Vyama vya siasa vyakabana koo na CAG kuhusu kasoro kwenye hesabu zao

Muktasari:

  • Ripoti hiyo ya ukaguzi ya 2016/17 iliyotolewa hadharani na CAG, Profesa Mussa Assad ilibaini mambo makubwa mawili kwa upande wa vyama vya siasa, uwapo wa ufisadi katika suala zima la fedha na vyama kutokuwa na utaalamu katika utunzaji wa kumbukumbu za hesabu zao.

Wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini ufisadi ndani ya vyama vya siasa ikiwamo udhaifu katika utunzaji wa kumbukumbu za hesabu zao, baadhi ya vyama vimemjia juu vikidai anatumika kuvikandamiza.

Ripoti hiyo ya ukaguzi ya 2016/17 iliyotolewa hadharani na CAG, Profesa Mussa Assad ilibaini mambo makubwa mawili kwa upande wa vyama vya siasa, uwapo wa ufisadi katika suala zima la fedha na vyama kutokuwa na utaalamu katika utunzaji wa kumbukumbu za hesabu zao.

Katika ripoti hiyo, vyama vya CCM na Chadema vimepewa hati zenye shaka, huku Chama cha Wakulima (AFP), ADC, Demokrasia Makini, Chama cha Kijamii, NLD, Sauti ya Umma na TLP vikipata hati mbaya.

Miongoni mwa mambo yaliyosababisha Chadema kupata hati yenye shaka ni kufanya malipo ya masurufu ya Sh558.91 milioni ambayo hayakurejeshwa, ambapo CAG anasema fedha hizo zililipwa kwa waajiriwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ofisi.

Pia, CAG anasema ukaguzi umebaini marejesho ya mikopo kwa mwaka 2014/15 kuna kiasi cha Sh158,877,000 kilirejeshwa kutokana na mikopo iliyokuwa imetolewa kwa wafanyakazi wa Chama.

Japo anasema hakukuwa na mkataba wala nyaraka zinazothibitisha uhalali wa marejesho hayo, na kama yamerejeshwa kulingana na makubaliano. Kuhusu mkopo wa Sh2 bilioni ambao haukuthibitishwa mapokezi yake ndani ya chama, CAG anasema

Aprili 11, 2015, menejimenti ya Chadema (Mkopaji) iliingia makubaliano na mwanachama wake (mkopeshaji) kuhusu kukopeshwa kiasi cha Sh2 bilioni kwa shughuli za Chama.

“Hakuna nyaraka zinazoonesha kuwa kiasi cha mkopo walichokubaliana kilitolewa na kupokelewa na Chama husika. Zaidi niliona kwamba, ankara ya kodi (tax invoice) na.201508226 ya Agosti 26, 2016 ya kiasi cha Sh866.60 milioni ililipwa na mwanachama kwa niaba ya Chama kwa ajili ya mabango ya matangazo yaliyoletwa na mzabuni M/S Milestone International Co. Ltd,” anasema CAG.

Anaongeza: “Nje ya hilo deni, kiasi cha Sh715 milioni kililipwa kwa mwanachama kama marejesho ya fedha iliyokopwa kulipia ununuzi wa mabango bila ya kuambatishwa makubaliano ya kisheria. Yote hii ni kwa sababu chama hakijaandaa sera ya mikopo.”

Vilevile CAC amegusia makusanyo ya Sh2.30 bilioni ambayo hayakupelekwa benki na Chadema jambo alilosema ni kinyume cha kifungu na.15 (1) cha Sheria ya Usajili wa Vyama vya siasa.

Kuhusu manunuzi yaliyofanyika bila ushindanishi, CAG ameitaja Chadema kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma zenye thamani ya Sh24.21 bilioni ambayo yanakinzana na kifungu cha 16.2.2 cha Muongozo wa fedha za Chama kinachoeleza:

Kuhusu malipo yenye nyaraka pungufu Sh735.978 milioni, CAG amebaini vyama vya siasa vitatu (3) kati ya vyama tisa (9) vilivyokaguliwa vina malipo yenye nyaraka pungufu zenye thamani ya fedha hizo kinyume na miongozo ya kiuhasibu pamoja na kanuni Na. 86(1) na kanuni na.95 (4) ya Kanuni za fedha za Umma za mwaka 2001 ambazo zinaelekeza kila malipo yawe yameambatishwa na nyaraka sahihi.

INAENDELEA UK 20

INATOKA UK 17

Vyama hivyo ni pamoja na Chadema ambayo katika mwaka 2014/15 kulikuwa na Sh276.79 milioni zenye nyaraka pungufu, huku pia katika mwaka 2016/ 17 kuliwa na zaidi ya Sh240.16 milioni, hivyo kuwa na jumla ya Sh520. 44 milioni zenye upungufu wa nyaraka.

Chama kingine ni SAU ambacho kilikuwa na Sh639,100 zenye upungufu wa nyaraka na ADC chenye zaidi ya Sh89.49 milioni zenye upungufu wa nyaraka.

Hata hivyo akijibu hoja hizo za CAG, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Rodrick Rutembeka amemkosoa CAG akisema utaratibu wa kila mwaka ulikuwa ni kuwapatia ripoti ya awali ambayo hutoa maoni yao kabla ya kusambazwa.

“Sasa bahati mbaya safari hii hatujapata ripoti, ripoti hii nilioyonayo tumeomba kwa mbunge wetu,” anasema Rutembeka.

Ameongeza kuwa hesabu zilizotolewa zinaonyesha mapato ambayo hata chama hakijawahi kuyapata.

“Unajua kosa la Sh24 bilioni, sijui alikusudia kuandika bilioni mbili au vipi? Kwa hiyo kuna ‘over statement’. Yaani pesa iliyowekwa ni Sh20 bilioni, ni pesa ambayo chama hakijawahi kuzipata kwenye vyanzo vyote vya mapato kwa miaka mitatu mfululizo,” anasema kuongeza:

“Sasa hili jambo kweli halikuwashtua? Kwamba sisi tumekusanya Sh 14.1 bilioni, sasa kuna manunuzi ya Sh24 bilioni? Haiingii akilini. Tunachojiuliza ni kosa la uchapaji au ni kosa la makusudi ya kisiasa? Kwa minajili ya kisiasa, nchi yetu inakoelekea si pazuri, lakini sitaki kuamini hivyo.”

Anasema ukaguzi uliofanyika ni wa miaka mitatu ya 2014/15, 16 na 17 halafu umekuja kutolewa kwa mwaka mmoja hivyo kupotosha maana.

“Hii ni taarifa ya fedha ya taasisi za Serikali Kuu inayoishia Juni 30, 2017. Sasa unapounganisha miaka mitatu ya ukaguzi ukatoa taarifa kwa mwaka husika wa ukaguzi unapotosha,” anasema.

Anasema licha ya kupeleka hesabu za miaka mitatu mfululizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, wakaguzi hawakufika mpaka walipoletewa barua ya Msajili akihoji sababu ya kutopeleka hesabu.

“Tukaenda ofisi ya Msajili na uthibitisho wote kwamba tuliwasilisha hesabu zetu, lakini mkaguzi alikuwa haji. Ndipo walipoleta wakaguzi waliofanya ukaguzi kwa miaka mitatu mfululizo,: anasema Rutembeka.

Mbali na Chadema, CCM nako hakuko shwari kwani ukaguzi wa CAG kuwepo kwa mikopo ya Maendeleo kwa makampuni isiyo na faida Sh12.01 bilioni ambayo CCM ilitoa kwa kampuni nne ikiwa ni mikopo ya maendeleo.

“Hata hivyo, tumejifunza kwamba mikopo hiyo haina faida yoyote iliyoonekana imeingia kwenye chama. Pia, ilibainika kuwa, Sh80 milioni zilitambuliwa kama mapato ya uwekezaji katika taarifa za fedha kutoka Jitegemee Trading Company Limited lakini hazikuwa na kiambatisho kinachothibitisha kama ni gawio au kitu kingine,” anasema CAG.

CAG pia amebaini kutokuwepo kwa sera ya uwekezaji, akisema uwekezaji wa chama hicho upo katika hatari ya kutumiwa vibaya na malengo yaliyowekwa yanaweza yasifikiwe kama ilivyopangwa.

Vilevile CAG amebaini kuwepo kwa mikopo ya uwekezaji ya Sh455.97 milioni isiyokuwa na viambatanisho.

“Nilibaini kupitia ukaguzi wa taarifa za fedha za CCM kwa mwaka 2016/2017 kuwa, haina taarifa za kutosha juu ya mikataba, masharti, kiasi na sababu za kutoa msaada wa kifedha wa Sh455.97 milioni kwa Radio Uhuru,” anasema CAG.

“Kwa hiyo, siwezi kuthibitisha mikopo ya maendeleo iliyoenda kwenye matawi hayo. Menejimenti inashauriwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji hesabu (IFRS 12) kwa kuonyesha mpangilio wa mkataba, masharti, kiasi na madhumuni ya msaada wa kifedha wa Sh455,974,146.90 zilizotolewa kwa Radio Uhuru kwa mwaka,” amesema.

Pia, CAG amebaini mikopo ya ndani ambayo haikurejeshwa ya Sh337.14 milioni. CAG anasema menejimenti ya CCM ilikopa na kuhamisha fedha kiasi cha Sh337.14 milioni kutoka akaunti ya malipo ya pensheni kwenda akaunti ya katibu mkuu wa chama na kupokelewa kwa stakabadhi namba 156424.

“Hata hivyo, kiasi hicho hakijarejeshwa hadi wakati huu wa ukaguzi Februari 2018; matokeo yake, madai ya wafanyakazi wastaafu yanaweza yasilipwe kwa wakati,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za CCM, katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole alisema:“Mkaguzi akishakagua kunakuwa na maoni ya aliyekaguliwa. Yasome tena halafu unipigie. alisema Polepole.

Hata hivyo, maoni hayo hayakuonekana kwenye ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu.

Miongoni mwa vyama vilivyopewa hati chafu ni TLP na mwenyekiti wake, Augustine Mrema amekiri kuwepo kwa kasoro japo ripoti hiyo haijafika ofisini kwake.

“Najua kuna mambo yaliyosababisha tupate hati chafu. Kwanza ni jengo la ofisi yetu tulilolinunua kwa Sh80 milioni, ilitakiwa tubadilishe jina kutoka la aliyetuuzia na kuweka la chama. Kwa kuwa hatujabadilisha, mkaguzi akifika anaweka kosa,” anasema Mrema.

“Baada ya kununua jengo, tulitakiwa tulipe kodi ya Sh30 milioni kwa TRA, hatujalipa. Chama kwa sasa hakina fedha, japo mchakato umeshaanza. Bado kuna madeni ya hapa na pale ambayo tulikopa fedha za kuendesha chama, mkaguzi akiona hatujalipa anaweka kosa. Kwa hali hiyo ni lazima tupate hati chafu.”

Hata hivyo, Mrema anajivunia kwa kukamilisha deni la ununuzi wa ofisi, akisema japo chama ni kidogo, kina ofisi kubwa kuliko vyama vingine na wanaaweza kulitumia kibiashara.

“Lile jengo ni zuri kwa biashara, kwa hiyo tunajipanga kulipangisha. Kwa sasa tunapata ruzuku ya Sh200,000 kwa mwezi, kwa hiyo CAG akipiga domo ajue hela tunayopata. Kama kuna mtu amekula pesa atakamatwa,” anasema Mrema.

Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda amemshangaa CAG kuja kukagua chama chake wakati hakipati ruzuku ya Serikali.

“Tuwe wa kweli tu. Chama chetu hakina ruzuku ya Serikali hata Sh100. Hapa tuna cheti cha usajili tu unakuja kukagua makaratasi ya nini? Siasa yenyewe tumezuiwa kufanya, hata kufanya vikao vya ndani tunafuatwa. Tutapataje hela ya kujiendesha?” anahoji Akitanda.

“Wanasema wanafuata Sheria ya vyama vya Siasa. Mbona sheria hiyo inatupa haki ya kufanya siasa, lakini tunazuiwa? Kama hawatutaki wavifute vyama vya upinzani wabaki na CCM yao.”

Ameitaka Serikali kujitathmini kwa ripoti hiyo ya CAG, kabla ya kuvifuatilia vyama vidogo visivyopata ruzuku.

“Serikali yenyewe imepata hati chafu na inapata fedha za walipa kodi, wajitathmini kwanza wao, si kutufuatilia sisi ambao hatupewi hata Sh100,” anasema.