Viongozi wa Afrika watoe majibu ya maswali haya kwa wananchi wao

Muktasari:

  • Katika utenzi huo uliopewa kichwa cha maneno ‘Why Africa, why?. Ncube anawakilisha kilio cha Waafrika kwa kuelezea hali ya viongozi wa bara hilo kisha kuuliza swali “Why Africa, why?” Yaani kwa nini Afrika, kwa nini?

Mshairi wa Zimbabwe, Bongani Ncube ameandika utenzi kwa lugha ya Kiingereza ambao umekuwa maarufu barani Afrika. Katika makala haya, ninakusudia kuchambua utenzi huu kwa faida ya msomaji.

Katika utenzi huo uliopewa kichwa cha maneno ‘Why Africa, why?. Ncube anawakilisha kilio cha Waafrika kwa kuelezea hali ya viongozi wa bara hilo kisha kuuliza swali “Why Africa, why?” Yaani kwa nini Afrika, kwa nini?

Katika ubeti wa kwanza, Ncube anaandika hivi; Kwa nini hawa waoga wanaitwa makomredi? Kwa nini hawa ‘ziro’ wanaitwa mashujaa? Kwa nini hawa wezi wanaitwa machifu? Kwa nini hawa wauaji wanaitwa wafalme? Kwa nini hawa wachakachua kura wanaitwa washindi? Kwa nini hawa waasi wanaitwa marais? Kwa nini Afrika, kwa nini?

Hakika ni maswali magumu ambayo kwa kila mzalendo wa Afrika yatamuumiza moyoni. Ni kweli kabisa viongozi wengi wa Afrika ni waoga. Ni waoga kukabiliana na mabeberu wanaonyonya rasilimali za Afrika.

Viongozi wengi wa Afrika ni washirika wa magenge ya wawekezaji kutoka mataifa tajiri huku wao na familia zao wakijilimbikizia mali kutokana na wizi wa rasilimali za Afrika. Ndiyo maana Ncube anauliza, kwa nini wezi hawa wanaitwa machifu?

Viongozi wenye utajiri mkubwa

Kwa mujibu wa orodha ya marais na wafalme matajiri zaidi barani Afrika iliyotolewa na jarida liitwalo Forbes linalotangaza masuala ya watu maarufu na matajiri duniani, Rais Jose Edwardo Dos Santos wa Angola anaongoza kwa kuwa na utajiri unaofikia Dola20 bilioni za Marekani.

Anafuatiwa na Mfalme Mohamed VI wa Morocco mwenye Dola2.5 bilioni, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea Dola600 milioni na Rais Uhuru Muigi Kenyatta wa Kenya Dola500 milion.

Paul Biya wa Cameroon Dola 200 milioni, Mfalme Mswati III wa Swaziland Dola100 milioni anakabana koo na Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan.

Wanafuatiwa na Rais wa Chad, Idris Berby Dola50 milioni, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe Dola10 milioni na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Dola 75 milioni akiwa pia ni mwanasiasa anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wanasiasa wote duniani.

Hawa ni baadhi ya viongozi wa Afrika na utajiri walionao. Ni kweli kabisa Ncube anayo haki ya kuuliza kwa nini hawa waoga wanaitwa makomredi? Kwa nini hawa ‘ziro’ wanaitwa mashujaa? Kwa nini wezi hawa wanaitwa machifu?

Kwa mujibu wa jarida hilo la Forbes, mbali na Rais wa Angola kujilimbikizia mali kiasi hicho, binti yake, Isabel Dos Santos maarufu kama ‘African Princes’ ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola3 bilioni alioupata ndani ya miaka 10 tu katika nchi ambayo wananchi wa kawaida wanaishi kwa kipato cha chini ya Dola2 kwa siku. Pia, binti huyo ndiye mwanamke tajiri kuliko wote barani Afrika.

Katika ubeti wa tatu wa utenzi wake, kama tutakavyouona baadaye, Ncube anasema, “wao ni viongozi matajiri zaidi kutoka nchi maskini zaidi duniani”.

Inawezekanaje nchi zetu maskini zitoe mabilionea kama siyo kwa kushirikiana na wale waitwao ‘economic hitmen’ yaani wauaji wa kiuchumi kuiba rasilimali zetu?

Wanawaogopa wanyonyaji?

Jambo la kusitikisha zaidi ni kwamba viongozi wa Afrika wako tayari kupambana na wananchi wao wanaodai haki na uhuru wa kusikilizwa zaidi, kuchagua viongozi wawatakao na kuamua kuhusu mustakabali wa nchi zao, huku viongozi hawa wakiwa waoga kuwakabili wanyonyaji wa Afrika na kibaya zaidi wanashirikiana nao.

Ncube anasema tena katika ubeti wake wa kwanza “Kwa nini hawa wauaji wanaitwa wafalme? Kwa nini hawa wachakachuaji kura wanaitwa washindi? Kwa nini hawa waasi wanaitwa marais? Kwa nini Afrika, kwa nini?”

Ni kweli, viongozi wengi wa Afrika ni wauaji wa wananchi wao hasa wale walio na ujasiri wa kukabiliana nao miongoni mwa wanasiasa, wanahabari, wapigania haki za binadamu na viongozi wa vyama vya upinzani.

Nchini Uganda kila uchaguzi wapinzani huswekwa ndani, mikutano ya uchaguzi ya wapinzani kuhujumiwa, madai ya wizi wa kura yanathibitishwa hata na jumuiya za kimataifa, lakini bado Rais wa nchi hiyo, Yoweli Museveni na chama chake cha waasi wa NRA atatawala tu.

Ndiyo maana Ncube anauliza “Kwa nini hawa waasi wanaitwa marais?” Kwa kuwa nchi nyingi za Afrika hukabiliwa na machafuko ya kisiasa mara kwa mara, Afrika ni ya tatu kwa idadi kubwa ya waandishi wa habari 15 waliouawa duniani mwaka jana.

Hata hapa Tanzania, wanahabari ni waathirika wa misuli ya watawala. Taifa kwa sasa linasubiri hukumu ya kesi ya mauaji ya Daudi Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten aliyeuawa wakati wa makabiliano ya polisi na wandamanaji wa Chadema mkoani Iringa mwaka 2012.

Wachakachua kura

Baadhi ya viongozi wa Afrika ni wachakachua kura wakitangazwa washindi kwa kuiba kura. Kwao uchaguzi huru na haki wa kisiasa siyo jambo la muhimu ila kushinda na kutangazwa washindi kwa gharama yoyote ndiyo lazima. Burundi, Uganda, Zimbabwe hata hapa nchini tuhuma ni hizo hizo iwe Zanzibar au Bara.

Katika nchi nyingi za Afrika watawala wanashinda kwa ‘mbinu’ ndiyo maana katika utenzi wake Ncube anauliza “Kwa nini wachakachuaji hawa wa kura wanaitwa washindi? Kwa nini Afrika, kwa nini?

Matokeo ya wizi wa kura ni kuingia madarakani viongozi ambao wanajua hawana ridhaa ya wananchi. Kwa kutambua hili, viongozi hao hufanya kila wawezalo ikiwamo kujikusanyia utajiri ili kugharimia uchaguzi unaofuatia, kutumia vyombo vya dola kubakia madarakani na ikibidi hata ‘kukanyaga’ katiba za nchi zao au hata kuzibadili kabisa.

Mfano mzuri ni wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dk Kiza Besigye anayestahiki kupewa tuzo ya ujasiri kwa kuthubutu kwake kukabiliana na mmoja wa madikteta wa Afrika, Museveni.

Ni sahihi kabisa kwa Ncube kuuliza kwa nini hawa waoga wanaitwa makomredi? Kwa nini hawa ‘ziro’ wanaitwa mashujaa?

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected]