Utekelezaji wa bajeti ya Serikali unahitaji uwazi

Muktasari:

Mapendekezo ya matumizi katika kila kasma yaliwekwa kwenye tovuti wakati mjadala wa bajeti unaendelea.

Wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Serikali ilianzisha utaratibu wa kuchapisha vitabu vya bajeti kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha. Utaratibu huu ulianza baada ya makubaliano ya serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mapendekezo ya matumizi katika kila kasma yaliwekwa kwenye tovuti wakati mjadala wa bajeti unaendelea. Vitabu vitatu vilichapishwa na kuwekwa kwenye tovuti: makadirio ya matumizi ya kawaida ya wizara, idara na taasisi za Serikali; makadirio ya matumizi ya kawaida ya mikoa na; makadirio ya matumizi ya maendeleo.

Hata hivyo, makadirio ya mapato na vyanzo vyake hakikuwekwa na mafungu yake yaliwekwa sehemu nyingine ya tovuti. Makadirio ya mapato ya mwaka 2015/16 hayajawekwa kwenye tovuti mpaka sasa.

Wenye uwezo na utashi wa kuchambua bajeti na kasma zake waliweza kufanya hivyo na kutoa maoni yao kwenye vyombo vya habari au kuwashauri wabunge wao kujenga hoja za ubora au udhaifu katika mjadala ndani ya Bunge.

Baada ya kuijadili na kuipitisha, Serikali ilichapisha bajeti iliyoidhinishwa. Wachambuzi walipata fursa ya kulinganisha kati ya bajeti iliyopendekezwa na iliyopitishwa na kubaini endapo Serikali ilikubali marekebisho yaliyopendekezwa katika mjadala husika.

Bajeti ya kwanza ya Rais John Magufuli pia haijawekwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa kila kasma wala bajeti iliyoidhinishwa na bunge hazijawekwa vilevile.

Hii inawanyima fursa wachambuzi kufuatilia mgawanyo wa matumizi ya serikali kwa kila kasma. Vitabu vya bajeti vinaonyesha matumizi halisi katika kila kasma ya bajeti ya miaka miwili ya nyuma.

Kwa mfano vitabu vya bajeti vya 2016/17 vitakuwa na matumizi halisi ya mwaka 2014/15. Watafiti na wachambuzi wanaweza kulinganisha matumizi halisi ya 2014/15 na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge ya mwaka 2014/15 na kubaini kama matumizi ya serikali yaliongozwa na bajeti iliyoidhinishwa na bunge.

Kwa muda mrefu udhaifu wa bajeti yetu ni tofauti kati ya kiasi kilichoidhinishwa na bunge na matumizi halisi. Mara kwa mara bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa huwa haitekelezwi na matumizi ya kawaida yanakuwa makubwa kuliko ilivyoidhinishwa.

Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2015/16, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilitengewa Sh35.4 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo lakini mpaka Machi, 2016, ilikuwa imepokea Sh1.6 bilioni sawa na asilimia 4.5 ya fedha zilizoidhinishwa. Miradi ya wizara ya haikutekelezwa.

Bajeti ya mwaka huu imeongeza makadirio ya matumizi ya maendeleo mara mbili zaidi. Kutoka Sh5.9 trilioni mwaka 2015/16 mpaka Sh11.8 trilioni mwaka huu. Sawa na asilimia 40 ya bajeti yote. Vitabu vya bajeti vikiwekwa kwenye tovuti tutaweza kuchambua mgao wa bajeti kwenye kila kasma.

Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge.

Mradi unategemea kugharimu zaidi ya Sh16 trilioni. Upembuzi yakinifu wa mradi nao bado haujawekwa wazi ili wachambuzi na wadadisi waone kama utajilipa na kuongeza ukuaji wa pato la taifa ama la. Wananchi tumeaminishwa kuwa ni mzuri bila kupewa uchambuzi na upembuzi yakinifu.

Katika kutekeleza bajeti ya 2016/17, Serikali imenunua ndege mbili kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL). Hata hivyo haijaweka wazi mkakati wa kulifufua shirika hilo ili lifanye kazi kwa ufanisi na faida.

Baada ya ununuzi wa ndege hizo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Kapteni Johnson Mfinanga na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Sadick Muze kwa makosa ya uteuzi wa marubani wanaotakiwa kwenda kusoma nje ya nchi. Hii ni dalili ya kutokuwepo kwa mkakati na maandalizi ya kutosha ya utekelezaji wa mpango wa kuifufua ATCL.

Bajeti imelenga kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje na mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh18.46 trilioni, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote. Hata hivyo, mwezi wa kwanza wa utekelezaji wa bajeti hiyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) imeshindwa kufikia lengo. TRA imekusanya S1.055 trilioni sawa na asilimia 95.6 ya Sh1.103 trilioni zilizokusudiwa.

Ikiwa lengo halikufikiwa mwezi wa kwanza wa mwaka wa fedha ni vigumu kuamini malengo yatafikiwa katika miezi ijayo. Nina wasiwasi serikali itakuwa na wakati mgumu kupata mapato yanayokidhi kugharamia matumizi ya kawaida na ya maendeleo.

Taarifa ya IMF Julai 2016 inaeleza kuwa Serikali itaanza ujenzi wa Reli ya Kati katika robo ya mwisho wa mwaka wa fedha kama bajeti itaruhusu. Hata hivyo, Rais Magufuli amesisitiza kuwa shilingi trilioni moja zimetengwa kwa ajili ya mradi wa reli mwaka huu. Je mapato yakiwa kidogo kuliko ilivyokadiriwa, ni miradi gani itakayochwa?

Suala la nidhamu katika masuala ya bajeti bado ni changamoto. Baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kura zote za wajumbe walioshiriki, Rais Magufuli aliahidi kuhamishia makao makuu ya Serikali mijini Dodoma. Kipaumbele hiki hakimo kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Bajeti ya mwaka huu haikuweka mafungu ya kuhamisha makao makuu. Ikiwa bajeti ya kuhamia Dodoma haikuandaliwa mwaka huu, ni vyema utekelezaji wake wa uhakika ungeanza mwaka ujao wa fedha kutoleta athari kwenye miradi iliyoainishwa na kupitishwa na bunge.

Serikali itumie uzoefu iliyoupata wa miradi ya Akaunti ya Changamoto za Milenia (MCA) iliyofadhiliwa na Marekani.

Miradi hiyo ilifanyiwa upembuzi yakinifu ulio wazi. Gharama ya miradi ililinganishwa na faida yake. Mradi unatekelezwa ikiwa faida yake ni kubwa kuliko gharama zake. Kila Dola 100 inayowekezwa walau izae matunda yasiyopungua Dola 110.

Uchambuzi wa miradi yote uliwekwa bayana kwenye tovuti ya kitengo cha Wizara ya Fedha kinachotekeleza miradi ya MCA. Ili kuongeza uwazi na uwajibikaji ni vizuri serikali ingepanua utaratibu wa miradi ya MCA na kuutumia kwenye miradi yake yote.

Serikali iwe na nidhamu katika mambo ya bajeti. Vitabu vyote vinne vya bajeti viwekwe kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.