Vijana wajengewe uzalendo kwa Taifa, si kwa vyama vyao

Muktasari:

  • Rais anasisitiza suala la kufanya kazi kwa kila mtu mwenye uwezo huo. Hii aliianza tangu wakati wa mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 alipoanzisha kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”

Tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza na kurejea baadhi ya mambo mara kadhaa akisema kuwa ndiyo misingi na malengo ya uongozi wake.

Rais anasisitiza suala la kufanya kazi kwa kila mtu mwenye uwezo huo. Hii aliianza tangu wakati wa mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 alipoanzisha kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”

Pia uzalendo, uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma, vita dhidi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali na fedha za umma pia ni miongoni mwa mambo anayoyahimiza sana Rais Magufuli.

Leo nimechagua kuzungumzia moja pekee. Nalo ni uzalendo ambalo kila mmoja anaweza kuwa na tafsiri yake kuhusu neno hili.

Wapo wanaoamini ni kuonyesha upendo, thamani na imani kwa jambo au kitu ambacho mtu au kundi la watu wanayo.

Nionavyo mimi, uzalendo unaweza kujengwa kwenye utaifa, itikadi, imani ya dini na hata makundi mengine ya kimasilahi. Wakati mwingine uzalendo unaweza kuwa hata kwa makundi ya kimasilahi kama vyama vya siasa na jumuiya mbalimbali za kijamii.

Hata hivyo, Kamusi ya Kiswahili sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, inautaja uzalendo kuwa ni “hali ya mtu kuwa tayari kufia nchi yake”; au “hali ya kuwa mzalendo.”

Wapo watu ambao ni wazalendo kwa mambo ya msingi, mema na yenye faida na kulinda maslahi mapana kwa jamii, umma na Taifa kwa ujumla. Vivyo hivyo wapo ambao wanajiona ni wazalendo kwa mambo yaliyo kinyume na jamii au umma.

Lililo dhahiri ni kwamba makundi yote ya Wazalendo (kwa jema au baya), hujivunia, hutukuza, huthamini, hulinda, hutetea na ikibidi hata hufikia hatua ya kupigania wanachokiamini.

Uzalendo kwa kitu, jambo, imani au itikadi wakati mwingine hufifisha uwezo wa kufikiri na kufanya tafakuri.

Uzalendo pia huweza kufifisha utu kwa mtu au kundi la watu na kufikia hatua ya kukiuka au kukanyaga haki za wengine kulinda, kutetea, kutukuza na kuendeleza kile wanachokiamini au wanachotaka kukifia.

Nguvu iliyomo ndani ya neno uzalendo ndiyo husukuma makundi yote kuanzia mataifa, dini na madhehebu, vyama vya siasa na makundi mengine ya kimasilahi kuwafundisha watu au wanachama wao neno uzalendo.

Kwenye majeshi yote duniani, askari au wapiganaji hufundishwa na kujengwa katika misingi, tabia na hulka za uzalendo yaani kufia nchi yao.

Kwa lugha ya mitaani wanasema wananyweshwa maji ya bendera ndiyo maana askari wa Taifa lolote yuko tayari kwenda vitani kupigania Taifa na watu wake dhidi ya adui yeyote.

Uzalendo ndio huwapa ujasiri na utayari wa kuingia uwanja wa vita wakiwa na hamasa, ari na imani kuu ya ushindi bila kujali hatari iliyoko mbele yao, kifo kikiwamo iwapo adui atawawahi.

Tangu wakati wa harakati za ukombozi na hata baada ya uhuru mwaka 1961, Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ilijenga Taifa lenye watu wazalendo. Vijana walijengewe uzalendo kwa chama na nchi yao wangali wadogo.

Chama cha Tanganyika African Union (Tanu), kilichopigania Uhuru kilifanya kazi hiyo kupitia kitengo chake cha vijana (TYL) kilichoongozwa na vijana wa wakati huo, Rashid Kawawa, Moses Nnauye na Kingunge Ngombale-Mwiru, nikitaja kwa uchache.

Hata ilipozaliwa CCM mwaka 1977 kwa kuunganisha Tanu na Afro Shiraz Party (ASP) nayo iliendeleza kazi ya kujenga uzalendo wa vijana kwa chama na Taifa kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Kupitia TYL na baadaye UVCCM, vijana waliandaliwa na kupikwa kuwa viongozi kwa kujengewa uzalendo kwa chama na Taifa lao.

Kipindi kile, uzalendo wa mtu kwa Taifa ulipimwa kwa uzalendo kwa chama. Hakukuwa na maisha kijamii, kiuchumi na hata kiuongozi nje ya Tanu na baadaye CCM.

Kadi za Tanu na baadaye CCM ndizo zilikuwa ufunguo katika kila kitu kuanzia maisha ya kawaida hadi utumishi wa umma au jamii.

Kwa wakati huo, ilikuwa sahihi vijana kujengewa uzalendo kupitia Tanu na baadaye CCM kwa sababu vyama hivyo ndivyo vilikuwa vyama vya siasa na wakati huohuo ndiyo Serikali.

Wakati huo Tanu na CCM vilikuwa sawa na hadithi ya kuku na yai. Hakuna aliyekuwa muhimu kuliko mwingine kwa sababu bila yai hakuna kuku. Vivyo hivyo bila kuku hakuna yai.

Kila eneo la kazi au jumuiya palikuwa ni lazima pawepo ofisi ya chama huku viongozi wa matawi ya chama wakiwa imara na wenye nguvu kuliko hata watendaji wakuu wa taasisi husika kwa sababu walikuwa na jukwaa la kuwajadili na kuwashughulikia kwenye vikao.

Wengi wa viongozi nchini (kutoka vyama vyote vya siasa), wote wametokana au ni matunda ya Umoja wa Vijana ama wa Tanu au CCM.

Hata hivyo, tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwanzoni mwa miaka ya tisini, kumetikisa misingi imara ya uzalendo kwa Taifa na kubadili tafsiri yake.

Kwanza ile kaulimbiu ya chama kushika hatamu ilififia huku ofisi za chama maeneo ya kazi na kwenye taasisi za umma na shuleni zikafutwa.

Kwa bahati mbaya kwa Taifa, CCM haikukubali kuliachia kundi lenye nguvu la vijana kubakia kuwa jukwaa la vijana wote kitaifa bila kujali itikadi zao.

CCM, kama ilivyofanya kwa jumuiya zingine za wanawake na wazazi, ikaing’ang’ania Umoja wa vijana na kuufanya kuwa taasisi ya chama.

Hatua hii ikavilazimisha vyama vingine shindani navyo vikalazimika kuanzisha makundi yao ya vijana, wanawake na wazee, kila moja kwa jina lililoona linafaa.

Hivi sasa tunazo UVCCM ya chama tawala, iko Bavicha ya Chadema na JUVICUF ya CUF nikitaja kwa uchache.

Badala ya uzalendo kwa Taifa, vijana wa makundi haya kwa kiasi kikubwa wanafundishwa na kujengewa uzalendo kwa vyama na makundi yao ya kimaslahi.

Uzalendo kwa Taifa umekuwa si jambo la kipaumbele kwa makundi ya vijana kwenye vyama vyao.

Mara kadhaa tumewashuhudia vijana wa vyama hivi, wengine wakiwa ndugu wa damu wakinyukana kutetea itikadi na maslahi ya vyama na kisiasa zao ambazo zingine zinakinzana na masilahi na faida kwa jamii na Taifa.

Vijana wa Kitanzania waliopigania na kutetea masilahi ya Taifa hivi sasa wanapigania vyama vyao vya siasa na makundi yao ya kimaslahi.

Hakuna baraza wala umoja wa kitaifa linalowaweka pamoja vijana katika kusimamia, kutetea na hata kupigania masuala ya msingi ya Taifa. Kwanini?

Jibu ni rahisi. Hawana uzalendo tena kwa Taifa lao. Uzalendo sasa ni kwa vyama, itikadi na kibaya zaidi, wakati mwingine kwa dini, madhehebu au makundi yao ya kimasilahi.

Kila chama kina wajibu na haki ya kikatiba ya kuwafundisha na kuwajenga vijana katika itikadi zao, lakini wajibu na haki hiyo isiwe juu ya uzalendo na maslahi ya Taifa.

Ingawa tayari tumeshuhudia madhara, naamini bado hatujachelewa. Tunao muda wa kuanza kuwajengea vijana wetu uzalendo kwa Taifa lao badala ya vyama na itikadi za kisiasa.

Tuanzishe Baraza la Kitaifa la Vijana litakalowajumuisha vijana wote kwa pamoja bila kujali tofauti zao kitikadi na kisiasa.

Kwenye baraza hilo, vijana wajengewe uzalendo kwa Taifa na walitumie kujadili, kuweka msimamo, kutetea na kulinda masuala ya msingi yenye maslahi ya umma na Taifa.

Ndiyo. Itikadi kisiasa ni muhimu kwa sababu vyama vya kisiasa ndivyo vinaunda Serikali na kuongoza Taifa baada ya kushinda chaguzi za kidemokrasia, lakini kamwe tusiviweke vyama juu ya utaifa wetu. Tujenge, tulinde, tukuze, tujivunie na kutukuza utaifa wetu juu ya makundi yote ya kijamii na kimaslahi.

Tusiendelee kujenga Taifa lenye vijana waliogawanyika kiitikadi, ambao kwao vyama na makundi yao ya kimaslahi ni bora kuliko nchi.

Tuwajengee vijana wetu uzalendo kwa Taifa. Huu ndio urithi tulioachiwa na waasisi wa Taifa hili ambalo nasi tunapaswa na hakika ni wajibu wetu, kuwarithisha watoto na wajukuu wetu.

Badala ya kutumia nguvu na rasilimali nyingi kuwajengea vijana wetu uzalendo kwa vyama na makundi yetu ya kimaslahi, tufanye hivyo kwa kujenga uzalendo kwa Taifa wenye nguvu juu ya itikadi, dini, makabila, maeneo yetu na makundi yote ya kimaslahi.

Mungu ibariki Tanzania.

Kwa maoni; [email protected], 0766434354.