Friday, March 17, 2017

MAONI YA MHARIRI: Viongozi wa Serikali wawe wanajitathimini, washirikishe wananchiMkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda 

Juzi, wakuu wa mikoa nchini walitimiza mwaka mmoja tangu wateuliwe katika nafasi hiyo ikiwa ni katika utawala wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli. Lakini kati ya hao ni Paul Makonda pekee wa Dar es Salaam ambaye alisimama hadharani na kutoa tathmini ya mambo aliyoyafanya na ambayo anatarajia kuyafanya mwaka wake wa pili. Makonda alibainisha mambo 10 aliyoyafanya na kutaja mengine idadi kama hiyo atakayoyafanya miezi 12 ijayo huku akiahidi kuongeza kasi ya utendaji wake, jambo ambalo tunadhani ni zuri.

Pia, aliahidi kuhakikisha anaboresha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam na kumsaidia Rais John Magufuli kutekeleza ilani ya CCM.

Kwa maelezo yake, Makonda alibainisha aliyoyafanya kwenye sekta za afya, mazingira, elimu, ardhi na ulinzi. Kati ya aliyoyaeleza, nusu yalilenga kuimarisha afya za wakazi wa jiji hilo lenye watu wengi zaidi ambao wanakadiriwa kufika milioni tano.

Katika kutekeleza hilo, mkuu huyo wa mkoa alisema amesimamia ujenzi wa wodi za wagonjwa, amesimamia vita dhidi ya dawa za kulevya na kufanya kampeni ya kuchangia damu. Hakuishia hapo, amejigamba kuwa amepiga marufuku uvutaji wa shisha na kuimarisha usafi wa jiji.

Ili kuboresha mandhari, Makonda amesema aliendesha kampeni ya ‘mti wangu’ inayohamasisha upandaji miti kisha akatatua migogoro ya ardhi. Katika kuhakikisha kunakuwa na hofu ya Mungu, amesema amefanikisha ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Vilevile, ameweka misingi ya elimu kwa kutengeneza madawati kwa ajili ya shule za umma. Ili kudumisha usalama, na alitoa wito kwa wakazi wanaomiliki silaha kuzihakiki na kusalimisha zilizo haramu.

Tunaamini kuwa kila mkuu wa mkoa atakuwa amefanya tathimini yake ya mambo aliyoyafanya na yale ambayo alishindwa kuyafanya huku kila mmoja akijiwekea malengo mapya kwa ajili ya mwaka wa pili tangu kuteuliwa nafasi hiyo muhimu.

Tunaamini kuwa wakuu wa mikoa watakuwa wamefanya tathimini kwa maandishi na kupeleka sehemu husika ili wapimwe kwa yale waliyoyafanya mwaka huo wa kwanza na waone jinsi ya kujipanga upya kwa mwaka wao wa pili.

Na hili lisifanyike kwa wakuu wa mikoa tu, bali iwe ndio mfumo kwa viongozi wote wa serikali kujitathimini kila wanapomaliza kipindi fulani cha uongozi.

Tunaamini kuwa, endapo kila kiongozi kuanzia ngazi ya shina, wilaya, mkoa mpaka taifa atasimama na kujifanyia tathimini mambo aliyoyafanya, baada ya muda mfupi Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa. Kwa sababu tathimini ya kila mmoja ndiyo itakayosaidia kujua tunakoelekea na mambo tunayopaswa kuyafanya ili kufikia malengo.

Kama kila, kiongozi atakuwa na vipaumbele vyake ambavyo wananchi na wadau watajitokeza na kumpa ushirikiano, kisha hali iwe hivyo kwa ngazi ya zote kuanzia chini mpaka juu, hakuna kingine kitakachotokea zaidi ya maendeleo.

Tungependa kuona viongozi wote kwenye himaya zao wakiwa na mipango ya wazi itakayowasukuma kuongeza tija. Isiwe ya kwenye makabrasha inayowafikia wachache ambao huenda haisomwi na waliokusudiwa.

Tunajua kila kiongozi huwa na staili yake ya uongozi, wengine hawapendi kutangaza mipango yao nje kwa umma, lakini katika hili tungependa mipango na mikakati ya viongozi wa serikali kwa ngazi zote iwe inawekwa wazi ili wananchi wapate kushiriki na wao wao sehemu ya maendeleo ya nchi yao.

-->