KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Vyombo vya habari huomba radhi; ndani, nje ya mahakama

Muktasari:

Yaani wafanyakazi wote wa MCL – kuanzia Mkurugenzi Mtendaji, Mhariri Mkuu, wahariri, wakurugenzi wa idara mbalimbali, waandishi wa habari hadi mwajiriwa wa nafasi ya chini kabisa – wanakuomba radhi.

Usiote. Fikiria tu siku moja gazeti la Mwananchi linakuomba radhi – wewe msomaji. Namaanisha Mwananchi Communications Limited (MCL), Kampuni ya kuchapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen – inakuomba radhi.

Yaani wafanyakazi wote wa MCL – kuanzia Mkurugenzi Mtendaji, Mhariri Mkuu, wahariri, wakurugenzi wa idara mbalimbali, waandishi wa habari hadi mwajiriwa wa nafasi ya chini kabisa – wanakuomba radhi.

Si hao tu. Kwa kuwa MCL ni mshikamano wa kampuni za vyombo vya habari chini ya kundi la Kampuni ya Nation Media Group (NMG), basi wafanyakazi wake pia watakuwa wamekuomba radhi.

Na kwa kuwa suala lenyewe ni la vyombo vya habari litakuwa linahusu uandishi wa habari unaopaswa kuongozwa kwa maadili na misingi maalumu ya kitaaluma – kimataifa na kitaifa; basi dunia ya waandishi wa habari – kwa ngazi zote – itakuwa imekuomba radhi.

Wote hao wangekuwa wamekukosea na sasa wanaomba radhi, lisingekuwa jambo kuu kwa mwandishi wa habari. Lakini mara kadhaa, mtu mmoja katika jumuia ya waandishi na vyombo vya habari huweza kusababisha mazingira ya kuomba radhi. Mmoja tu.

Sasa huyu hapa ndiye ataombwa radhi na MCL na waandishi na jumuiya zao: Ni Winifrida Igogo (56). Siyo kuombwa radhi peke yake. Atakabidhiwa kifuta machozi kwa madhira aliyosababishiwa.

Yote haya ni sehemu ya makubaliano kati ya Winifrida na MCL ili kumaliza shauri la daawa au shtaka namba 199 la mwaka 2015 kwa njia ya upatanishi. Shauri lilikuwa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.

Mbele ya Jaji R.A. Teemba (mpatanishi), Winifrida Igogo akiongozwa na wakili wake David Komeye, alikubaliana na MCL iliyowakilishwa na Meneja Utawala Idara ya Habari, Daniel Mwaijega aliyekuwa akiongozwa na wakili Imam H. Daffa kuwa shauri lake liishe kwa upatanishi, nje ya mahakama.

Labda unajiuliza kwanini MCL iombe radhi na kutoa kifuta jasho? Ni kwa sababu mfanyakazi wake wakati huo, Joseph Zablon aliandika taarifa katika toleo la Alhamisi, Septemba 10, 2015, ambayo ilimtaja Winifrida Igogo kuwa chanzo chake cha taarifa.

Taarifa ilimnukuu Winifrida akizungumzia masuala ya Bodi ya Ununuzi (tafsiri ya MJ) – Procurement and Supplies Professionals and Technicians Board (PSPTB) ambako anafanya kazi. Lakini Winifrida alikana kuhojiwa na mwandishi huyo.

Mhariri wa Jamii alianza uchunguzi. Katikati ya uchunguzi mwandishi alikiri kutomhoji Winifrida. Alisema kuwa alihoji mtu tofauti bali yule aliyemhoji alimtaka aonyeshe kuwa “amefanya mahojiano na Winifrida Igogo.” Naye alifanya hivyo.

Ni hivi: Mwandishi anamhoji A na kupata taarifa; lakini anaandika kuwa taarifa hizo aliambiwa na B. Halafu mwandishi anang’ang’ania kuwa alifanya hivyo “kwa nia njema.”

Hili ni kosa kubwa kitaaluma. Ni maasi dhidi ya misingi ya uandishi wa habari. Ni kukiuka ukweli na uadilifu ambayo ni baadhi ya misingi mikuu ya uandishi wa habari. Ni waraka wa kuomba kufukuzwa kazi; lakini bahati mbaya, baada ya kuchafua mazingira.

Hata kwa Zablon ndilo lililomkuta, alijipa waraka wa kufukuzwa kazi.

Suala hili lingeisha kwa mjadala kati ya Winifrida na MCL; na huenda bila kufika mahakamani – kwa kuomba radhi, kupeana mkono na kunywa pamoja kikombe cha kahawa. Haikuwa hivyo.

Wakati Mhariri wa Jamii amewasiliana na Winifrida, amekamilisha uchunguzi na kabla ya mjadala kuanza, Winifrida akawa amekwenda mahakamani.

Winifrida hakumuaga Mhariri wa Jamii kuwa anakwenda mahakamani lakini hakukosea hata kidogo kwani mahakamani pia kuna hatua ya upatanishi.

Ndivyo ilivyokuwa…Oktoba 30, 2016 – wiki iliyopita. Mbele ya Jaji Teemba (mpatanishi), pande hizi mbili zilikubaliana kumaliza mgogoro uliokuwepo kwa MCL kumuomba radhi mlalamikaji kwa maandishi na kumpa kifuta jasho kama fidia kwake na gharama za shauri alizotumia kwa hatua za kufungua shauri hilo Mahakama Kuu.

Hayo ndiyo madhara ya uandishi wa habari wa kutozingatia kanuni na misingi ya taaluma ingawa bado kuna wengi wengine wanaotaka kujifukuzisha kazi baada ya kusababisha hasara kwa kampuni zao.

Kama yupo mwingine wa kudhalilisha taaluma na kufanya dunia nzima ya waandishi wa habari kuomba radhi, natumaini siyo wewe.

Mwandishi wa makala haya ni Mhariri wa Jamii wa gazeti hili. Unaweza kuwasiliana naye juu ya makala haya au habari nyingine yoyote iliyoandikwa humu: 0763 670 229