Uwezekano wa vita Korea Kaskazini waongezeka

Muktasari:

Kila baada ya miaka michache vichwa vya habari duniani hunadi: “Korea Kaskazini iko ukingoni mwa vita.” Watu wenye uzoefu wa kufuatilia mambo katika nchi hiyo hawashtushwi na habari hizo. Wameshazizoea. Lakini mara hii mambo yanaweza kwenda vingine. Kuna uwezekano wa kuzuka mzozo wa kijeshi katika Korea. Si masihara. Hii inatokana na mambo mawili mapya yaliyochomoza, kufanikiwa programu ya nchi hiyo ya kutengeneza maroketi ya masafa marefu, na pia Donald Trump kukamata urais wa Marekani.

Iko hatari ya kweli ya uwezekano wa kutokea vita katika Korea Kaskazini. Hii si dhihaka. Na ikiwa hakutapatikana suluhisho katika mgororo wa eneo hilo, basi mzozo wa kiuchumi pia utaweza kusababisha kuzuka uasi wa kimapinduzi huko Korea Kaskazini. Matokeo yake? Hamna mtu anaweza kuyatabiri.

Kila baada ya miaka michache vichwa vya habari duniani hunadi: “Korea Kaskazini iko ukingoni mwa vita.” Watu wenye uzoefu wa kufuatilia mambo katika nchi hiyo hawashtushwi na habari hizo. Wameshazizoea. Lakini mara hii mambo yanaweza kwenda vingine. Kuna uwezekano wa kuzuka mzozo wa kijeshi katika Korea. Si masihara. Hii inatokana na mambo mawili mapya yaliyochomoza, kufanikiwa programu ya nchi hiyo ya kutengeneza maroketi ya masafa marefu, na pia Donald Trump kukamata urais wa Marekani.

Trump ameifanya Korea Kaskazini kuwa moja ya sehemu muhimu ya masuala ya siasa zake za kigeni. Msimamo wake kuhusu kadhia hiyo ni wa uchokozi, hana msalie mtume. Kuna ishara kwamba Trump na duru inayomzunguka wanafikiria kufanya hujuma ya kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.

Pia, kuna uwezekano mkubwa kwamba hujuma kama hiyo itapelekea kuzuka vita vikubwa. Trump hatishiki na uwezekano huo.

Hata hivyo, Serikali ya Marekani inashughulika kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo. China, ambayo nayo hadi sasa ilijizuia kujiunga katika kuiwekea vikwazo vikali Korea Kaskazini, sasa imeamua kujiunga katika kuvitekeleza vikwazo hivyo.

Vikwazo hivyo vinakataza aina yeyote ya mabadilishano ya kiuchumi na Korea Kaskazini, hivyo kuinyima nchi hiyo fedha za kigeni. Pia, vinaingiza kupiga marufuku biashara baina ya Korea Kaskazini na nchi za nje, na jambo hilo ni muhimu sana kwa vile asilimia 80 ya jumla ya biashara ya kigeni ya Korea Kaskazini ni pamoja na China.

Sasa China itabidi ihakikishe kwamba biashara hiyo inasita. Hapo kabla China ilikuwa kila wakati ikihofia kwamba vikwazo vikali vitaweza kusababisha mzozo wa kisiasa ndani ya Korea Kaskazini. Viongozi wa China, kutokana na hamu ya viongozi wa Marekani kutaka kuendesha vita huko Korea, wanahisi kuporomoka utawala huko Korea Kaskazini ni hatari iliyo ndogo zaidi ikilinganishwa na hatari ya kuzuka vita vikubwa vya kimataifa ambavyo vinaweza kutokana na hujuma ya Marekani.

China itaendelea kushiriki katika vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, basi nafasi itazidi kwa Trump kuliahirisha shambulio lake hadi pale wakati ambapo athari za vikwazo zitakuwa zinaonekana wazi kabisa.

Vikwazo katika mfumo wake wa sasa havitoi suluhisho la kudumu. Ni kazi bure kutaja, lakini kila mtu anatambua kwamba serikali ya Korea Kaskazini haitaachana na silaha zake za kinyuklia.

Viongozi wa Korea wanatambua nini kilichompata Muammar al-Gaddafi wa Libya – mtu pekee aliyekuwa na nguvu na ambaye katika historia alikubali kuachana na programu yake ya kinyuklia na badala yake kupewa vivutio vya kiuchumi.

Pia, watawala wa Korea Kaskazini wanatambua yale yaliyomfika Rais Saadam Hussein wa Iraq. Israel ilikishambulia kutoka angani kinu cha kinyuklia cha Iraq.

Kwa hivyo, Korea Kaskazini imepata somo na katu haitoachana na mpango wake wa kinyuklia, hata kama vikwazo inavyowekewa vitapelekea kuzuka njaa kubwa miongoni mwa wananchi wake. Kwa vyovyote vile, ni raia wa kawaida ndio watakaokumbana na njaa na si watawala wanaotoa maamuzi.

Hadi sasa vikwazo havijauma, havijawa na athari kubwa. Lakini hilo ni suala la wakati tu, ni kungoja na kuwa na subira. Katika miaka mitano iliyopita uchumi wa Korea Kaskazini umepanda juu, lakini pindi fedha za kigeni zitakapokuwa haba kupatikana, basi uchumi utakwenda chini tena.

Nini ambacho kinaweza kikatokea baadaye? Pindi kutatokea mzozo au njaa kubwa, basi wananchi wa Korea Kaskazini hawatakuwa na la kufanya. Watabakia wanaumia na kufa kimyakimya. Uasi wowote kutoka upande wa raia utamaanisha sawa na raia hao kujiua wenyewe. Pindi wananchi watalalamika na kuandamana basi utawala utawatandika.

Viongozi wa Korea Kaskazini pamoja na tabaka la juu huenda watu milioni moja wanachukulia kwamba kusambaratika kwa utawala huo kutapelekea kuungana tena Korea mbili, ya Kusini na ya Kaskazini. Kwa hivyo, katika hali hiyo watu wa tabaka hilo hawatakuwa tena na mustakabali wa kisiasa. Zaidi ni kwamba kuna hatari watu hao wakaishia magerezani au kuuawa kutokana na kushiriki au kudaiwa kushiriki katika uvunjaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wa ukoo wa Kim.

Pia kuna uwezekano, japokuwa mdogo, kwamba mzozo mkubwa wa kiuchumi katika Korea Kaskazini utasababisha uasi wa kimapinduzi. Mapinduzi ya aina hiyo yatakuwa ya aina nyingine kabisa, tofauti na “mapinduzi malaini” yalioshuhudiwa Ulaya Mashariki mwishoni mwa miaka ya themanini.

Watawala wa Korea Kaskazini wanajua fika kwamba pindi utakuja mfumo mpya wa utawala nchini humo, basi wao wataishia gerezani au kwenye vyumba vya kungoja kunyongwa.

Kinyume na wakuu wa vilivyokuwa vyama tawala katika miaka ya thamanini huko Ulaya Mashariki, wao hawatakabidhi madaraka kwa njia ya salama, bali watapigana hadi dakika ya mwisho, hadi kufa.

Mapinduzi huko Korea Kaskazini yatapelekea vurugu kama ile tunayoiona hivi sasa huko Syria, kukichomoza wababe wa kivita watakaopigania madaraka, huku wakitafuta waungwe mkono na madola makuu. Kwa hakika, China, Urusi, Korea Kusini na Marekani zitajiingiza katika mzozo huo, kwa namna moja au nyingine. Zaidi ya hayo, vurugu hiyo itaathiri nchi hiyo licha ya silaha zake za kinyuklia na nyingine za maangamizi. Kwa hiyo mustakabali wa Korea Kaskazini ni wa kiza zaidi.