UCHAMBUZI: Vita ya viroba isiwe ya Waziri Makamba pekee

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba

Muktasari:

Hapana shaka aliona madhara ya matumizi ya pombe ambayo pamoja na kuzorotesha ufanisi kazini ni chanzo cha magonjwa mengi. Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba alitekeleza zuio la kuuzwa kwa pombe kali zinazofungashwa kwenye pakiti za plastiki maarufu kama viroba.

Mwanamuziki wa reggae, hayati Bob Marley, katika moja ya mahojiano yake aliwahi kusema ‘mimea ni uponyaji wa Taifa, lakini pombe ni uharibifu.’

Hapana shaka aliona madhara ya matumizi ya pombe ambayo pamoja na kuzorotesha ufanisi kazini ni chanzo cha magonjwa mengi. Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba alitekeleza zuio la kuuzwa kwa pombe kali zinazofungashwa kwenye pakiti za plastiki maarufu kama viroba.

Makamba alisema nia ya Serikali ni kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kufungashia pombe. “Natoa wito kwa watengenezaji, wasambaji na waagizaji wa mifuko ya plastiki waanze kujiandaa sasa kwa zuio hili,” alisema Makamba.

Alisema chanzo cha uchafu kwenye vyanzo vya maji hasa mito, maziwa na fukwe za bahari asilimia kubwa ni kutokana na mifuko ya plastiki. Zuio limelenga kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vifungashio hivyo kutokana na urahisi wa upatikanaji wake, hivyo kutumiwa hata na watoto.

Niweke wazi, zuio hili linahitaji afua kutoka sekta nyingine ikiwamo ya afya ambayo inatakiwa kuangalia zaidi madhara ya pombe hizo kwa watumiaji. Wakati Makamba akiviondoa viroba na kuwataka wauzaji watafute mbinu nyingine za kufungasha vinywaji hivyo, Wizara ya Afya ingetafuta mwarobaini utakaopunguza unywaji holela ya pombe.

Wizara ya Afya inatakiwa kuchukua hatua dhidi ya unywaji pombe kwa sababu ndicho chanzo cha magonjwa lukuki nchini. Mwongozo wa uchunguzi wa magonjwa uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) umeorodhesha madhara kuwa ni pamoja na uraibu unaomfanya mtumiaji kuitegemea pombe na kushindwa kuishi au kufanya chochote bila kuinywa.

Si hivyo tu, matumizi ya pombe husababisha madhara katika ubongo, wengi wanaoitumia kwa muda mrefu hupata magonjwa ya akili. Madhara mengine yanayotajwa katika mwongozo huo ni kuvimba kwa ini; ugonjwa usio na tiba.

Kadhalika, unywaji wa muda mrefu humuweka mtumiaji katika hatari ya kupata saratani ya mdomo, ulimi, koo, tumbo na utumbo. Ikiwa sugu mwilini, hupunguza hamu ya kula na kusababisha ugumu wa kukimeng’enya.

Sina shaka faida za pombe ni chache kuliko hasara kama zinavyoainishwa na kudadavuliwa katika vitabu na majarida ya afya. Ni vyema basi wizara zinazohusika zikaingilia kati alipoanzia Waziri Makamba.

Hii ni kwa kuwa Makamba amelenga kuviondoa viroba ili kulinda mazingira, lakini wafanyabiashara wanaweza kutafuta mbinu nyingine ya kuzifungasha pombe kali na kuziuza kwa bei nafuu. Kwa mfano, katika nchi nyingine ni marufuku pombe kuuzwa mchana, pia hakuna yeyote anayeweza kununua pombe bila kitambulisho ambacho hutumika kuzuia watoto, wanafunzi kununua.

Udhaifu uliopo nchini, licha ya viroba kuna utengenezaji wa pombe za kienyeji ambao hata kama vitazuiwa, wapo watakaozikimbilia hizo na isitoshe zinauzwa kwa bei nafuu zaidi.

Kwa mfano gongo, inatengezwa karibu mikoa yote nchini na kuuzwa kwa bei nafuu, kama watumiaji wa viroba watavikosa basi ni rahisi kwao kuanza kunywa gongo.

Kadhalika, pombe kali ambazo si haramu nazo zinauzwa kwa bei nafuu na zinafungashwa katika chupa. Je, watumiaji wanashindwa kununua pombe kali za kwenye chupa iwapo zitauzwa kwa bei nafuu?

Naipongeza hatua ya Makamba ingawa sekta nyingine hazina budi kutafuta njia za kupunguza matumizi ya pombe kwani yamekuwa juu nchini. Hali kadhalika wanaotumia pombe kupita kiasi hawana budi kujitathmini na kuangalia madhara hayo.