Utashi wa kisiasa kikwazo kikuu cha usawa wa kijinsia

Wanawake wakiandamana kudai mabadiliko yatakayoleta usawa wa jinsia.Picha ya maktaba

Muktasari:

  • Uwiano wa hamsini kwa hamsini haujafikiwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi, mila na desturi potofu, mafundisho mbalimbali ya kidini na elimu ndogo kwa jamii hasa kwa wanawake wenyewe.

Tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu, jitihada za wanaharakati mbalimbali kuleta usawa wa kijinsia bado hazijazaa matunda. Wanawake wamekuwa wakitengwa kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi na ndiyo waathirika wakubwa wa ukatili wa kijinsia.

Uwiano wa hamsini kwa hamsini haujafikiwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi, mila na desturi potofu, mafundisho mbalimbali ya kidini na elimu ndogo kwa jamii hasa kwa wanawake wenyewe.

Jumuiya ya kimataifa imekubaliana na kuandaa malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo yaliridhiwa mwaka 2015 na yanatakiwa kutekelezwa kwa miaka 15 mpaka mwaka 2030, ikiwamo kuleta usawa wa kijinsia.

Katika mwendelezo huo, Machi 8, ubalozi wa Ufaransa uliandaa kongamano la kimataifa la wanawake lililoambatana na siku ya kimataifa ya wanawake ulimwenguni. Kongamano hilo lilitoka na maazimio mbalimbali ya kusaidia kuleta usawa wa kijinsia.

Baadhi ya maazimio hayo ni wito kwa watunga sera na taasisi za kimataifa kuboresha mafunzo ya walimu katika ngazi zote; kutoa elimu ya jinsia na afya ya uzazi; kuwa na mfumo wa kutambua ugunduzi unaofanyika; kuunga mkono utawala bora na kuimarisha miradi ya kijamii.

Wadau wa jinsia wanasema elimu ndiyo njia pekee ambayo itaweza kuibadilisha jamii kuondokana na ukatili wa kijinsia na kuleta usawa kati ya wanawake na wanaume katika nyanja tofauti.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier anasema nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya sayansi kwa shule za sekondari na vyuo vikuu.

Anasema msaada huo unalenga kusukuma mbele maendeleo ya sayansi na teknolojia hapa nchini hasa kwa watoto wa kike ambao fursa yao ya elimu inazuiwa na jamii zao.

“Wakati huu, mkazo utawekwa kwenye kuinua ubora wa elimu hasa kwa masomo ya sayansi kwa sababu ndiyo kitovu cha maendeleo ya taifa lolote,” anasema Balozi Clavier.

“Mkazo huo utakuwa ni kusomesha wasichana wengi zaidi ili kuleta usawa wa kijinsia kwenye huduma za jamii. Wasichana wanatakiwa kuwezeshwa kama wavulana,” anaongeza balozi huyo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alifungua kongamano hilo, anasema Serikali imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi kwenye vyombo vya maamuzi, ikiwamo kuwapa nafasi za uongozi katika ngazi za juu serikalini.

Profesa Ndalichako anasema Rais John Magufuli ana imani na utendaji wa wanawake ndiyo maana aliwateua kwenye wizara nyeti kama vile elimu, afya na madini akiamini kwamba watafanya kazi kikamilifu kuleta maendeleo ya nchi.

Anasema Serikali imejizatiti kutekeleza malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu ikiwamo kuleta usawa wa kijinsia na kutoa fursa ya elimu hasa kwa mtoto wa kike.

“ Tumeshuhudia ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kupitia sera ya elimu bure. Pia, tumeboresha mafunzo ya walimu na kuweka uwiano wa mwalimu na mwanafunzi darasani,” anasema.

Waziri huyo anasema Serikali inasisitiza elimu kwa watoto wa kike kwa sababu wananyimwa fursa ya kwenda shule ili kujikomboa kifikra, pia kupata fursa ya ajira kuwawezesha kumudu maisha yao.

“Tunafanya jitihada kuboresha elimu hapa nchini. Tunaangalia pia elimu ya juu, tunashirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini,” anasema Profesa Ndalichako.

Kwa upande wake, Rais wa chama cha Taaluma za Sayansi nchini (TAAS), Profesa Esther Mwaikambo anasema ni idadi ndogo ya wanawake wanaoshiriki katika maeneo ya utafiti na maendeleo, uongozi serikalini na sekta binafsi.

Anasema sababu za wanawake kukosa fursa katika nyanja za sayansi, teknolojia na ugunduzi zinaanzia kwenye ukosefu wa fursa ya elimu na uwiano katika uwekezaji, mazingira ya kazi yasiyo rafiki, imani za kitamaduni na mila potofu.

“Kila mahali duniani lazima kushirikisha wanawake katika maamuzi ili maendeleo yawe endelevu. Hili litakamilika kwa kubadilisha mtazamo wa jamii, kuleta uhuru na usawa wa kijinsia, wanawake kuamua ukubwa wa familia na mambo mengine,” anasema Profesa Mwaikambo.

Wadau wasisitiza elimu

Wadau wa masuala ya jinsia wameikumbushwa jamii kutambua haki za wanawake na kuwapa nafasi katika nyanja mbalimbali za kielimu, kisiasa, kiuchumi na kijamii ili nao watoe mchango wao kwa jamii.

Hata hivyo, wanabainisha kwamba azma ya kufikia usawa wa jinsia wa hamsini kwa hamsini inakabiliwa na changamoto nyingi zinazosababishwa na uelewa mdogo wa jamii na kutokuwepo kwa maridhiano ya kitaifa ya kulinda haki za wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema vitendo vya ukatili bado vinaendelea kuripotiwa na wanawake wamekuwa waathirika wakubwa wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Dk Kijo-Bisimba anasema kuna haja ya kuwa na mpango maalumu wa kutoa elimu kwa jamii ili iondokane na matukio ambayo yanaripotiwa kila siku kuhusu unyanyasaji kijinsia. Anasisitiza kuwa Serikali kupitia jeshi la polisi lichukue hatua za haraka dhidi ya matukio yote yanayoripotiwa.

“Siku ya wanawake tunajikumbusha kuhusu haki za wanawake na kwamba ukatili haufai. Wanawake wana umuhimu mkubwa kwenye jamii zao, lazima waheshimiwe na kulindwa,” anasema mkurugenzi huyo.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Wabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga anasema kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa juu ya haki za wanawake ili Taifa liwe na msimamo wa pamoja wa namna ya kumlinda wanawake.

Anasema mwafaka huo wa kitaifa utalifanya Taifa kuwa pamoja na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika ulinzi wa haki za wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili. Anasema jamii itakuwa na wajibu wake, viongozi wa dini na sehemu yao na Serikali pia itakuwa na wajibu wake.

“Tunapenda kuona Serikali inakuwa na utashi mkubwa, kwa sasa utashi ni mdogo sana. Tunapenda kuona wanawake wengi wanateuliwa kwenye nafasi za uongozi katika idara na taasisi mbalimbali za Serikali,” anasema Sanga.

Mkurugenzi huyo wa Tamwa anaeleza kusikitishwa na mwenendo wa vyombo vya habari nchini kutoyapa kipaumbele mambo ya wanawake badala yake habari zinazopewa uzito mkubwa ni zile za siasa na watu maarufu.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii kwa kuripoti changamoto zinazowakabili wanawake na kuelimisha jamii juu ya mila potofu na imani ambazo ni kandamizi kwa wanawake,” anasema.

Kwa upande wake, mwanasheria na Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Felix Kibodya anafafanua kwamba sheria za Tanzania hazina tatizo lolote wala mianya inayosababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia bali tatizo liko kwenye mila na desturi ambazo zinakumbatiwa na makabila mbalimbali.

Kibodya anasema uwiano wa hamsini kwa hamsini haujafikiwa kwa sababu jamii nyingi hazitaki kumtambua mwanamke zikidai kwamba hawana uwezo wa kuwaongoza kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa.

“Tatizo siyo la kisheria bali ni la kimfumo, unaweza kuwa na sheria lakini hazitakuwa na nguvu kama hakutakuwa na mifumo inayomtambua mwanamke. Katiba na sheria zetu hapa Tanzania ziko vizuri, zinamtambua na kumlinda mwanamke,” anasema.

Anasisitiza kwamba jamii izidi kusomesha watoto wa kike ili wajitambue na kudai haki zao pale zinapokiukwa. Pia, anasema Serikali inaweza kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uteuzi na kuwapa nafasi kwenye majimbo badala ya kupewa nafasi za ubunge wa viti maalumu.