MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Vioja vya wasomi wa Kiafrika na lugha zao

Muktasari:

  • Mfano mzuri ni Taifa la China ambalo lina dhamira ya dhati ya kueneza utamaduni wake kote duniani. Katika mataifa mengi duniani, Kichina hufundishwa kupitia taasisi yake ya Confucius.
  • Tanzania, Kichina hufundishwa katika baadhi ya vyuo vikuu kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma. Vilevile, hufundishwa katika baadhi ya shule za sekondari.

Mataifa na mabara mbalimbali duniani yanayotambua thamani ya tamaduni zao, hufanya jitihada kubwa kuziendeleza tamaduni hizo kwa gharama yoyote kupitia lugha, muziki, maandishi na njia nyinginezo.

Mfano mzuri ni Taifa la China ambalo lina dhamira ya dhati ya kueneza utamaduni wake kote duniani. Katika mataifa mengi duniani, Kichina hufundishwa kupitia taasisi yake ya Confucius.

Tanzania, Kichina hufundishwa katika baadhi ya vyuo vikuu kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma. Vilevile, hufundishwa katika baadhi ya shule za sekondari.

Katika makala haya tutarejelea maandishi ya Profesa Euphrase Kezilahabi wa Tanzania na Ngugi wa Thiong’o wa Kenya.

Profesa Kezilahabi katika makala yake ya “Erasure and the Centrality of Literatures in African Languages”, yaliyochapishwa katika jarida la Kiswahili, juzuu na. 75 la TATAKI, anatueleza vioja alivyokutana navyo katika miktadha miwili tofauti.

Kioja cha kwanza kilitokea huko Frankfurt, Ujerumani, alipoalikwa wenye Kongamano la Waandishi wa Kiafrika wakati wa maonyesho ya vitabu ya kimataifa. Kongamano hilo lilihudhuriwa na waandishi wengi wakubwa wa Afrika.

Siku moja wakiwa katika chamshakinywa, mwandishi mmoja wa Kiafrika ambaye huandika kazi zake kwa Kiingereza, alimuuliza Profesa Kezilahabi ikiwa naye ni miongoni mwa waandishi wa Kiafrika. Profesa alikubali. Swali jingine lilifuata kutaka kujua lugha atumiayo katika uandishi wake.

Jibu lilikuwa ‘Kiswahili’. Muulizaji wa swali hilo alimwangalia Profesa, kisha katika kicheko cha kejeli alimuuliza, “Ikiwa waandika kwa lugha hiyo umefuata nini hapa?” Swali hili lilikuwa kama fumbo kwa Profesa Kezilahabi.

Jambo jingine lililomshtua Profesa Kezilahabi kwa mujibu wa makala yake tajwa hapo juu, ni pale alipompa rafiki yake mmoja nakala ya kitabu chake cha Nagona mara baada ya kuchapishwa ili akisome na kumpa maoni.

Msomaji huyo alikisoma kitabu hicho, baada ya siku mbili alimtafuta Profesa na kumwambia, “Kitabu hiki ni kizuri sana… lakini kwa nini hukuandika kwa Kiingereza?” Hilo lilikuwa fumbo jingine kwa Profesa Kezilahabi.

Pia, Ngugi wa Thiong’o katika kitabu chake cha Decolonising the Mind: The Politics of Language in African Literature (1981) anajadili ukoloni unavyojichomoza katika lugha za Kiafrika. Mwandishi anaonyesha athari za Ukoloni katika lugha ni kubwa kiasi cha kuwaathiri baadhi ya Waafrika kisaikolojia.

Kwa jumla, anasisitiza matumizi ya lugha za Kiafrika katika uandishi wa kazi za fasihi ziwahusuzo Waafrika. Suala hili pia analijadili katika usuli wa kitabu chake cha Shetani Msalabani asemapo, “…yeyote popote alipo yambidi ajimudu katika lugha mbili: lugha ya kabila lake na lugha ya Kiswahili.”

Kwa maandishi ya wanataaluma hawa, tunabaini tatizo kubwa ambalo chanzo chake ni kutawaliwa. Ukoloni umeathiri saikolojia za wengi katika suala la lugha. Mbele ya lugha za kigeni, lugha zetu ambazo ni sehemu ya tamaduni zetu hazina thamani yoyote.

Tamaduni zetu ndiyo utambulisho wa kuwapo kwetu. Ikiwa hatuthamini lugha zetu wenyewe tunawezaje kujitambulisha kifua mbele katika jumuiya za kimataifa?

Fasihi ya Kiafrika ambayo mlengwa wake ni Mwafrika, inawezaje kuandikwa kwa lugha ambayo mlengwa huyo haijui?

Inastaajabisha kuona msomi wa Kiafrika anayepaswa kuwa mfano kwa wengine akibeza fasihi ya Kiafrika kuandikwa kwa lugha ya Kiafrika. Tuige mfano kutoka kwa Wachina katika kuthamini na kueneza lugha na tamaduni zetu.