UCHAMBUZI: Vifo vya wajawazito vinaepukika

Muktasari:

Hii ina maana kwamba siku hizi kujifungua ni kufa au kupona. Lolote linaweza kutokea kwa mama au mtoto wake jambo linalofanya maisha ya wanawake wengi kuwa rehani.

Matukio ya kina mama wajawazito kufariki wakati wa kujifungua yamekuwa yakiongezeka kila siku hapa nchini.

Hayo ni pamoja na watoto kufariki mara tu wanapozaliwa na wakati mwingine kufia tumboni kabla ya kuzaliwa.

Hii ina maana kwamba siku hizi kujifungua ni kufa au kupona. Lolote linaweza kutokea kwa mama au mtoto wake jambo linalofanya maisha ya wanawake wengi kuwa rehani.

Jambo ambalo pengine jamii huwa inatarajia kulipokea kwa furaha pale mtoto anapoongezeka kwenye familia huwa linageuka kuwa uchungu baada ya mama au mtoto au wote kufariki kutokana na matatizo ya uzazi.

Takwimu zilizotolewa kwenye ripoti mpya ya Jamii na Afya (DHS) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu 2015/2016, inaonyesha kwamba kuna vifo 556 vya uzazi katika kila uzazi 100,000.

Kiwango hiki sio kidogo hata wala hakipaswi kufumbiwa macho.

Zipo sababu nyingi zinazochangia vifo hivi zikiwamo zile zinazosababishwa na jamii yenyewe kama kuzaa kwenye umri mdogo, utoaji wa mimba na kujifungulia nyumbani au kusubiri uchungu kuwa kwenye hatua ya mwisho, ndipo mjamzito apelekwe hospitali.

Wengi huamini, wanapokuwa kwenye dalili za mwisho wanaweza kufikishwa hospitali na kujifungua salama lakini matokeo yake huwa wanachelewa na mwishowe kuhatarisha afya zao na watoto wao.

Wapo ambao, kwa uzembe tu wanaamini kwamba wanaweza kujifungua salama kwa msaada wa wakunga wa jadi hata kama hawajui namna mtoto alivyokaa tumboni.

Inawezekana kuamini hivyo lakini hatari huja siku inapofika, pale mama anapotakiwa kujifungua na ikabainika kuwa kuna tatizo kwa mfano la mtoto kukaa vibaya.

Aghalabu wakunga wa jadi nyumbaji hawawezi kusaidia badala yake itabidi mama awahishwe hospitalini na akichelewa kupata tiba anaweza kufa.

Inawezekana kabisa kuepuka vifo vya uzazi vinavyosababishwa na uzembe wa aina hii kwa wanawake wenyewe kuwahi hospitali, vituo vya afya au zahanati ili wapewe huduma stahiki.

Jambo jingine linalochangia kuongezeka kwa vifo vya uzazi ni uwekezaji duni kwenye huduma za afya.

Mpaka sasa kuna baadhi ya vijiji havina zahanati na kibaya zaidi, hali ya barabara sio nzuri jambo linaloongeza ugumu kwa wanawake wajawazito kupata huduma za uhakika.

Si hivyo tu, katika baadhi ya zahanati au vituo vya afya hakuna vifaa bora vya kujifungulia. Baadhi ya vituo vinatumia taa za chemli au tochi kuwahudumia wanawake wakati wa kujifungua, jambo ambalo ni hatari.

Licha ya kuwa sera ya elimu inataka huduma za afya kwa mama mjamzito na mtoto kutolewa bure, bado katika baadhi ya hospitali za Serikali, wanawake wanaagiza vifaa vya kujifungulia kama glovu na vingine jambo ambalo pia linazorotesha huduma za afya.

Lakini pia ni wakati kwa wauguzi na wataalamu wa afya kufanya kazi hiyo kwa upendo.

Yapo matukio ya baadhi ya wauguzi kuwa ‘wakali’ wakati mama anapohotaji msaada wa kujifungua huku wakitoa kauli mbaya bila kujua tatizo la mama mjamzito ni nini.

Mfano, mama anapohitaji usaidizi kwa muuguzi huambulia kuambiwa ‘jikaze nani alikutuma’.

Lazima kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuepuka vifo vya wajawazito na watoto vinavyoepukika. Mfano lazima kuacha utoaji mimba holela na mimba za utotoni kwa sababu takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana walio kwenye umri wa mika 15 hadi 19 wamejifungua, jambo ambalo ni hatari hasa kwa umri huo.

Tumaini Msowoya ni mwandishi wa habari wa Mwananchi. [email protected]