Viwavi jeshi wanavyoacha kilio kwa wakulima

Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavi jeshi aina ya African army warms ambao kitaalamu wanajulikana kwa jina la Spodoptera  exempta.

Muktasari:

AINA
Sampuli za mdudu huyo alibainika kwa jina la  Spodoptera frugiperda au fall arymworm ambaye ni hatari na amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Wakati wakulima wengi wakianza kuona mwanga wa matumaini baada ya kuanza kunyesha mvua za masika, changamoto kubwa inayowaweka roho juu imeibuka katika baadhi ya maeneo nchini.

Katika maeneo mengi, badala ya wakulima kuona mimea yao ikishamiri kufuatia mvua kunyesha, wanastaajabu wanapokumbana na viwavi jeshi kwenye majani. Katika baadhi ya maeneo wadudu hao hatari wamefikia hatua ya kuhiliki mimea yote shambani hasa mahindi.

Mpaka sasa maeneo yaliyoripotiwa kuwa na idadi kubwa ya wadudu hao ni wilaya za Morogoro, Mbozi, Kilombero na Mvomero huku wakiacha kilio kikubwa kwa wakulima.

Ofisa Mazao wa Wilaya ya Mbozi, Lydia Sheonyela anasema wadudu hao wameonekana katika Kijiji cha Shilanga na vijiji vingine ambavyo ofisi yake anasema imeanza kuweka mikakati ya kuwadhibiti.

Katika Manispaa ya Morogoro, viwavi jeshi wameonekana kushambulia  mahindi na nyasi. Hali ni mbaya zaidi katika Uwanja wa Michezo wa Jamhuri, kwani wadudu hao wametafuna nyasi zote ni kuzua wasiwasi kwa wadau.

Mkulima wa mahindi kutoka Kata ya Mlimani, Neema Sanga ana huzuni kubwa baada ya shamba lake la eka mbili kuvamiwa na viwavi jeshi na kuharibiwa. Kinachomuuma zaidi ni kuwa mazao yalishaota na kumpa matumaini ya kuvuna.

“Shamba hili lilikuwa tegemeo langu na la familia, sijui cha kufanya kwa sasa,” anaeleza.

Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mimea kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Uvuvi, Cornelius  Mkondo anasema wana taarifa za uvamizi huo katika wilaya za Kilwa, Kilombero na Mvomero na kuwa dawa husika zimesambazwa kwa ajili ya kuwadhibiti.

Anasema Serikali mpaka sasa ina lita 1,000 za dawa ya kuua wadudu hao na imeagiza lita 4,000 ili kuongeza nguvu endapo wadudu hao watasambaa na kuwa tishio zaidi.

Mjue kiwavi jeshi

Mkondo anasema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavi jeshi aina ya African Army warms ambaye kitaalamu anajulikana kwa jina la  Spodoptera exempta. Mara zote Serikali imekuwa ikiwadhibiti wadudu hao wanapojitokeza.

Athari ya viwavi jeshi haishii kuharibu majani ya mimea, wadudu hao wanapokula majani wanatengeneza sumu aina ya ‘firenide’ inayodhuru mifugo inapokula majani yaliyoathiriwa.

Sumu hiyo husababaisha matumbo ya wanyama kujaa na hatimaye kuwasababishia vifo.

Mkondo anasema wadudu hao  hawafi kirahisi kwa kunyeshewa na mvua kama ambavyo watu wengi wanavyoamini.

Anasema kiwavi jeshi ni hatua ya ukuaji wa kipepeo anayeruka hasa nyakati za  usiku.

“Kipepeo huyo hutaga mayai na yanapoanguliwa hupitia katika hatua sita za ukuaji na kinapofikia katika hatua hiyo ya kiwavi ndiyo hushambulia mazao. Kikishavuka hatua na kuwa kipepeo hakina athari,” anafafanua.

Anasema wakiwa katika hatua ya kipepeo wana uwezo wa kuruka na kusambaa maeneo mengi na kutaga tofauti na wengine ambao ni hatari zaidi wanaodondoka.

Mtalaamu huyo anasema walipata taarifa ya uvamizi katika shamba la mwekezaji mkubwa wilayani Nkasi na walipofuatilia na kupeleka sampuli maabara mdudu huyo alibainika kwa jina la  Spodoptera frugiperda au Fall arymworm ambaye ni hatari na amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Kauli ya Wizara

Kutokana na unyeti wa suala hilo, Mkondo anasema wamewasiliana na  Shirika la Chakula Duniani (FAO), kwa ajili ya msaada wa kumdhibiti mdudu huyo kabla hajasambaa kwenye maneo mengi nchini.

“Pamoja na jitihada hizo,  wizara imekuwa ikichukua tahadhari za kudumu kwa kusambaza mitego 400 ya kubashiri uwepo wa wadudu hao na tumekuwa tukiihudumia mara kwa mara kwenye halmashauri zote ambazo zimekuwa zikikumbwa na tatizo la viwavi jeshi,” anasema na kuongeza:

“Pia, tunatoa mafunzo kwa wakulima wawili kwenye kila kijiji kilichopewa mtego. Vilevile, tunatoa mafunzo kwa  ofisa mtendaji na maofisa kilimo wa wilaya husika ili waweze kufuatilia na kutoa taarifa kwa mfuatiliaji wa kitaifa aliyepo Tengeru mkoani Arusha.”

Mkondo anasisitiza kuwa halmashauri kutumia mitego na mfumo wa ufuatiliaji na utoaji taarifa kwa wizara ili ichukue hatua za haraka kwa kusaidiana na wakulima.

“Zipo wilaya nyingine hazitumii vizuri mfumo huo wa ubashiri wa viwavi jeshi wa jamii (community based army warm forecasting) na hivyo kusababisha hali kuwa ngumu kwenye udhibiti wake hasa wakishasambaa kwenye maeneo mengi,” anaonya.

FAO inasema kiwavi jeshi aina ya Fall armyworm ameonekama pia katika nchi za Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Namibia Afrika ya Kusini na Zambia.

Kwa mujibu wa Redio ya Umoja wa Mataifa, FAO bado haijatangaza   kiwango kamili cha uharibifu katika nchi hizo, huku ikiongeza kuwa shirika hilo na  wadau wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wiki hii walitarajiwa kujadili udhibiti wa viwavi jeshi.

Taarifa za kitaalamu zinadai wadudu hao walitokea nchini Ghana na itawachuku muda watafiti kupata dawa sahihi na njia za kuwakabili.

Nchi kama Zambia imelazimika kutumia ndege kwa ajili ya kumwaga dawa za kuwaua wadudu hao katika maeneo walipo.

Aidha, nchi hiyo imetumia kiasi cha Dola za Marekani milioni tatu kudhibiti wadudu hao wa mazao waliovamia kiasi cha eka 130,000.