Viwanda vya kahawa nchini ni mkombozi wa wakulima

Wawkulima wakichambua kahawa

Muktasari:

Badala ya kusubiri kuuza kwenye soko la dunia ambako mara nyingi bei yake haitabiriki, wanauzia viwanda nchini ambavyo vinauza ikiwa tayari imesindikwa na hivyo kufanikisha ule mnyororo wa thamani.

Mwaka 1989 Serikali ilipoamua kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ililenga kuwapa soko la uhakika wakulima na kuwapunguzia adha ya kusafirisha.

Mbali ya kiwanda hicho kuwa soko la uhakika kwa wakulima, pia kinatoa ajira za moja kwa moja na nyingine nyingi zisizo za moja kwa moja.

Mwaka mmoja baadaye yaani 1990 Serikali iliamua kupanua wigo wa umiliki wa kiwanda hicho, iliuza sehemu ya hisa zake kwa vyama vya ushirika wa wakulima wa kahawa ili kuwapa wakulima fursa ya kuwa sehemu ya wamiliki wa kiwanda hicho. Kiwanda hicho kwa Mkoa wa Ruvuma ndiyo cha kwanza kikubwa. Vipo viwanda vingine kama Dae LTD pamoja na kiwanda cha CMC vilivyoko wilayani Mbinga.

Meneja wa kiwanda hicho Jonas Mbunda alisema baada ya hisa kuuzwa, Kiwanda cha Kahawa Mbinga kwa sasa kinamilikiwa kwa ubia kati ya vyama vya ushirika vinavyolima kahawa Tanzania vyenye hisa 56.54 huku Serikali ikibaki na hisa 43.46.

Mbunda alisema kazi kubwa ya kiwanda ni kukoboa na kusindika kahawa. Lakini pia kutokana na uwapo wa maghala, kinahifadhi kahawa iliyokobolewa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi au kwenye viwanda vingine.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kahawa inayokobolewa katika kiwanda hicho inanunuliwa kutoka kwa wafanyabiashara binafsi, vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima kutoka wilaya za Mbinga, Nyasa na Songea vijijini. “Kiwanda hiki kina uwezo wa kukoboa kahawa kati ya tani 25,000 na 30,000 kwa mwaka. Kinatumia mashine zilizo bora, zenye uwezo mkubwa na za kisasa kutoka Brazil,” alisema Mbunda. Baada ya kukoboa kahawa inawekwa katika madaraja kisha kinasindika katika paketi au makopo bidhaa iitwayo Mbinga Café katika ujazo wa gramu 40, gramu 50, gramu 250 na ujazo mkubwa zaidi kulingana na mahitaji ya wateja wao.

“Hizi ni bidhaa pekee ambazo zina ubora wa pekee na muonjo wa pekee kwa kuwa ni bidhaa zinazotokana na kahawa aina ya Arabica, haina mchanganyiko wa aina nyingine ya kahawa au vionjo vinginevyo, hivyo kuifanya bidhaa yetu kuwa ya pekee katika soko la kahawa,” anaeleza.

“Usindikaji ukishakamilika bidhaa hiyo husafirishwa hadi kwa wateja wao wanaopatikana nchi nzima kupitia kwa mawakala wetu walioko mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na visiwani Zanzibar,” anasema Mbunda. Kiwanda kina maghala na wafanyakazi wa kutosha kumudu kazi hiyo ya uhifadhi.

 

Ajira

Kuna ajira tofauti zinazotokana na uwapo wa kiwanda hicho. Kwanza, wananchi wengi wamejiajiri katika kilimo cha kahawa aina ya Arabica inayopendwa sana nchini na duniani.

Pili, kiwanda chenyewe kinatoa aina tatu za ajira; za kudumu, mikataba na za muda mfupi yaani vibarua. Jumla yao hufikia kati ya 250 na 300 kutegemea msimu ulivyo. Tatu, uwapo wa kiwanda hicho umesababisha ajira katika nyanja za uvunaji, usafirishaji na uuzaji mitaani.

“Kiwanda hiki kimekuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga pamoja na wilaya jirani katika kujipatia ajira zao hasa kipindi cha msimu wa uvunaji,” alisema Mbunda.

 

Mafanikio

Mafanikio ya kwanza ni namna kiwanda kilivyoendelea kuwa soko la uhakika kwa wakulima. “Kiwanda chenyewe kimepata mafanikio. Katika msimu wa 2015/ 2017 kiwanda kimeweza kuvuka malengo ya uzalishaji. Tulipanga kuzalisha tani 7,500 lakini tumezalisha 9,400 yaani ongezeko la tani 1,900,” anasema.

“Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 25 ya malengo ya msimu huu. Mafanikio hayo yanatokana na huduma nzuri zinazotolewa na kiwanda hicho kwa ushirikiano wa wafanyakazi na wadau wetu kwa ujumla, huduma bora kwa wateja wetu, nafasi kubwa na ya kutosha kuhifadhi kahawa za wateja na ufanisi wa mitambo yetu. Hali hii imewafanya wateja wengi kuhama viwanda vingine na kuleta kahawa zao katika kiwanda chetu,” anasisitiza.

Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa kahawa, Julius Mbunda anasema kiwanda hicho kwao ni mkombozi kwani kimewanufaisha kwa kuwapatia elimu bora ya utunzaji na usindikaji wa kahawa bora. “Tumefundishwa kuchuma kahawa iliyoiva vizuri na kuikoboa siku hiyohiyo na kuianika kwenye vichanja ili ikauke vizuri na kisha tunachambua kahawa mbovu na kuacha yenye ubora,” anasema.

Mkulima huyo anasema, elimu wanayopewa na wataalamu wa kiwanda hicho soko limeanza kuwa zuri kidogo ambapo kilo moja ya kahawa kavu inanunuliwa kilo moja kwa Sh2,500 wakati kahawa mbichi kilo moja ni Sh600.

Anatoa ushauri kwa Serikali iwasaidie wakulima kuwapatia pembejeo na kusimamia ubora ili wakulima waweze kufuata kanuni za uzalishaji bora kwani gharama za dawa za kahawa zipo juu.

Mkulima Gerald Ndunguru wa kijiji cha Luwahita wilayani Mbinga anasema kuwapo kwa kiwanda hicho kuna manufaa makubwa kwa wakulima, kwani wameweza kutunziwa kahawa yao vizuri pamoja na kumbukumbu za mazao yao ikiwa ni pamoja na kukopeshwa magunia ambayo yanawasaidia kutunzia kahawa zao na baada ya kuiuza ndiyo wanalipia gharama za utunzaji.

 

Changamoto

Kwa mujibu wa Mbunda kiwanda cha kahawa Mbinga, kama ilivyo kwa bidhaa au viwanda vingine kinakabiliwa na changamoto kadhaa na mojawapo ni uzalishaji mdogo wa kahawa kutoka kwa wakulima. Kiwanda kina uwezo mkubwa wa kukoboa na kusindika kahawa, lakini uzalishaji ni mdogo hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wa mitambo ikilinganishwa na uwezo mkubwa wa mitambo hiyo.

Changamoto nyingine ni miundombinu mibovu ya usafirishaji kutoka mashambani hadi kiwandani hivyo huathiri ubora wa kahawa. “Kahawa haitakiwi kuathiriwa na vumbi kwani litaathiri muonjo na hatimaye bei ya kahawa kwa ujumla,” anasema Mbunda.

Mbunda anasema changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa wakulima au wateja wanaodhani kuwa kiwanda hiki ni cha Serikali, hivyo wanataka gharama za ukoboaji ziwe chini kwa dhana kuwa kinapata ruzuku kutoka serikalini.

Pia, Mbunda alitaja changamoto nyingine kuwa ni mwamko mdogo wa Watanzania katika matumizi ya kahawa. Watanzania wengi si watumiaji wa kinywaji cha kahawa kutokana na dhana mbalimbali ikiwamo ile ya kudhani ni kinywaji cha watu wa tabaka la juu, na kwamba kinasababisha magonjwa ya shinikizo la damu.

 

Mikakati mipya

Anasema kiwanda cha kukoboa kahawa, kimejipanga katika kuboresha zaidi huduma zake kwa wateja ili kuwapatia kilicho bora ili kuhimili ushindani uliopo. Uboreshaji huo utalenga katika maeneo ya huduma kwa wateja, ufanisi zaidi katika uhifadhi wa mali za wateja, mitambo na elimu ya ubora wa kahawa kwa wateja ili kuwezesha kupata bei iliyo nzuri pale inapouzwa ndani na nje ya nchi.

Ametoa ushauri kwa Serikali isaidie kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya vijijini na hasa ile inayoelekea kiwandani ili kuwezesha kahawa kubaki katika ubora wake bila kuathiriwa na vumbi ikiwapo ghalani.

Kuhamasisha wananchi kuongeza uzalishaji kwa kupanua mashamba ya kahawa na hata kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi. Kuongeza maofisa ugani katika maeneo ya wakulima ili kuwasaidia wakulima katika zao hili la kahawa hali itakayoongeza uzalishaji na ubora wake.

Kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wa zao hili la kahawa ili kuwasaidia wakulima kumudu gharama za uzalishaji ambazo ni kubwa na ni vigumu kwao kuzimudu.

Kupunguza gharama za umeme kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za kilimo ili kuwapunguzia mzigo wakulima na kuviwezesha viwanda kujiendesha kibiashara zaidi.

Wito kwa vyama vya ushirika na wadau wengine kukitumia kiwanda hiki kwa kuwa ni kiwanda chao na kina uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora kwa wateja wake.