Utoro unavyozalisha wanafunzi mbumbumbu wilayani Kilindi

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Majengo wakicheza katika viwanja vya shule. Walimu wanalalamika utoro mkubwa wa wanafunzi, jambo linalochangia wanafunzi wengi kutojua stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.  Picha na Abeid Poyo.

Muktasari:

Hivi sasa katika shule nyingi nchini, uwiano wa wanafunzi na vitabu unakaribia 1:1, yaani mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.

Pongezi kwa Serikali kuhakikisha vitabu sio kitu adimu tena shuleni.

Hivi sasa katika shule nyingi nchini, uwiano wa wanafunzi na vitabu unakaribia 1:1, yaani mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.

Hiki ndicho kilichopo katika Shule ya Msingi Majengo iliyopo Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Wanafunzi wa darasa la pili shuleni hapo wapo darasani.

Juu ya madawati kumejaa vitabu vya somo la Kiswahili. Karibu kila mwanafunzi ana kitabu chake kilichoandikwa: Najifunza kuandika.

Wanafunzi hawa wamebakisha siku chache kuingia darasa la tatu, ngazi ya elimu ambayo inatarajiwa kila anayebahatika kuifikia awe tayari ameshazijua stadi muhimu za kusoma, kuandika, kuhesabu na hata kufanya hesabu rahisi.

Hata hivyo, hali haiko hivyo katika darasa hili la watoto 164. Naamua kuwapitia baadhi ya wanafunzi ili kupima uwezo wao wa kujua kusoma.

Namuonyesha mwanafunzi mmoja sentensi hii: ‘Nyumba inafanyiwa matengenezo’. Anayatazama maandishi kwa sekunde kadhaa, hakitoki kitu mdomoni mwake, na kadri muda unavyoyoyoma, nabaini kuwa sentensi hiyo imemshinda.

Mwingine namtaka anisomee sentensi: ‘Amina ni mwanafunzi’ Huyu hakusubiri kupoteza muda, kwa haraka akakiri kuwa hajui kusoma.

Kwa mujibu wa mwalimu wa darasa, Jenny Msigwa, hali hiyo sio jambo geni kwao, kwani katika darasa hilo la wanafunzi 164 wanaojua kusoma hawazidi 20.

Utoro unatajwa kama sababu kuu inayochangia maendeleo duni ya taaluma. Mwalimu Msigwa anasema karibu nusu ya wanafunzi wa darasa hilo ni watoro wa kudumu.

Kibaya zaidi kwa mujibu wa walimu, sio wazazi wala viongozi wa serikali ya kijiji wanaoonyesha dhamira ya dhati ya kuisaidia shule kupambana na hali hiyo.

‘’ Wazazi hawana ushirikiano, wanatukatisha tamaa, tumeamua kupambana na hali zetu. Ukiona anayejua kusoma basi ni yule anayekuja shule kila siku,’’ anasema mwalimu Msigwa anayelalamikia pia idadi kubwa ya wanafunzi, jambo linalompa wakati mgumu kumpitia kila mwanafunzi wakati wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mazingira yanavyochangia

Pamoja na utoro kutajwa kuwa sababu ya wanafunzi hao kutojua kusoma, mazingira ikiwamo miundombinu shuleni sio rafiki. Darasani wanafunzi wanasongamana.

Wanafunzi wanasema hawapati chakula cha mchana, licha ya walimu kusema kuwa wamekuwa wakiwapatia uji mchana.

Shule ina mashamba ya mazao kadhaa yakiwamo maharage na miembe. Wakati wa msimu, angalau embe hutumika kupunguza ukali wa njaa kwa wanafunzi.

Kwa maharage, mwalimu Ezekiel anasema mapato ya mavuno yake hutumika kugharimia baadhi ya masuala ya uendeshaji wa shule.

Mkakati wa shule

Mwalimu Mkuu, Joel Ezekiel, anasema wameamua kuushirikisha uongozi wa kijiji uwasaidie kuhusu kadhia hiyo kwa kupeleka majina ya wanafunzi watoro. Hata hivyo, analia ushirikiano mdogo wanaoupata walimu.

‘’ Tumechukua hatua ya kupeleka orodha ya wanafunzi watoro kwa hatua ya awali. Nasikitika bado hawajachukua hatua yoyote. Nilitaka nipeleke orodha nyingine lakini ile ya awali haijafanyiwa kazi na sijapewa jibu wamefikia wapi,’’ anasema.

Awali mwalimu Ezekiel anasema kwa kupitia vikao na wazazi waliamua kuweka adhabu ya Sh 1000 kwa kila siku ambayo mtoto atatoroka shule, suala analosema mwishowe halikuwa na tija.

Mmoja wa wazazi, Msekwa Mbotwe, anasema tangu mwaka 2017 uanze hajawahi kukanyaga shule iwe kwa kuhudhuria vikao au kufuatilia maendeleo ya mwanawe.

Kuhusu sababu ya kutofanya hivyo, anasema:’’ Sijawahi kuletewa barua ya kutakiwa kwenda shule.’’ Kwa Mbotwe, elimu ya mtoto wake ni mpaka aletewe barua kutoka kwa walimu!

Mwalimu Ezekiel anasema wanapoitisha mkutano katika shule hiyo yenye wanafunzi takriban 970, wazazi wanaohudhuria hawazidi 50!

Uongozi wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo anasema wanajitahidi kupunguza wimbi la wanafunzi kutoroka shule. Utoro uliopo sasa ni ule anaouita; ‘ utoro wa rejareja’ ambao pia wanaushughulikia.

‘’Hali ya utoro inapungua, bado upo utoro wa rejareja tunaoushughulikia. Kama Serikali tunaendelea kuwahamasisha. Nikienda katika vikao nawahamasisha kuhusu elimu kuwa ni wajibu wao,’’ anaeleza.

Mwamko mdogo wa elimu

Kilindi ni kati ya maeneo ambayo wakazi wake wengi bado hawajatambua thamani ya elimu kwa watoto wao.

Kwa Kilindi, uchunguzi mdogo wa Mwananchi, umebaini kuwa sio tukio geni kwa mzazi kumshtaki mwalimu au kumpa vitisho kwa kuwa tu amemrudi mwanawe mwenye matatizo ya kinidhamu.

Mwalimu mmoja (jina tunalihifadhi), anasema baadhi ya wazazi wamefikia hatua ya kujenga uadui na walimu.’’

‘’Kijijini kitu anachouziwa mwanakijiji mwingine kwa Sh 500 mimi mwalimu nauziwa kwa Sh 700, maji ya Sh 300 mimi napandishiwa bei,’’anasema mwalimu huyo.

Uchunguzi unaonyesha wakazi wengi wa wilaya hii iliyomegwa kutoka Wilaya ya Handeni, hawajasoma au wameishia darasa la saba.

Tatizo la kitaifa

Bila shaka wanafunzi wa Shule ya Msingi Majengo, ni kiashiria cha kuwapo kwa wanafunzi wengi nchini wanaovuka darasa la pili wakiwa hawana stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK.

Mfumo wa elimu nchini unamtarajia mwanafunzi wa darasa la pili awe na uelewa wa kutosha wa stadi hizo muhimu katika mchakato wa ujifunzaji na maisha kwa jumla.

Kisa cha shule hii kinashadadiwa na matokeo ya mara kwa mara ya tathmini za Uwezo zinazofanywa na asasi isiyo ya kiraia ya Twaweza.

Aghalabu, tathmini hizo zinazojumuisha watoto wenye umri kati ya miaka saba hadi 16, hubaini kuwapo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wakiwamo wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kwa mfano, matokeo ya tathmini ya mwaka 2015 iliyojumuisha watoto 32,694 kutoka kaya 16,013 na shule za msingi 1,309, yanaonyesha baadhi ya watoto wa darasa la saba walishindwa kufanya majaribio ya darasa la pili.

‘’Wanafunzi wanne kati ya 10 (sawa na asilimia 44) hawawezi kusoma hadithi ya Kingereza ya kiwango cha darasa la pili, wawili kati ya 10 (asilimia 16 ) hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili, na wawili kati ya 10 (asilimia 23 ) hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la pili,’’ inasema sehemu ya ripoti yab tathmini hiyo iitwayo; Je watoto wetu wanajifunza? Hali ya Elimu nchini Tanzania mwaka 2015.