai yetu ni kwa Tume ya Maadili kuandaa mfumo utakaowezesha kuongeza wigo wa watumishi wengine wa umma wasio wateule wa Rais, kula kiapo kwenye eneo lao husika.

Pia, kwa kuwa Rais anataka kuanza upya, basi wale watumishi ambao wanaendelea na uteuzi uliofanywa na Serikali iliyopita ambao hawakufanya hivyo, waandaliwe utaratibu ili nao wafanye kazi kwa kiapo kimoja.