Viwanja vya ndege ni msingi kuimarisha uchumi

Rais John Magufuli akizindua ndege mbili aina ya bombardier zilizonunuliwa kuliboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kuimarisha huduma za usafiri wa anga. Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Ili uchumi ukue kwa kasi ya kutosha kuondoa umasikini wa wananchi hata kulifanya Taifa lijitegemee kwa bajeti, ni lazima miundombinu hiyo iwepo kuwawezesha wananchi kusafirisha taarifa na bidhaa mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Upo uhusiano mkubwa kati ya maendeleo ya kiuchumi na miundombinu bora ya usafirishaji hasa wa anga.

Ili uchumi ukue kwa kasi ya kutosha kuondoa umasikini wa wananchi hata kulifanya Taifa lijitegemee kwa bajeti, ni lazima miundombinu hiyo iwepo kuwawezesha wananchi kusafirisha taarifa na bidhaa mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Mataifa mengi yaliyoendelea yana viwanja vikubwa vya ndege vinavyounganisha viwanja vya mikoani na mataifa mengine.

Marekani wanao uwanja unaohudumia watu wengi zaidi duniani, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hartsfield-Jackson Atlanta uliopo huko Georgia. Mwaka 2015, kumbukumbu zinaonyesha ulihudumia zaidi ya abiria milioni 101.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing ni miongoni mwa vyanzo vya mapato vya China inayotajwa kuwa ya pili kwa uchumi imara baada ya Marekani. Mwaka 2015 ulihudumia zaidi ya abiria 90.1 wakati zaidi ya abiria milioni 78 wakiutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow uliopo Uingereza mwaka jana.

Ingawa Serikali inaendelea kuboresha viwanja vya ndege mikoani, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) bado ni nguzo muhimu ya usafirishaji wa abiria na mizigo nchini na kimataifa.

Ripoti ya mwaka 2017 ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) iliyotolewa Januari, inaonyesha uwanja huo umechangia zaidi ya asilimia 40 katika usafirishaji wa abiria na mizigo kwa mwaka 2015 na 2016.

Mwaka 2016, takwimu zinaonyesha kati ya abiria milioni 4.9 waliotumia usafiri wa anga nchini, asilimia 49 walipita katika uwanja huo. Asimilia 21 ya abiria hao walipita katika viwanja vingine Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar (ZIA) ukitumiwa na asilimia 17 na asilimia 13 zilizobaki wakiutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Abiria wa anga waliongezeka kidogo mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Takwimu zinaonyesha kulikuwa na abiria milioni 4.8 mwaka 2015 ambao asilimia 48 kati yao walipita JNIA na viwanja vingine vikipitisha asilimia 20. Asilimia 19 ya abiria hao walipita ZIA asilimia 13 KIA.

Mizigo

Wakati zaidi ya abiria 100,000 waliongezeka mwaka 2016, tani 5,990 za mizigo zilizosafirishwa kwa anga zilipungua. Ripoti ya TCAA inaonyesha mwaka 2016, 24,030 pekee za mizigo zilisafirishwa zikilinganishwa na tani 30,021 za mwaka 2015. Upungufu huo ni sawa na asilimia 20.

Ukweli ni kwamba, asilimia 73 ya mizigo yote iliyosafirishwa mwaka 2016 kwend amikoani au nje ya nchi, ilipita JNIA ukifuatiwa na KIA uliosafirisha asilimia 11. Viwanja vingine vilisafirisha asilimia 10 na ZIA asilimia 6 pekee.

Hata tani 30,021 za mwaka 2015, asilimia 72 ya mzigo wote ulipita JNIA ukifuatiwa na KIA kwa asilimia 14 na ZIA asilimia nane huku viwanja vingine vikichangia kwa asilimia sita tu.

Licha ya ukweli kwamba viwanja vya ndege ni nguzo ya usafirishaji, bado viwanja hivyo nchini vina changamoto zinazowashawishi wananchi kutumia viwanja vya nchi jirani kusafirisha mizigo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari anatoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara wa samaki jijini Mwanza wanasafirisha mzigo wao kupitia Uwanja wa Entebe kwenda nje wakati Mwanza kuna uwanja pia.

“Si hao tu, hata wafanyabiashara wa maua huyasafirisha kwanza kutoka Kilimanjaro hadi Nairobi kabla ya kwenda nje ya nchi wakati kuna KIA. Kuna tatizo mahali,” anasema Johari.

Miongoni mwa sababu za wafanyabiashara na abiria kw aujumla kuvihama viwanja vya ndege vilivyopo nchini, wadau wanasema ni miundombinu isiyo rafiki na kukosa mvuto wa kibiashara.

Mkurugenzi mkuu wa Chama cha Wakulima wa Maua na Mbogamboga Tanzania (Taha), Aman Temu anasema katika mwaka wa fedha 2016/17, uzalishaji wao ulikuwa tani milioni 6.2 za ujazo na kati ya hizo asilimia 50 zilisafirishwa kwa ndege kwenda nje ya nchi.

Katika mzigo huo, anasema, asilimia 20 ulipitia Kenya na asilimia 30 JNIA na KIA. Ili kuongeza kiasi cha mzigo unaosafirishwa kupitia viwanja vya ndani, Temu anasema: “Ni muhimu kuimarisha miundombinu ya viwanja na uhifadhi wa mizigo.”

Mkurugenzi wa Mipango na utafiti wa Repoa, DK Abel Kinyondo anasema: “Katika kila nchi lazima kuwe na uwekezaji wa viwanja vya ndege hasa katika maeneo yenye shughuli za maendeleo au utalii.”

Anasema licha ya kuwa JNIA unaonekana kuwa nguzo kuu ya usafirishaji wa anga kwa abiria na mizigo, ipo haja kwa Serikali kuendelea kujenga na kuboresha viwanja vidogo vya ndege maeneo tofauti nchini.

“Ni kawaida kwa kila nchi kuwa na uwanja mkubwa wa ndege unaotoa huduma muda wote kwa ndege zinazotua na kuondoka kwenda nje ya nchi au mikoani,” anasema Dk Kinyondo.

Anasema, kadri teknolojia inavyokua na gharama kupungua, wasafirishaji wa baadhi ya bidhaa wataacha kutumia reli au meli badala yake watatumia usafiri wa anga.

Anatoa mfano wa wasafirishaji wa maua na mbogamboga kwamba ni ngumu kwao kutumia usafiri wa maji au reli kupeleka bidhaa zao nje ya nchi kwa sababu wakifanya hivyo; maua yatanyauka au matunda yataharibika.

Anasema mikakati ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga katika maeneo yote yenye vivutio vya kiuchumi.

“Kwa mfano, Mbeya wanalima maparachichi hivyo ni lazima Serikali iangalie jinsi ya kuboresha uwanja wake wa ndege na kuwa wenye mazingira mazuri kuvutia biashara ili itakapotokea likapatikana soko la nje kuwe na uwezekano wa kuyasafirisha matunda hayo moja kwa moja yakiwa bado na ubora,” anasema Dk Kinyondo.

Anasema kukosekana kwa miundombinu wezeshi katika baadhi ya mbuga za wanyama nchini na vivutio vingine vingine vya utalii kumesababisha idadi ya wageni kutembelea sana maeneo yaliyozoeleka kama Ngorongoro, Zanzibar na Kilimanjaro kutokana na urahisi wa usafiri.

“Kwa mfano, Hifadhi ya Mikumi haina umaarufu kama ilivyo Ngorongoro licha ya kuwa wanyama ilionao wanapatikana Mikumi pia lakini hakuna uwanja wa ndege. Ni ngumu sana kwa mtalii kushuka kwenye ndege na apande basi kuelekea Morogoro wakati kuna sehemu anafika moja kwa moja kwa usafiri wa anga,” anasema Dk Kinyondo.

Kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta za uchumi zitakazotoa ajira zenye staha, anasema upo ulazima kwa Serikali kuendelea kujenga viwanja vya ndege ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma zinazozalishwa maeneo tofauti nchini hivyo kupunguza umasikini.