Thursday, November 9, 2017

Utengenezaji mvinyo wa nyanya unatuweka mjini

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi; asimtowe@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa waliozoea kutumia nyanya kama kiungo cha mboga hawawezi kuamini kuwa huwa zinatumika kutengeneza mvinyo, kimiminika maridhawa kwa wanywaji.

Mvinyo huu ni mchanganyiko wa nyanya, malimao na machungwa. Unatengenezwa Tanzania kwa ajili ya Watanzania. Unaweza usiwe maarufu kwa wengi lakini wakazi wa Makambako wanaufahamu.

Mvinyo huo ni fahari ya Kikundi cha Muungano kilichopo mji mpya wa Makambako mkoani Njombe ambacho kilipata umaarufu katika maonyesho ya wajasiriamali wanawake yaliyofanyika jijini hapa mwezi uliopita, Oktoba.

Wanywaji waliozoea kutumia mvinyo kutoka nje walipoujaribu walikiri ‘hauna tofauti na unaotengenezwa nje ya nchi licha ya kuwa viambata vilivyotumika ni vya asili.’

Ofisa wa Masoko w akikundi hicho, Alice Lugenge anasema mbali na kutumia nyanya, malimao na machungwa, majani ya chai pia hutumika kwa ajili ya kuweka rangi katika mvinyo huo.

Mafanikio yao, anasema yamekuja baada ya kufundishwa utengenezaji na wataalamu wa Shirika la Kusaidia Viwanda Vidogo (Sido) na kwa miaka mitatu wamekuwa wakitengeneza mvinyo huo na kufanikiwa kuimarisha uchumi wa kila mwanachama.

“Tulianza watu 30 lakini tumebaki watatu kutokana na taratibu za utengenezaji wa mvinyo huu hutumia muda mrefu. Wengi walishindwa kuvumilia na tumebaki wenye nia tu,” anasema Ludende

Anasema watu wengi wanapenda kuona faida baada ya muda mfupi jambo linalowafanya washindwe kuvumilia na kuona ujasiriamali hauna faida.

Anasema mpaka uwe tayari, mvinyo huo hutumia siku 21 baada ya hatua zote kukamilika.

“Tumia nyanya zilizoiva. Tunazizisafisha mara mbili; kwa maji ya baridi baadaye yaliyochemka kisha tunazikata moja baada ya nyingine kujiridhisha hakuna mbovu inayoweza kuharibu mvinyo. Tukimaliza kukata tunasaga na kuipika juisi yake,’’ anasema Ludende.

Baada ya kupikwa hupozwa na kuchanganywa na juisi ya limao na machungwa na kuhifadhiwa kwa siku 21 ndipo huwa tayari. “Kwa mfano kama una lita 10 za uji wa nyanya utatumia machungwa 21 na malimao 21 ili kuweka uwiano sawa na majani ya chai kidogo,” anasema Ludende.

Ukishakamilika, kikundi hicho kinajivunia soko lake lililopo Mbeya, Songea, Morogoro hata Dar es Salaam. Hata hivyo, anasema mwamko wa watu kuutumia mvinyo huo bado ni mdogo kwa sababu wengi wanapenda kutumia ya nje. “Tunatengeneza kiasili, hatutumii kemikali yoyote na kiwango chake hakina tofauti na ile iliyotoka nje ya nchi,” anasema Ludende

Anasema mvinyo huweza kutumiwa na watu wenye kisukari kwa sababu hupunguza tatizo hilo, hutoa mafuta mwilini, husaidia mmeng’enyo wa chakula na huongeza hamu ya kula.

Anasema wana uwezo wa kutengeneza lita 200 kila baada ya wiki mbili. Katika lita 160, wanapata chupa 168 ambazo huuzwa kwa Sh10,000 kila moja. Kutokana na mauzo ya mvinyo huo, anasema kwa mwezi wanaingiza mpaka Sh3 milioniinayotosha kutimiza mahitaji yao. “Tungekuwa na vitendea kazi vya kisasa tungeweza kuvundika hadi lita 10,000 na baada ya hapo tungekuwa tumeongeza uzalishaji mara nyingi zaidi ya uliopo,” anasema Ludende.

Kikundi hicho kina vibali vyote vya Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hivyo kuwa na uhuru wa kufanya biashara sehemu yoyote wakiwa na uhakika wa salama wa wanachokifanya.

-->