UCHAMBUZI: Vyama vya siasa vishindane kwa ubora wa sera

Muktasari:

“Upinzani nchini umejengwa katika msingi wa udhaifu wa CCM. Kufuatia uongozi mpya wa JPM, lazima sasa tujipange katika kushindanisha ubora.”

Maneno hayo ya Profesa Mkumbo ni kielelezo cha umuhimu wa kuwa na siasa za kisayansi katika kushindana. Mwanasiasa huyo anatuambia kwamba sasa ni zama nyingine, lazima vyama vya siasa vibadilishe mbinu za ushindani ili viweze kufikia malengo.

Wiki iliyopita baada ya Rais John Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mshauri wa chama cha ACT Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba;

“Upinzani nchini umejengwa katika msingi wa udhaifu wa CCM. Kufuatia uongozi mpya wa JPM, lazima sasa tujipange katika kushindanisha ubora.”

Maneno hayo ya Profesa Mkumbo ni kielelezo cha umuhimu wa kuwa na siasa za kisayansi katika kushindana. Mwanasiasa huyo anatuambia kwamba sasa ni zama nyingine, lazima vyama vya siasa vibadilishe mbinu za ushindani ili viweze kufikia malengo.

Kwa hotuba aliyoitoa Rais Magufuli wakati wa mkutano mkuu wa CCM, vyama vya upinzani vina kazi kubwa ya kupambana na chama hicho. Mambo yote ambayo wamekuwa wakiyazungumzia ndiyo anakwenda kupambana nayo.

Rais Magufuli aliahidi kwenda kusimamia suala la rushwa hasa wakati wa uchaguzi, chama kuiwajibisha Serikali yake, viongozi kutekeleza ahadi za chama na kuwasaidia wananchi katika kero mbalimbali.

Sehemu kubwa ya mambo hayo ndiyo ambayo yamekuwa yakililiwa na vyama vya upinzani. Huenda hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Profesa Mkumbo kuja na wazo mbadala litakalovisaidia vyama vya upinzani kuendelea kuwapo.

Kasi ambayo Rais ameanza nayo serikalini, inanifanya niamini kwamba atakwenda kufanya jambo la kipekee katika kubadilisha taswira ya chama tawala ambayo kwa hakika ilikuwa mbaya miaka mingi iliyopita.

Hii haiondoi umuhimu wa vyama vya siasa nchini. Bado vinahitajika ili kukikumbusha chama tawala majukumu yake, kukishauri na kutoa njia mbadala za kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Moja ya majukumu ya vyama vya upinzani ni kutoa njia mbadala kwa mambo yanayofanywa na Serikali ambayo wanadhani yangefanyika kwa namna nyingine yangeleta ufanisi katika jambo husika.

Uzoefu hapa nchini unaonyesha kwamba vyama vya siasa vimekuwa vikitumia upungufu wa chama tawala na Serikali yake kama ajenda. Hii ina maana kwamba wamekuwa ni wakosoaji tu badala ya kubuni njia mbadala ambazo wangetaka Serikali ifanye.

Kwa mfumo huo, vyama vya siasa vitakosa ajenda endapo chama tawala kitasahihisha makosa yake. Profesa Mkumbo ameliona hilo na kuja na njia bora ya kisayansi ya kuvitaka vyama kushindanisha ubora wa sera zao kwa wananchi.

Hilo likifanyika kikamilifu, tutakuwa na vyama vya siasa ambavyo vina nguvu. Vyama vitakuwa na ushawishi mkubwa hata bila kuwa madarakani. Tunataka tufike hatua ambayo vyama vya siasa vitakuwa vinabadilishana kuongoza nchini kama ilivyo kwa nchi za Marekani na Ulaya.

Kwa nchi kama Marekani, tunaona vyama vya Republican na Democratic vikibadilishana nyakati za kuongoza Serikali. Miaka ya hivi karibuni, alikuwapo Rais George H.W Bush (Republican), akafuatiwa na Bill Clinton (Democratic), baadaye George W. Bush (Republican) na sasa ni Barrack Obama (Democrats). Siyo kwamba vyama hivi vinakaa na kukubaliana kubadilishana. La hasha! Wananchi ndiyo wanaoamua kwa sababu wanaviamini vyama vyote, isipokuwa wanaangalia mtu anayekuwa amesimamishwa katika chama husika.

Hii ni hatua ya juu sana kwa nchi zenye ustaarabu wa kufuata demokrasia. Maamuzi ya watu yanaheshimiwa na mamlaka na taasisi mbalimbali za Umma. Tunahitaji pia kufika huko, tusijivunie kuwa na vyama vingi au kupigania uhuru wa mikutano ya hadhara wakati vyama havitumii uhuru huo ipasavyo.

Peter Elias ni mwandishi wa gazeti hili, anapatikana kwa barua pepe: [email protected] au simu namba 0763891422.