UCHAMBUZI: Viwanda havijengwi kwa matarumbeta ila mikakati makini

Muktasari:

Kwa dhana hiyo, siyo jambo rahisi kwa nchi moja yenye uchumi wa viwanda, ambao ndio tegemeo lake kiuchumi, kujitokeza kuwa tayari kuisaidia nchi nyingine changa yenye uchumi wa kujikimu bila ya kuwa na “sababu za kiuchumi na kisiasa zilizo jificha nyuma ya pazia.

Kila nchi duniani ingependa kuwa na uchumi wa viwanda. Lakini kupenda ni jambo moja na kuwa nchi ya viwanda ni jambo lingine.

Kwa dhana hiyo, siyo jambo rahisi kwa nchi moja yenye uchumi wa viwanda, ambao ndio tegemeo lake kiuchumi, kujitokeza kuwa tayari kuisaidia nchi nyingine changa yenye uchumi wa kujikimu bila ya kuwa na “sababu za kiuchumi na kisiasa zilizo jificha nyuma ya pazia.

Na suala la kuwa na utajiri wa maliasili na rasilimali lingekuwa kigezo tosha cha kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda basi bara la Afrika lingekuwa la kwanza duniani kwa uchumi wa viwanda.

Lakini, hali halisi haiko hivyo. Uzoefu unadhihirisha rasilimali watu ni kigezo muhimu zaidi cha uwezo wa kuanzisha viwanda kuliko rasilimali asili; madini, gesi asili, na misitu.

Ubora wa elimu, hususan ya ufundi na teknolojia ya kisasa, mafunzo ya ufundi na stadi mbalimbali kwa vitendo, ujuzi pamoja na uzoefu wa miaka mingi katika ubunifu, tafiti za kiwango cha juu na uzalishaji, ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa rasilimaliwatu kuanzisha viwanda bila msaada wa kiufundi kutoka nje.

Hata ikitokea nchi kuwa na utajiri wa maliasili na rasilimali watu ya uhakika bado uanzishaji wa viwanda unatahitaji usiri na umakini mkubwa. Ni vyema kiwanda kikajulikana uwepo wake baada ya bidhaa zake kuanza kupataikana sokoni na siyo kwenye hatua za mwanzo.

Kuutangazia ulimwengu kwamba Tanzania inakusudia kuanzisha kiwanda cha kutengeneza bidhaa fulani, kimkakati siyo jambo sahihi. Ni kosa kubwa la kiufundi ambalo linahitaji kuepukwa kwa siku za usoni iwapo tumedhamiria kutekeleza uanzishaji wa viwanda kwa mafanikio.

Viwanda vinajengwa kimyakimya ila kwa mikakakati mahsusi inayoshirikisha wazalendo wenye uwezo wa kubuni, kuanzisha na kuviendesha. Wazalendo wanaotambua sheria na sera kandamizi zilizopo ambazo ni kero na kikwazo cha maendeleo hayo.

Tanzania ni moja ya nchi masikini duniani. Kuifanya ichupe kutoka katika uchumi wa kujikimu hadi wa viwanda ni mchakato mrefu utakaochukua miongo kadhaa kuukamilisha.

Mazingira ya uchumi wa viwanda duniani katika miaka ya 1890 ni tofauti sana na yale yaliyokuwepo miaka ya 1920 au ya 1950 au ya 2000. Ni tofauti pia na ya sasa.

Hivi sasa, karibu kila kitu utakacho fikiria kukitengeneza, tayari kinatengenezwa mahali fulani duniani. Ushindani wa bidhaa za viwandani duniani ni mkali zaidi kuliko wakati mwingine wowote uliopita toka kuanzishwa kwa viwanda vya kwanza duniani.

Kila nchi ipo makini kulinda viwanda na soko la bidhaa zake huku vita baridi vya kuibiana teknolojia vikishika kasi. Tanzania kuendelea kuomba au kubembeleza misaada ya kiteknolojia kutoka nchi nyingine duniani ambayo ni muhimu katika uanzishaji wa viwanda nchini ni dalili ya kutofanikisha adhma hiyo.

Ninachomaanisha hapa ni kwamba Watanzania wasitarajie mteremko katika mchakato wa uanzishaji wa viwanda nchini. Litakuwa kosa kubwa la kiufundi kuendelea kutegemea nchi nyingine kuja kutusaidia kujenga viwanda nchini bila sisi wenyewe kujipanga sawasawa kwa rasilimali zilizopo nchini.

Jambo muhimu ni kujiuliza juu ya viwanda vya kipaumbele vitakavyozalisha bidhaa ili kutosheleza mahitaji ya ndani kwanza kabla ya kukidhi masoko ya nje. Ni lazima kufahamu kuwa soko la nje lina ushindani mkubwa kabla busara haziona uelekeo wa nguvu kwa soko ya nje au kutosheleza mahitaji ya ndani.

Ni wakati muafaka kuangalia namna Tanzania ilivyojigawa kikanda katika uwekezaji viwanda na Serikali kuonyesha dhamira yake ya kuifanya ya mfano na kuibua vipaji vitakavyochochea ubunifu.