Visingizio vya usingizi

Muktasari:

Naam, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukutana, uhuru wa kuchagua viongozi wetu wa kisiasa, kitaaluma, kiuchumi na kadhalika ni mambo ya msingi sana hapa petu, ndiyo maana tunajivunia sasa kuwa Wabongo. Kwa hiyo, hata huyu Musa Lendo ana haki kabisa ya kusikilizwa na wanaopenda kumjadili na kutofautiana naye nao wana haki ileile. Ndio msingi wa kutafuta maendeleo ya kina kabisa. Ni katika kusikiliza pande zote na kujifunza kutokana na watu wenye mitazamo mbadala ndipo sera na mipango inakuwa na mafanikio zaidi.

Naona nimefanya makosa makubwa kunyong’onyea mbele ya huyu Musa Lendo. Sasa kila mtu anafikiri anaweza kusimama mbele yangu na kutunisha misuli ili nikubali kubandika upuuzi wake katika safu yangu. Kwa hiyo, napenda kuwaarifu kwamba misuli ninayotambua ni ile inayovaliwa na watu tu. Huyu Musa Lendo sikumruhusu kwa sababu ya vitisho vya misuli yake bali kwa kuwa nilitaka wengine wapate fursa ya kutoa maoni maana sote twajua kwamba hii ni nchi inayoheshimu haki za binadamu.

Naam, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukutana, uhuru wa kuchagua viongozi wetu wa kisiasa, kitaaluma, kiuchumi na kadhalika ni mambo ya msingi sana hapa petu, ndiyo maana tunajivunia sasa kuwa Wabongo. Kwa hiyo, hata huyu Musa Lendo ana haki kabisa ya kusikilizwa na wanaopenda kumjadili na kutofautiana naye nao wana haki ileile. Ndio msingi wa kutafuta maendeleo ya kina kabisa. Ni katika kusikiliza pande zote na kujifunza kutokana na watu wenye mitazamo mbadala ndipo sera na mipango inakuwa na mafanikio zaidi.

Kwa hiyo, anayetaka kuja kwangu na kunitunishia misuli asahau. Atunishe akili, alete mawazo, anishawishi na hoja zake za nguvu ndipo tutaenda pamoja.

Ndiyo maana huyu aliyeniletea makala hii na kunilazimisha kuchukua kwa misuli yake feki kama vyeti, ajue kwamba nilitaka kuichanachana kwanza lakini baada ya kuisoma, niliona haya, na tumsikilize yeye na kuwapatia watu wengine nafasi ya kutoa maoni yao.

Bwana Makengeza,

Kuna jambo moja linanisumbua sana juu ya Wabongo wenzangu. Waweza kuwafanyia lolote lile na watapokea tu. Inabidi kufanya nini hadi waamke na kusema “La! Hapana! No no no!”. Nakumbuka huko nyuma wewe ulisema mara nyingi kwamba Wabongo ni watu wa ajabu. Wanapenda amani lakini hawapendi sheria.

Hivyo, ilimradi mtu anavunja sheria kwa amani, hakuna ambaye atalalamika. Enzi zile, uliweza kufunga barabara na kujenga ghorofa katikati bila wasiwasi. Uliweza kutanua na kuchepuka, uliweza hata kutafuna mamilioni ilimradi utafune bila kuwashtua watu. Tena watu walipenda hata kutetea uvunjaji wa sheria. “Kwani kuna ubaya gani kujenga hapa. Kila mtu ana haki ya kuwa na nyumba.”

“Ungekuwa wewe, si ungetafuna Bwana.” “Nani atajizuia?”

“Na kama kawaida, wengine walimwachia Mungu tu. Kweli ningekuwa, Mungu ningejiuzulu maana hizi kazi duh.”

Wakati ule nilikumbuka kitabu cha Chinua Achebe cha A Man of the People (Mtu wa Watu). Alitoa hadithi ya mwenye duka ambaye alijulikana sana kwamba ni mwizi. Alikuwa anawaibia watu kila siku dukani kwake, kwa vipimo feki, kwa bei feki (hadi labda hata cheti kilikuwa feki, lakini tusiyaongelee haya).

Watu walivumilia tu. Lakini siku moja akaja kipofu. Mwenye duka alipenda sana ile fimbo yake maalumu kwa hiyo akampokonya. Weeee! Acha watu waje juu. Jamaa alilazimishwa kufunga duka lake moja kwa moja.

Achebe alitoa wazo kwamba, hatimaye, watu walikuja juu kwa sababu jamaa alikuwa ameiba waziwazi, hadi watu wakamwona. Kisha Achebe akamlinganisha huyu mwenye duka na wanasiasa au wenye mfumo.

Ni wakati gani wezi na walafi hatimaye wanatafuna hadi waonekane? Enzi hizo za kashfa ambazo zimezikwa moja kwa moja maana watu wanaogopa kufukua, nilijiuliza kweli ni wakati gani Wabongo wenzangu wataona? Watakataa kuona hadi lini? Sasa mambo yamebadilika. Makaburi ya zamani yanabaki yamefungwa, lakini tumepata awamu ya kuchukua hatua. Sasa nashangaa kwamba bado wananchi wanamwachia mwingine. Hatuamki na kusema, Bwana eee, imetosha. Badala yake tunamwachia mtu mmoja na watu wake wachache kufanya yote kwa niaba yetu.

Na kwa kuwa tunafanya hivyo, ina maana kwamba tumejinyima nafasi yetu ya kusema chochote. Kama tulivyokuwa watazamaji wa mashindano ya nani mwizi zaidi, sasa tumekuwa watazamaji wa mashindano wa nani mwenye amri zaidi.

Kwa kuwa hatukutaka kuamka na kuchukua hatua sisi wenyewe huku tunaibiwa mali zetu, sasa tunashindwa kuamka na kuchukua hatua tukiibiwa nafasi yetu ya kusema, na kutoa mawazo mbadala na kushiriki maamuzi. Na kama kawaida yetu tunajitetea.

“Unajua Bongo Bwana, tunahitaji dikteta. Tunahitaji mtu wa kuwakomesha hawa wazembe, wabadhirifu, mafisadi na kadhalika.”

Kwa nini? Kwa sababu hatuko tayari kuchukua hatua sisi wenyewe. Kweli visingizio vya usingizi ni vingi hata kama amri hizohizo mwisho zinatugeukia. Tutabaki kulalama na kuloloma tu, bila kuchukua hatua yoyote. Tulifinywa kiuchumi, kimya, twafinywa kisiasa, kimya.

Ndiyo maana nimeamua kukuletea shairi linalofanana na lile lililoandikwa na Mjerumani enzi zile za udikteta huko kwao. Si kwamba sisi tumefikia hali hii, bali nataka kuonesha jinsi ambavyo tunaweza kujipeleka hukohuko.