Vijana wafia vyama kuliko nchi ni janga la Taifa

Vijana wakicheza mchezo wa drafti. Vijana wengi hutumia muda wao kushiriki michezo mbalimbali na kuzungumzia masuala ya siasa. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Haimaanishi vijana ndiyo wanapaswa kumiliki kila kitu kwa sababu ya wingi wao, hapana. Mantiki ni kuwa dunia na mzunguko wake, ujenzi wake unapaswa kubeba maono ya vijana.

Ulimwengu ni wa vijana. Sababu ni kuwa nyakati zote na katika nchi yoyote, vijana ndiyo tabaka kubwa kuliko makundi mengine ya kiumri. Kwa vile demokrasia ni wengi wape, basi vijana ndiyo wamiliki wa sayari.

Haimaanishi vijana ndiyo wanapaswa kumiliki kila kitu kwa sababu ya wingi wao, hapana. Mantiki ni kuwa dunia na mzunguko wake, ujenzi wake unapaswa kubeba maono ya vijana.

Vijana ndiyo wenye dunia kwa sababu ni tabaka la kati kubwa kati ya mawili. Watoto na wazee wametenganishwa na vijana. Hivyo, vijana wanafaa kuunganisha makundi yote kutokana na ukaribu wao. Upo umbali mkubwa kati ya mtoto na mzee, angalau kijana anakuwa katikati.

Harakati za kupigania uhuru wa mataifa mengi yaliyowahi kutawaliwa na ukoloni zilitekelezwa na vijana. Hata hivyo, baada ya mafanikio ya kukomboa nchi zao, vijana wamekuwa wakiachwa nyuma kwenye nafasi za uongozi.

Kuachwa nyuma kwa vijana kwenye uongozi wa nchi kumetokana na hisia za wengi wao kuwa kufanya siasa ni uzee. Wakati huo wazee hujimilikisha haki ya kuongoza kwa kujenga dhana kuwa vijana bado hawajapevuka kiuongozi.

Siasa inaweza kutafsiriwa kwa maneno mengi lakini kwa sentensi fupi, siasa ni sayansi ya kutawala nchi na watu wake. Fani ambayo inatawala vizazi vyote vilivyopo na kutengeneza matarajio ya vizazi vijavyo inakuwaje haiwafai vijana?

Siasa na vijana Tanzania

Kwa macho unaweza kudhani vijana wameamka na kuchangamkia siasa kwa kutazama uwakilishi bungeni pamoja na harakati nyingi ambazo zinafanywa. Ukweli ni kuwa idadi ni ndogo mno.

Tanzania kama ilivyo mataifa mengine mengi, vijana wao wamejitengeneza kuwa kundi la ufuasi na ushangiliaji. Vijana wamekuwa watu wa kuunga mkono harakati mbalimbali. Hawajipambanui kama kundi la watu ambao wanaweza kufanya mabadiliko.

Tabia ya vijana kuwa washangiliaji imekuwa sugu. Vijana wanatumiwa kubishana kwa mambo ambayo hayajengi utaifa. Wanatumika kupigana, nao wanakubali kutumika na kuharibu mustakabali wao wa kimaisha.

Wazee ambao ni tabaka kubwa linawatumia vijana. Japo kifo kinaweza kumpata yeyote, lakini kwa kutazama hali halisi ya kimaisha, vijana wanakuwa bado na umri mrefu zaidi wa kuishi kuliko wazee kwa wakati husika, kwa hiyo wanapaswa kuilinda nchi kwa nguvu kubwa wanayokuwa nayo.

Mathalan, wewe ni mwenyeji lakini nyumbani kwako anakuja mgeni kisha anakutumia kupaharibu. Nawe unakubali kuharibu wakati unafahamu kuwa mgeni hana muda mrefu ataondoka, kisha utabaki umeharibikiwa na hivyo kupata shida ya kuishi.

Mfano wa mwenyeji kutumiwa na mgeni kuharibu kwao ni sawa na vijana ambavyo hutumiwa na wazee wakati inafahamika kuwa wazee wapo ‘magharibi’ na vijana ndiyo kwanza ‘saa sita adhuhuri’.

Huo mfano wa mwenyeji na mgeni haumaanishi kuwa wazee ni waharibifu, la hasha. Wazee wanahitajika sana, lakini nchi hazipaswi kujengwa kwa kufuata maono ya matakwa yao, bali matakwa ya vijana ambao wanao umri mrefu zaidi wa kuishi.

Vijana hawapaswi kuwa mashabiki wa wazee wanapofanya uamuzi juu ya nchi, bali wanatakiwa washiriki na kama kuna mambo wanaona hayafai wawagomee. Hata kama vijana hawaongozi lazima waweke utaratibu wa kuelezwa na kuridhishwa juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa.

Nguvu na thamani ya kijana

Dira ya Taifa lolote hulalia kwenye maono ya vijana. Hivyo ni hasara kubwa kwa nchi kama vijana hawapewi nafasi kushiriki ujenzi wa Taifa lao au hata kuwa na fursa ya kushauri.

Vijana ndiyo kundi lenye watu wenye nguvu zaidi za kimwili, ubongo wao unachemka na unafanya kazi kwa kasi kubwa, vilevile wanakuwa na tamaa ya mafanikio. Taifa linaposhindwa kuwatumia ipasavyo ni hasara isiyopimika.

Vijana wenyewe kwa kutambua thamani yao, wanapaswa kufahamu kuwa wanao wajibu wa kujielimisha namna ya kuendesha nchi yao. Wanatakiwa kujua kwamba uchumi unakuzwaje ili wakiona mambo yanakwenda mrama wapaze sauti kukataa uharibifu wa uchumi wao, maana ni wao wenye kuishi zaidi na kwa hiyo machungu watayaishi kwa muda mrefu.

Vijana wanatakiwa kusoma na kufuatilia hatua kwa hatua masuala ya nchi. Vijana wana wajibu wa kujifunza namna bora ya kufikiri na kuchanganua mambo. Ni hapo ndipo wakiambiwa uongo watakataa na wataukubali ukweli.

Vijana lazima wajifunze kujenga hoja na kujadili masuala ya nchi yao, hawatakiwi kuwaachia watu wa kundi jingine waifanye hiyo kazi kwa niaba yao. Mafanikio ya nchi ni lazima yaegemee kwenye jitihada za vijana.

Ujana ni chemchem ya maisha. Ndiyo umri ambao watu wake huota ndoto kubwa na kufanya ugunduzi. Vijana wakitulia ni rahisi kufanya mapinduzi chanya.

Wana nguvu na uwezo wa kuongoza makundi mengine kuelekea maisha bora zaidi kulingana na ndoto zao.

Ulinzi wa nchi haumtegemei yeyote zaidi ya kijana kwa sababu ndiye mpambanaji na ana nguvu. Kwa nafasi hiyohiyo ya ulinzi na ujenzi, pia ni jukumu lake. Na jukumu hilo ni la lazima.

Hasara ya kijana Tanzania

Vijana walioingia kwenye siasa kwa uchache wao, maisha yao ya kisiasa ndani ya vyama yamekuwa ya upambe. Hawakai mbele, isipokuwa wanajiweka kwenye miavuli ya wengine.

Ufuasi wa kisiasa haukatazwi tatizo ni kuwa unazidi kipimo. Vijana wengi sasa hivi wameamua kuwa wafia vyama badala ya kufia nchi. Wanashindwa kuelewa kuwa nchi inawadai miaka mingi zaidi ya kuishi.

Kufa au kudumaa kwa vyama vya siasa kuna athari ndogo kuliko kuharibu nchi. Vijana ambao wanatakiwa kuwa na sauti kali pale wanapoona mustakabali wao unachezewa ndiyo wamekuwa bendera fuata upepo. Vijana walioingia kwenye siasa wamejifyatua ule uwezo wao wa kufikiri na kuhoji. Kila wanachoambiwa wanapokea tu kisha wanakitetea. Chochote kinachotoka upande wa pili wanakipinga tu, wala hawakitafakari kwa faida au hasara zake.

Kama vijana wangekuwa imara na kutambua nguvu yao, wasingekuwa wanasubiri kulishwa maneno kisha wao wayaseme kwa kuyabebea mabango, badala yake wao ndiyo hasa wanatakiwa kuwa wapishi wa hoja zao.

Kijana mzuri mwenye kutambua nafasi yake katika ujenzi wa nchi hawezi kuwa anakubali kulishwa maneno na kuyapokea kama yalivyo bila hata kuyaweka kwenye mzani ili kuyapima kwanza faida na athari zake. Janga la Taifa ni kuwa kizazi cha vijana ambao hawajengi hoja kwa masilahi ya nchi, bali wanabishana kwa manufaa ya itikadi zao za kisiasa. Vijana wanaponzwa na viongozi wa vyama vyao ambao hawatarajiwi kuishi miaka mingi kama wao.

Ni kubishana tu, njaa ipo haipo, ukame upo haupo, fedha zimefichwa hazijafichwa, Bunge lionyeshwe moja kwa moja lisionyeshwe, sukari imefichwa na wafanyabiashara au haijafichwa. Wanapobishana huoni uwezo wa kufikiri wa vijana na ujenzi wa hoja, bali kinachoshuhudiwa ni misimamo.

Vijana wenye kujitambua sharti kuwe na mambo yenye kuwaunganisha kama Taifa. Hata wanapolazimika kutofautiana, hutokea hivyo kwa sababu ya kubisha kuhusu namna bora ya ujenzi wa nchi. Vijana hawatakiwi kubishana kuhusu ujenzi wenyewe wa nchi. Hilo ni janga.

Sifa ya kijana mzuri

Vijana wanatakiwa kuwa na mawazo ya kutatua matatizo na siyo kuweka misimamo ya vyama. Wanatakiwa kuwa na macho ya kuziona changamoto kisha wawe na namna bora ya kuzikabili.

Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandaowww.luqmanmaloto.com