TEHAMA : Vifaa vipya vya teknolojia vilivyopo sokoni 2017

Muktasari:

  • Xiaoyu Zaijia (Little Fish) au kwa Kiswahili samaki mdogo ni kifaa kinachoweza kujibu maswali kwa kuangalia picha, sauti au maandishi. Samaki mdogo anaweza kucheza muziki, kuonyesha maeneo, kupiga simu na kuongoza vifaa vingine vya ndani ya nyumba.
  • Kifaa hiki kimebuniwa na kampuni ya Kichina inayoitwa Ainemo Inc, ila kinatumia programu iliyotengenezwa na Kampuni ya Baidu.

Mwaka 2017 umeanza na maonyesho mbalimbali ya teknolojia duniani. Makala haya yanaangazia vifaa vya kisasa vilivyoanza kutangazwa Januari mwaka 2017.

Xiaoyu Zaijia (Little Fish) au kwa Kiswahili samaki mdogo ni kifaa kinachoweza kujibu maswali kwa kuangalia picha, sauti au maandishi. Samaki mdogo anaweza kucheza muziki, kuonyesha maeneo, kupiga simu na kuongoza vifaa vingine vya ndani ya nyumba.

Kifaa hiki kimebuniwa na kampuni ya Kichina inayoitwa Ainemo Inc, ila kinatumia programu iliyotengenezwa na Kampuni ya Baidu.

Kampuni zinazojihusisha na usafiri wa baharini wamebuni kifaa cha kuvaa shingoni au kuweka mfukoni kinachoitwa Ocean Medallion. Kifaa hiki kitaweza kumtambua mteja anapokua maeneo yote ndani ya meli, anaponunua vyakula au chochote, kumtafuta rafiki. Kitafungua mlango pale mteja anapokaribia mlango wake hasa kwa walevi.

Ocean Medallion kitaunganishwa na mtandao wa meli kwa kutumia teknolojia ya ‘internet of things’ baadaye mwaka huu.

L’Oreal ni moja ya kampuni kubwa ulimwenguni ya urembo na mwaka huu imekuja na brashi ya kipekee inayoweza kujua kama nywele imekatika kichwani au sehemu yoyote pale inapopitishwa.

Brashi hii inaitwa Hair Coach bei yake ni dola 200. Itakuwa ikitikisika pale itakapogundua nywele zimekatika au kutumia nguvu. Unapomaliza kujichana, itaweza kukupa taarifa zote kwa kutumia simu au kompyuta na kukuambia kama umependeza au la.

Hair Coach imetengenezwa kwa kipindi cha miezi 18 na kampuni ya L`Oreal kwa kushirikiana na kampuni nyingine za Kerastase na Withings.

Kampuni ya LG imezindua jokofu liitwalo Smart InstaView yenye kioo kinachoweza kuonyesha kilichomo ndani na tarehe ya kuharibika au kuisha kutumika (expiration dates ).

Jokofu hili lina kamera maalumu ndani ambayo inatoa taarifa kwa mtu wa nje ili aamue kama ni kuongeza bidhaa ndani au la lakini pia mwenye jpkofu anaweza kujua kwa kutumia simu au kompyuta hata akiwa nchi nyingine. Pia inaweza kumkumbusha mtumiaji tarehe za kuzaliwa na kumbukumbu muhimu.

Flow ni kifaa kilichotengenezwa na kampuni ya Plume Labs kazi yake ni kuangalia uchafuzi wa hali ya hewa kama ni nyumbani, mitaani au popote mtu anapokua. Ina taa maalumu ya kuonyesha viwango vya uchafuzi ili mtumiaji aweze kuchukua tahadhari au hata kuondoka eneo husika kwa ajili ya afya yake. Kifaa kina ukubwa wa nchi 1.5 kwa 3.5, kinaweza kuwekwa katika begi au kiunoni. Taarifa zinazokusanywa na kifaa hiki hutumwa katika simu kwa kutumia programu maalumu.

Ukiwa na Whistle 3 hutohofia usalama wa mbwa au mnyama wako hasa kama amepotea. Kifaa hiki kinavalishwa shingoni mwa mnyama kisha unaweza kuweka umbali ambao mnyama wako anatakiwa awe nawe ili kama akienda zaidi basi upate taarifa na kama akipotea basi unaweza kujua alipo na uende kumfuata.

Kwa wale wafugaji ambao wanategemea kengele, tekinolojia za kisasa kama hizi zinawafaa ili kuweza kudhibiti mifugo yao. Kifaa hiki kinatumia Wi-Fi, Bluetooth, cellular, na GPS ili kurahisisha mawasiliano.

Kufuli ni moja ya teknolojia ya kale kabisa inayoendelea kutumika mpaka karne hii ya 21. Lakini kuna watu wameanza kuboresha ili kuwe na kufuli za kisasa kwa kuweka mfumo wa kutambua alama za vidole.

Kampuni moja ya marekani imekuja na BenjiLock ambayo ni aina ya kufuli yenye mambo yote ya usasa.Unaweza kuamua kutumia funguo au kutumia alama za vidole kufungua kufuli hiyo.