Uzuri na ubaya wa mbolea za viwandani

Muktasari:

Madini mengine muhimu ni salfa, chokaa, magneziam, boroni, shaba, zinki, molybedenum, chuma na mengineyo.

Mbolea ni chakula cha mimea ambacho ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mmea kwa kiasi kikubwa kama vile naitrojeni, fosiforasi na potashi. Haya yanahitajika kwa kiasi kikubwa na ndiyo mana kila mbolea inayotengenezwa kiwandani huwekwa madini haya muhimu matatu.

Madini mengine muhimu ni salfa, chokaa, magneziam, boroni, shaba, zinki, molybedenum, chuma na mengineyo.

 

Mbolea za viwandani

Hizi ni mbolea zinazotengenezwa kiwandani kisasa na kuwekewa kiwango maalumu cha virutubisho muhimu katika ukuaji bora na uzalishaji bora wa mmea. Mfano wa mbolea hizi ni kama CAN, Urea, DAP na nyinginezo.

Kama tulivyowahi kuona katika safu hii kuwa mmea unahitaji virutubisho 16, lakini kuna vinavyohitajika kwa kiasi kikubwa na vingine ni kiwango cha kawaida.

Mmea unaweza kushindwa kukua vizuri kwa kudumaa, kuwa na rangi ya njano au ukashindwa kuzalisha vizuri kwa kukosa virutubisho vinavyohitajika kwa kiasi kikubwa kwa ukuaji wa mmea.

Virutubisho hivyo muhimu ni naitrojeni, fosiforasi na potashi. Kila mbolea ya dukani ambayo itatengenezwa huwekwa virutubisho hivi vikuu vitatu kwa uwiano tofauti kutokana na mahitaji ya mmea. Kwa mfano, kuna mbolea zenye naitrojeni kwa wingi kama vile CAN (27:0:0). Uwiano huo una maana kuwa naitrojeni (27), fosiforasi (0) na potash (0).

Hivyo, mkulima ajiulize anapoweka naitrojeni kwa wingi, anajua kazi yake kwa mmea? Naitrojeni ndiyo inayotengeneza kijani kibichi katika mmea.

Mfano wa pili ni mbolea ya DAP; hii ina fosiforasi kwa wingi (18:46:0). Uwiano huo una maana kuwa naitrojen (18), fosiforasi (46) na potasiam (0).

Tunawashauri wakulima watumie DAP kupandia kwani mmea kwa maisha ya mwanzo kabisa unahitaji fosiforasi kwa wingi. Hii ni faida moja kubwa kwa mbolea za viwandani dhidi ya mbolea za asili.

Mkulima anayetumia mbolea asili, hawezi jua kiwango cha naitrojeni wala potash anachoweka kwenye mmea wake.

Faida za mbolea za kemikali

1.Hufanya kazi kwa haraka, Ni rahisi mno kuokoa mmea unaokaribia kufa kutokana na ukosefu wa virutubisho.

Hii ni kwa sababu virutubisho vilivyopo katika mbolea za kemikali huwa rahisi kufyonzwa na mmea mara moja baada ya mbolea hii kuwekwa kwenye mmea. Mara nyingi huwa katika hali ya chenga chenga hivyo mkulima akishamwagilia maji mmea wake kisha akaiweka umbali wa sentimita nne kuzunguka mmea huyeyushwa na kufyonzwa na mmea moja kwa moja.

2.Upatikanaji rahisi: mbolea hii ni rahisi kupatikana katika maduka ya pembejeo na maeneo mengine..

3.Hutumika kidogo tu: Kwa ekari moja kwa mfano wakati wa kupandia mfuko mmoja wa kilo 50 unaweza kutosha kwa baadhi ya mazao kwa kuwa uwekaji wake ni gramu tano kwa shimo.

Lakini kwa mmea unaokaribia kutoa maua mpaka mifuko miwili ya kilo 50 inaweza kutumika kwani hapa mkulima atahitajika kuweka gramu 10 kuzunguka mmea.

4. Ina virutubisho muhimu vinavyohitajika katika mmea na mkulima hutambua ameweka kiasi gani. Mkulima hujua anaweka naitrojeni kiasi gani, fosiforasi kiasi gani na potashi kiasi gani. Mkulima anayetumia mbolea za asili hawezi kujua kaweka virutubisho kiasi gani kwenye udongo wake.

 

Wito

Mbolea hii ni nzuri kama itatumiwa na mkulima kwa muda mfupi na siyo kutumia kwa muda mrefu, kwani ina athari kwenye rutuba ya udongo.