Monday, March 20, 2017

Vanesa Mansilla anavyoogelea noti za Tevez

 

Alhamisi, Desemba 22, 2016. Carlos Tevez akiwa kwenye suti yake ya rangi ya bluu mpauko, muda wote alikuwa akitabasamu tu huko San Isidro, kitongoji kilichopo jirani na mjii mkuu wa Argentina, Buenos Aires.

Tabasamu halikuiacha sura yake. Alitabasamu zaidi kila alipotazama ubavu wake wa kushoto. Alizidi kutabasamu, kwa sababu huo kulikuwa na mrembo bomba kabisa, Vanesa Mansilla. Wakawa wanatazamana, wakawa wanatabasamu pamoja. Haikuwa maigizo, na kwa taarifa tu siku hiyo ilikuwa muhimu kwao kwani wawili hao walioanza kupendana ndani utotoni, walikuwa wakifunga pingu za maisha.

Tevez hakuwa na chaguo jingine zaidi ya kumbeba jumla tu, kipenzi cha moyo wake, ambaye ni mama wa watoto wake watatu, wakiwamo mabinti, Florencia na Katie.

Si unajua Muargentina huyo kwa sasa ndiye mwanasoka anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani, lakini hilo halijawahi kuwa kishawishi kwa mrembo Vanesa kukubali kuolewa na staa huyo, licha ya kwamba kwa sasa atakuwa anaogelea tu pesa.

Kwa taarifa yako, si kwamba mrembo Vanesa alitega mtego wa pesa kwa Tevez, la wawili hao walikutana, tangu Tevez alipokuwa na umri wa miaka 13. Walibaki kuwa pamoja wakati Tevez akihangaika huku na kule, ikiwamo kwenda kucheza soka Corinthians, West Ham United, Manchester United, Manchester City na Juventus.

Hata kipindi kile ambacho Tevez alitoweka klabuni Man City, hata kipindi kile ambacho Tevez alitibuana na kocha mwenye nguvu kubwa kwenye soka, Sir Alex Ferguson, mrembo Vanesa alikuwa nyuma yake. Kwa maana hiyo hajadandia treni kwa mbele, anachovuna Tevez kwa sasa kinamhusu pia kwa uvumilivu wake.

Amevuka kwenye vigingi vyote vya kipindi cha ujana wa Tevez hadi wanafikia kufunga pingu za maisha, wakati Tevez akiwa na umri wa miaka 32. Kumbuka, mwaka 2010, Tevez aliripotiwa kuwa na uhusiano na mwanamitindo Mariana Paesani na baadaye mwigizaji, Brenda Asnicar, lakini Vanesa hakujali, alisubiri wakati wake na hatimaye amemnasa Tevez jumla jumla.

Katika kulifanya tukio la kuoana linakuwa pekee kabisa kwa upande wao, Tevez alipanga kufanya sherehe kwa siku nne na kutoa mwaliko kwa watu 260. Tevez alikuwa na jeuri ya kufanya hivyo, kwa sababu wakati huo kulikuwa na dili la pesa nyingi lilikuwa kiliendelea kwenye mazungumzo kwa ajili ya kwenda huko China.

Si unajua ukiweka kando mpira, Tevez ni mwanamuziki mzuri tu. Ni mwimbaji kwenye kundi la Piola Vago, sambamba na ndugu yake, Diego. Wimbo maarufu zaidi wa kundi hilo unaitwa ‘Lose Your Control’ ambao ulishika chati za juu huko Argentina.

Basi wakati mwingine, Tevez anatumia umahiri wake wa kuimba kumshushia mashairi mrembo Vanesa. Chezea Tevez wewe!

Uvumilivu wa Vanesa umempa matunda. Labda pengine alitazama mbele zaidi, hivyo acha tu kwa sasa aoge mihela ya mwanasoka huyo.

Unajua kwanini tunasema aoge mihela ni kwa sababu mshahara anaolipwa mumewe huko kwenye timu yake mpya ya Shanghai Shenhua, inayoshiriki Ligi Kuu China.

Kutoka Alhamisi ya harusi yake na mrembo Vanessa, hadi Alhamisi ya Desemba 29 mwaka jana, Tevez tayari alikuwa amenyakua dili hilo la Shanghai, ambalo linafichua kwamba mshahara wake wa wiki ni Pauni 615,000.

Ndiyo! Pauni 615,000 kwa wiki sawa na shilingi za Kitanzania 1.6 bilioni. Sh1.6 bilioni kwa wiki. Zidisha mara mwezi, zidisha mara mwaka. Huo ndiyo mzigo anauvuta Tevez. Mkwewe atafanya shopping hadi atachoka mwenyewe.

Usisahau pia, Tevez hakuwa na mshahara wa kitoto alipokuwa akizichezea klabu za Man United na Man City. Hata alipokwenda Juventus, ambako mishahara ya Italia ilikuwa chini ukilinganisha na England, lakini fowadi huyo alikuwa kwenye kundi la wachezaji waliokuwa wakilipwa mshahara mnene.

Walikoanzia Vanesa na Tevez baada ya kukutana wakiwa na umri wa miaka 13, walipofika umri wa miaka 19, wanadaiwa wenyewe tu walifunga ndoa ya kivyao kabla ya Desemba mwaka jana kuamua kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki. Umri wa Tevez kwa sasa ni miaka 33, ambayo alitimiza Februari 5 mwaka huu.

Sherehe nyingine ya ndoa yao waliifanya huko Uruguay na hawakutaka kuweka kificho ambapo walitembelea mitaani na kuwaonyesha watu waliokwenda kushuhudia cheti cha ndoa yao. Na sasa kwa mkwanja ambao Tevez anakusanya kila kitu, mrembo Vanesa ataweza kununua na kumiliki kila kitu kinachoweza kununulika kwa pesa ambacho kipo kwenye matamanio yake.

Atake nini? Kwa mkwanja huo, pesa ya mwezi tu anaweza kununua gari analotaka, boti ya kifahari na hata ndege binafsi ya kwenda kuwapigia bakora marafiki zake.

Hiyo ndiyo raha anayokutana nayo mrembo Vanesa kwa sasa. Kuhusu mapenzi hakuna mashaka, kama walianza pamoja wakiwa na umri wa miaka 13 hadi kufikia ndoa, kuna nini tena hapo?

Taarifa za kutoka Argentina zinafichua kwamba Vanesa alikuwa kwenye uvumilivu sana kwa sababu karibu miaka sita, Tevez alikuwa akizurura huko Ulaya, wakati mrembo hiyo alikuwa mpweke huko Argentina.

Machi 2010 ilidaiwa kwamba Tevez alijifungia hotelini na mrembo mkali sana kuliko hata Vanesa. Unadhani Vanesa alitetemeka? Alijua tu Tevez ni ndege wake, atarukaruka atarudi tu bandani.

Kuna kipindi alionekana pia asubuhi akitoka kwenye chumba cha mrembo Mariana. Mariana na Muargentina huyo alionekana mara kadhaa kwenye hoteli ya nyota tano ya Kempinski huko Munich, Ujerumani.

Mrembo mwingine anayehusishwa kuwa na uhusiano na Tevez ni mtangazaji wa Televisheni na mwimbaji, Brenda Asnicar.

Mwaka 2008 iliripotiwa kwamba Tevez alifikia hatua hata ya kumtosa Vanesa kisa Mariana baada ya kuwa na uhusiano na mrembo huo kwa miezi mitatu, lakini baadaye waliripotiwa wawili wamerudiana hadi kufikia mwaka jana walipoamua kubebana jumla jumla.

 

Pesa za Tevez

Taarifa za kutoka Argentina zilifichua kwamba Teve anatengeneza Dola 121.7 milioni kwa miaka miwili kwenye mkataba wake ikiwa ni zaidi ya mara ya 20 ya kile alichokuwa akivuna zamani.

Klabu ya Boca Juniors wao walimshukuru Tevez kwa kurejea kwenye timu yao na kufunga mabao 25 katika mechi 56 kitu ambacho ndicho hasa kilichoishawishi Shanghai Shenhua na kwenda kumsajili.

Mshahara wa Tevez, ambao unadaiwa kuwa ni Dola 42 milioni kwa mwaka unaelezwa kumfanya kuwa mwanasoka anayelipwa ujira mkubwa zaidi duniani. Supastaa wa Real Madrid na Ureno, ambaye walikuwa pamoja na Tevez klabuni Man United, anaripotiwa kupokea mshahara wa Dola 23 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi.

Wachezaji wengine walionaswa kwa pesa nyingi na klabu za China ni Mbrazili Oscar, aliyetua kwenye kikosi cha Shanghai SIPG kwa ada ya Pauni 60 milioni. Klabu hiyo ya Shanghai SIPG inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Tottenham Hotspur na Chelsea, Andre Villas-Boas ilimsajili pia Mbrazili mwingine, Hulk kwa ada ya Euro 55.8 milioni, hao ikiwa ni miongoni tu kwa wachezajai walionaswa kwa pesa nyingi na klabu za China.

-->