Vikwazo vya biashara bado vipo licha ya kusainiwa mkataba Soko la Pamoja EAC

Muktasari:

  • Nchi hizo zilitiliana saini ya kuwa na Soko la Pamoja kama ambavyo inahitajiwa na mkataba wa jumuiya hiyo ambao unaruhusu uhamaji huru wa mambo hayo ili kukuza biashara na uwekezaji ndani ya jumuiya hatimaye kuongeza uzalishaji na ustawi kwa wananchi husika.

Wakuu wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) waliposaini Mkataba wa Soko la Pamoja mwaka 2009, walikubaliana mambo mengi likiwamo kuruhusu uhamaji huru wa nguvukazi, huduma na bidhaa.

Nchi hizo zilitiliana saini ya kuwa na Soko la Pamoja kama ambavyo inahitajiwa na mkataba wa jumuiya hiyo ambao unaruhusu uhamaji huru wa mambo hayo ili kukuza biashara na uwekezaji ndani ya jumuiya hatimaye kuongeza uzalishaji na ustawi kwa wananchi husika.

Tanzania iliridhia mkataba huo utekelezwe kwenye sekta ndogo saba kati ya 46 zinazohusiana na huduma za kitaalamu kama vile uhandisi na uhasibu.

Hata hivyo, taarifa iliyowasilishwa hivi karibuni katika mkutano wa kuondoa Vikwazo Visivyo vya Kodi (NTBs) ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inaonyesha kuwa vikwazo vingi vilivyokuwapo kabla ya kuanza kwa Soko la Pamoja bado vinaendelea hadi leo.

Akitoa mfano wa matokeo ya kura ya maoni kuhusu Soko la Pamoja ya mwaka 2016, Mshauri Mwelekezi kutoka kampuni ya Integrity Business and Investment Solutions, Octavian Kivyiro anasema nchi wanachama wa jumuiya bado zinawekeana vikwazo kwenye baadhi ya maeneo yaliyoridhiwa na mkataba huo.

Anaeleza kwamba utafiti huo umebaini Tanzania ina vikwazo vinavyopingana na mkataba huo kwa asilimia 27, ikifuatiwa na Kenya yenye asilimia 24 huku Rwanda na Uganda zikiwa na asilimia 17 na Burundi ikipata asilimia 15.

Andiko la mshauri huyo ambalo lilijikita zaidi katika huduma za uhandisi linaonyesha huduma za kitaalamu bado zinakabiliwa na vikwazo vingi. “Kwa kiasi kikubwa, vikwazo vipo katika huduma za uhandisi,” anasema.

Vikwazo vya kisheria

Tanzania iliahidi kuondoa vikwazo vyote dhidi ya huduma za uhandisi ifikapo mwaka 2010 lakini baadhi ya sheria zilizopo zina vipengele ambavyo vinazuia utekelezaji wa mkataba huo wa kusafirisha bila kikwazo kwa huduma na bidhaa zilizokubaliwa.

Kwa mujibu wa Kivyiro, ‘mhandisi mgeni’ ametafsiriwa na Sheria ya Usajili wa Uhandisi ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa mwaka 2007 kwamba ni mhandisi asiye raia wa Tanzania hali inayowatenga wanaotoka nchi wanachama wa EAC.

Anasema baadhi ya vifungu vya sheria vinakwaza usajili wa wahandisi na kampuni za ushauri elekezi zinazotoka katika nchi wananchama wa EAC kwa kuongeza vipengele sawa na za kigeni.

Sheria nyingine inayotajwa kuwa kikwazo cha utengamano wa huduma ni ile ya ununuzi ya umma iliyorekebishwa mwaka 2016 ambayo inabana ushiriki wa kampuni kutoka nje ya Tanzania kwa kuzilazimisha ziwe na ushirikiano na wataalamu wa ndani katika kazi wanazofanya nchini.

Muswada wa Ununuzi wa Umma na Uuzaji Mali wa mwaka 2016 (Zanzibar) unataka kuwapo kwa maudhui ya nyumbani na unatoa upendeleo kwa bidhaa na huduma zinazotoka Zanzibar na unalazimisha ubia na Wazanzibari kwa kampuni zote kutoka nje ya Tanzania.

Sheria ya Taasisi za Utafiti wa Uvuvi mwaka 2016 na Sheria ya Taasisi za Utafiti wa Kilimo ya mwaka 2016 zina vipengele vinavyohitaji kampuni au mtu yeyote kutoka nje kushirikiana na wazawa.

Kifungu cha 15 cha Sheria ya Wakemia ya mwaka 2016 inaagiza usajili wa muda maalumu kwa wataalamu ambao hawana uraia wa Tanzania.

Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa Uhandisi (ERB), Patrick Barozi anasema hakuna kikwazo chochote cha kufanyiwa marekebisho sheria zenye haja hiyo ila kinachotakiwa wahusika kufuatilia ili mamlaka husika zichukue hatua.

“Sheria zote hizi zinaweza kufanyiwa marekebisho bila shida kabisa na wala siyo jambo gumu,” anasema Patrick.

“Hata hivyo, shida ya wahandisi wa Tanzania sio kukosa masoko ya nje ya nchi bali sera na sheria ambazo zinatoa kandarasi za miradi mikubwa kwa wageni zaidi. Wakati mwingine miradi hii huchelewa utekelezaji wake kutokana na kurudiwa hasa baadhi ya mambo yanapokuwa hayajazingatiwa katika ujenzi. Ingefanywa na Watanzania, wangezingatia utamaduni na tabia za kwetu wakati wa kubuni michoro husika,” anaongeza.

Anafafanua kuwa tofauti na nchi nyingine wanachama wa EAC, Tanzania ina miradi mingi kuanzia kwenye ujenzi hadi uchimbaji madini ambayo kama itawatumia Watanzania hawatahitaji kutoka nje ya mipaka ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye anasema wanaandaa utafiti utakaoangalia sheria zote zenye vikwazo ili kuzifanyia marekebisho na wataanza na huduma za kitaalamu hasa uhasibu na uhandisi.

Alisema Tanzania bado ipo nyuma katika kutekeleza mahitaji ya Soko la Pamoja la EAC, lakini watashirikiana na Serikali kuhakikisha marekebisho muhimu yanafanyika.

Athari za mtangamano

Soko la Pamoja la huduma linatarajiwa kuimarisha uwezo wa wahandisi wa ndani kutokana na kushirikiana na wenzao wa nchi za EAC.

Ushirikiano pia unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa wataalamu na kuwawezesha wahandisi wa Kitanzania kutoa huduma zenye ubora na kiwango cha kimataifa ndani ya jumuiya hiyo.

Kuongezeka kwa ubora wa huduma na ushindani kutoka kwa watoa huduma za kikanda ni suala jingine linalotarajiwa. Hali hiyo itafanikiwa kwa kuongeza mawasiliano na upashanaji habari miongoni mwa watendaji wa sekta binafsi na biashara katika kanda ya Afrika Mashariki.

Mapendekezo

Chapisho hilo linapendekeza Serikali iweke kipaumbele katika kusawazisha mchakato wa sheria zake, kanuni na taratibu ili kuzifanya ziende sambamba na matakwa ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki.

Vilevile ihakikishe sheria, kanuni au taratibu mpya zinazowekwa zinaendana na soko hilo kupitia uhamasishaji kwa wabunge ambao ndiyo watunga sheria na marekebisho yoyote yanayohitajika.

“Tunaitaka Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha mageuzi yoyote na kuanzisha timu ya wadau kutoka serikalini na sekta binafsi,” anasema Kivyiro.