Viwango vya Olimpiki, Madola hapa hapa Tanzania

Muktasari:

  • Kila kitu kitamalizikia pale Kilimanjaro iwe kusaka viwango vya Olimpiki, Michezo ya Jumuioya ya Madola na hata vile vya mbio za dunia.

Sio muujiza lakini sasa unambiwa kwenda Ulaya itakuwa ni matakwa ya mwanariadha mwenyewe kutaka tu kubadili mazingira, lakini kama suala la kutafuta viwango, hakuna haja ya kusafiria nje.

Kila kitu kitamalizikia pale Kilimanjaro iwe kusaka viwango vya Olimpiki, Michezo ya Jumuioya ya Madola na hata vile vya mbio za dunia.

Tangu Uhuru 1961, wanariadha wa Tanzania walikuwa wakitoka kushiriki mbio za kusaka viwango ambavyo vinatambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), lakini sasa mambo ni hapa hapa.

Anayesubiriwa kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha marathoni na mbio ndefu (AIMS), Hugh Jones kuithibitisha Kilimanjaro International Airport Marathon (KIA Marathon) na baada ya hapo itakuwa na hadhi kama zilivyo mbio za marathoni za Berlin, Amsterdam na London.

KIA Marathon na IAAF

Mtaalamu wa masuala ya njia ambaye aliwahi kuwa mwanafunzi wa Jones katika upimaji njia kwenye riadha, John Bayo anasema kitu ambacho AIMS inaangalia kwanza ni njia ambazo zinatumika, lakini pia hali ya hewa ya mahali husika ambako haitakiwi kuwa na upepo mkali.

“Pia inatakiwa kuwa na nyuzi joto kati ya 21 na 25 ili kuwa na mazingira rafiki kwa mkimbiaji, ukiwa na vigezo hivyo na mtaalamu wa AIMS akathibitisha na kutoa taarifa IAAF , mbio zako zinakuwa za kimataifa na zitakuwa zikitoa viwango vya Olimpiki, dunia na hata madola,” anasema Bayo.

Anasema, njia ambayo inatumika kwenye mbio za KIA Marathon haina tofauti na ile ambayo inatumika kwenye mbio za Berlini, Amsterdam na London marathon ambako bingwa anaweza kukimbia kwa saa 2:03 na kuvunja rekodi kutokana na njia kuwa rafiki kwa mwanariadha.

“Kitaalamu, njia ambazo ni tambarare huwa na mazingira rafiki kwa wanariadha na wengi na huwa wanapenda kwenda kuchuana katika mbio ambazo njia za tambarare zinazosaidia kuvunja rekodi, KIA marathon imebahatika kwenye hilo,” anasema Bayo.

Mchakato utakavyoanza

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka anasema hiyo ni bahati kwa Tanzania kwani katika mbio zote zinazofanyika nchini hakuna ambayo inatoa viwango vya kufuzu kushiriki Olimpiki, Madola wala mashindano ya dunia.

“KIA Marathoni imekidhi vigezo hivyo, lakini sasa ili kujitofautisha na mbio nyingine kwanza inapaswa kusajiliwa ili zitambulike kimataifa, hatua hii inaanza kwa waandaaji kukutana na uongozi wa RT kwa ajili ya kuanza mchakato huo.

“Baada ya mbio za msimu huu (zinafanyika Novemba 19 ambazo zitakuwa mbio za kwanza nchini kuanzia KIA na kumalizikia hapo), tutajadili mpango huo,” anasema Mtaka.

Anasema kauli mbiu ya mbio hizo ni utalii kwanza, hivyo itakapokuwa ya kimataifa itavutia wanariadha wengi maarufu duniani kuja kushiriki kutokana na njia zake, lakini pia hali ya hewa ya mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambako zile za Kilomita 21 zitapitia Kilimanjaro na zile za Kilomita 42 zitapitia Arusha.

Wanariadha, Nchi watanufaika vipi

Mtaka anasema KIA Marathoni itakapopata hadhi hiyo, kwanza itapunguza mzigo wa gharama kwa Shirikisho na wanariadha katika mchakato wa kusaka viwango.

“Upande wa KIA wenyewe ambao ndiyo waandaaji kupitia kampuni yao ya KADCO, mbali na kutangaza mbio zao kuwa za kimataifa, lakini pia itautangaza Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.

“Wakazi wa Kilimanjaro, Arusha na mikoa jirani watanufaika kwa kufanya biashara, lakini pia nchi itaingiza fedha za kigeni kwani katika riadha wale mastaa wa dunia uwa watafuta mahali pa kufanyia mazoezi lakini pia wanapigia hesabu ya kushiriki mbio za kufuzu katika nchi watakayokuwa wameweka kambi.

“Huwa wanakuwa kambini si chini ya miezi sita, Tanzania tulikosa fursa hiyo kwani tunayo maeneo ambayo mazingira yake ni rafiki kwa kufanyia mazoezi ya riadha, lakini tulikosa mbio ambazo baada ya mazoezi watakimbia kwa ajili ya viwango.

“Hivyo mkimbiaji anaona kero kuja ‘kupasha’ Tanzania halafu aende Morocco au Ujerumani kwa ajili ya kushiriki mbio za viwango, ndiyo sababu tulikosa fursa hiyo, Kenya wanafanikiwa kwa kuwa wana mbio za Nairobi Marathon ambazo zina viwango, tukikamilisha usajili wa KIA Marathon tutakuwa ‘tumelamba dume’,” anasema Mtaka.

Mchakato wa usajili kuanza 2018

Kwa mujibu wa Bayo, IAAF huwa haina ugumu katika kuzipa hadhi mbio kuwa za kimataifa ili mradi tu njia zake ziwe zimethibitishwa na AIMS, lakini Mtaka anafafanua kwamba itakapopewa hadhi hiyo itabidi iwe na udhamini wa kutosha ikiwano kuweka zawadi nono kwa bingwa ili kuwavutia nguli wa riadha ulimwenguni.

“Ikiwezekana bingwa kwa kuanza wampe hata Dola 15,000 au hata 20,000 na kuendelea, hii itawavutia wanariadha maarufu duniani kuja kushiriki, lakini itakuwa ni miongoni mwa mbio chache ulimwenguni ambayo inaanzia uwanja wa ndege na kumalizikia uwanja wa ndege,” anasema.