VAT iendane na dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda nchini

Muktasari:

Ni mfumo unaostahili kuachwa uendelee lakini marekebisho yafanywe, kwa kushirikisha wadau, popote penye upungufu uliobainishwa.

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) imekuwa ikitumika nchini takriban miaka 20 sasa. Ni muda mrefu wa kutosha kujifunza panapohitaji marekebisho.

Ni mfumo unaostahili kuachwa uendelee lakini marekebisho yafanywe, kwa kushirikisha wadau, popote penye upungufu uliobainishwa.

Ili mfumo huo wa kodi uendane na dhamira ya Serikali kujenga uchumi wa viwanda nchini, maridhiano kati ya walipaji na wakusanyaji kodi ni muhimu.

Kiwango cha VAT kilichotumika miaka ya 1997, kodi hiyo ilipoanza kutumika kilikuwa asilimia 20, lakini kwa sasa ni asilimia 18. Mabadiliko hayo yamefanywa ndani ya miongo miwili tangu kuanzishwa kwake.

VAT ni kodi anayotozwa mlaji au mnunuzi wa mwisho wa bidhaa au huduma.

Yeye ndiye anayebeba kodi hiyo kutokana matumizi anayoyafanya. Hilo hufanyika baada ya bidhaa au huduma husika kutozwa kodi nyingine katika hatua mbalimbali kabla haijamfikia.

Hakuna anayejua kwa hakika katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, utozaji wa VAT umechangia kiasi gani kuimarisha viwanda au kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Hakuna anayefahamu mchango wa VAT kurudisha nyuma juhudi za kukuza viwanda au kuchochea mfumuko wa bei hatimaye kuzidisha kiwango cha umaskini nchini.

Katika hali ya kawaida, VAT inatakiwa iakisi wastani wa kodi mbalimbali ambazo zingetozwa tofauti kwa kila aina au makundi ya bidhaa zinazowiana matumizi.

Kodi siyo nyenzo pekee ya kukusanya mapato ya Serikali. Muhimu zaidi ni nyenzo hiyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kulinda viwanda vya ndani bila kusahau kuvipa msukumo wa uzalishaji na kupanua uwekezaji.

Kodi inadhibiti kasi ya mfumuko wa bei, inalinda kipato cha wafanyakazi hususan wa kipato cha chini na mapato ya wafanyabiashara kutoka sekta zote za uchumi.

Wakati matumizi ya VAT yanaanza nchini mwaka 1997, kiwango kilichowekwa cha asilimia 20 kilikuwa kikubwa kikilinganishwa na mataifa mengine yaliyokuwa yanatumia mfumo huo kukusanya mapato.

Ujerumani walioanza kutumia VAT mwaka 1968 ilikuwa ni asilimia 11 ambayo ilipanda mwaka 1984 na kufikia asilimia 14. Kiwango hicho kilipanda mpaka asilimia 16 kati mwaka 2002 hadi 2006 na kilifika asilimia 19 kuanzia mwaka 2009.

Japan walianza matumizi ya kodi hiyo mwaka 1989 kwa asilimia tatu. Kuanzia mwaka 2002, VAT ilipanda hadi asilimia tano nchini humo.

Canada walioanza kutumia VAT mwaka 1991 kwa kiwango kikiwa asilimia saba ilipunguza mwaka 2008 mpaka asilimia tano.

Korea walianza mwaka 1977 wakitoza asilimia 10 kiasi ambacho kilidumu kwa muda mrefu hadi mwaka 2010.

Australia ilikuwa inatoza asilimia 10 mwaka 2000 ilipoanza kutumia mfumo huo. Kiasi hicho kilidumu mpaka baada ya miaka ya 2010.

Switzerland ilianza kutumia VAT mwaka 1995 kwa kutoza asilimia 7.6 na kudumu nayo hadi mwaka 2010 na kuendelea.

Huko Uingereza, walianza mwaka 1973 ila mpaka mwaka 1976 ilikuwa inatoza asilimia nane.

Mwaka 1980 kodi hiyo ilipanda mpaka asilimia 15 na mwaka 1992 ikawa asilimia 17.5 kabla haijashuka mpaka asilimia 15 mwaka 2009 ingawa kilipanda tena mwaka uliofuata na kubaki asilimia 17.5.

Ukichukua wastani kwa nchi za Ulaya, kati ya mwaka 1976 hadi 2008, VAT iliyotozwa ilikuwa kati ya asilimia 16 na 17.6. Na baada ya mwaka 2010 wastani ulikuwa asilimia 18.

Kabla ya hapo kila nchi ilikuwa na viwango tofauti vya kodi kwa makundi au aina maalumu za bidhaa kulingana na sera zake za kiuchumi.

Yapo mengi ya kuyazungumza kuhusu VAT. Ninachojaribu kukieleza au kukihoji ni nchi zinazotofautiana viwango vya maendeleo kwa kila sekta ya uchumi kuwa na kiwango sawa cha kodi.

Ukiangalia VAT inayotozwa nchini inalingana au kukaribiana na wastani wa mataifa ya Ulaya.

Hapa ndipo panapohitaji tafakuri na tathmini ya madhara ya suala hilo kwa uchumi wa nchi changa na zenye msingi duni wa viwanda kama ilivyo Tanzania.

Ikibainika faida ni chache kutokana na wadau muhimu kwenye suala hili au kwa kulinganisha na nchi nyingine zinazoendelea, itapendeza iwapo mamlaka husika zitachukua hatua na kurekebisha kasoro zilizopo.

Suala hili ni muhimu hasa kwa kuzingatia kwamba mapato ya Serikali yanatokana na kodi na tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara na watumishi wa sekta zote ambao ni lazima wawe na kipato. Ili kuhakikisha shughuli hazisimami na Serikali inaendele kukusanya inachostahili ipo haja ya kuweka mazingira yatakayohakikisha biashara zinashamiri.

Ushirikishaji ukiwapo, hilo litawezekana. Viwango vinavyoendana na mazingira halisi ya wafanyabiashara nchini vitaongeza wigo na kutunisha hazina ndani ya muda mfupi na kuiwesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo.