WAKONTA KAPUNDA : Dakika 10 na Wakonta; ‘Mimi siyo mlemavu’

Wakonta Kapunda

Muktasari:

  • Hii ni tofauti kwa Wakonta Kapunda ambaye kwa kutumia kichwa chake pekee, kikiwa ni kiungo kimoja kinachofanya kazi katika mwili wake, amekuwa na uwezo wa kuandika muswada wa filamu ‘script’ na kuahidi kuendelea kuitumikia jamii yake.

Wapo binadamu wenye viungo vilivyokamilika lakini wanashindwa kuvitumia kufanya kazi za kuingiza kipato.

Hii ni tofauti kwa Wakonta Kapunda ambaye kwa kutumia kichwa chake pekee, kikiwa ni kiungo kimoja kinachofanya kazi katika mwili wake, amekuwa na uwezo wa kuandika muswada wa filamu ‘script’ na kuahidi kuendelea kuitumikia jamii yake.

Wakonta aliyejulikana hivi karibuni, hakuzaliwa mlemavu bali aliupata miaka minne iliyopita baada ya kugongwa na gari siku ya mahafali yake ya kidato cha sita Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe.

Ilikuwa ni siku iliyoanza kwa furaha kubwa na kumalizika kwa huzuni kuu. Ilikuwa ni siku iliyobadilisha maisha yake na kuthibitisha ule usemi ‘hujafa hujaumbika’.

“Wiki moja kabla sijafanya mtihani wa mwisho yaani siku ya mahafali Februari 2012, tukiwa tunajianda, mmoja wa mwanafunzi aliwasha gari na kuweka ‘reverse’ badala ya kukanyaga break alikanyaga mafuta, ilirudi nyuma kwa kasi hivyo kunigonga pamoja na baadhi ya wanafunzi,” alianza kwa kusema Wakonta wakati wa mahojiano na gazeti hili wiki hii Visiwani Zanzibar.

Wakonta (24) anayeshiriki katika mafunzo ya uandishi wa muswada ya Maisha Lab, visiwani humo kwa sasa, amezungumza mengi kuhusu maisha yake, kubwa zaidi ikiwa ni mbinu alizozitumia kung’amua jinsi ya kutumia simu kwa njia ya ulimi.

Wewe ni miongoni mwa wasichana wenye uthubutu, licha ya matatizo uliyonayo uliona kuna kitu unaweza kuifanyia jamii, unazungumziaje mafanikio yako?

Mafanikio yangu ni makubwa na ninafurahi sana kwa hatua ambazo nimezifikia japokuwa bado sijafanikiwa kuandika filamu, lakini nimejifunza mengi leo ni siku ya tano ya mafunzo haya, nimefanikiwa kuwa katika nafasi nzuri, nimejua namna ya kuandika muswada, wahusika katika kazi yangu na mengine mengi ambayo awali sikuyafahamu.

Ulijifunza vipi kuandika kwa ulimi?

Nilijifunza nikiwa nyumbani wakati huo mdogo wangu aliniachia simu kwa bahati mbaya au nzuri ile simu ikaita, simu ilikuwa karibu na mwili sasa wakati nahangaika kuipokea nikaigusa gusa ile simu ikakubali ikajipokea, nikagundua kitu kumbe simu ukiigusa hata na mwili inakubali, siyo kidole pekee.

Mdogo wangu alivyoamka nikwamwambia tufanye namna ili simu inifikie, akaishirikisha familia wakakubali wakaniwekea mito na vinginevyo nikaweza kutumia, nadonoa taratibu awali kichwa kiliuma, kizunguzungu, ulimi uliuma ila nilifanya kila siku nikazoea. Kwa sasa nina spidi nzuri na ninafanya kazi kubwa kupitia ulimi wangu ninaandika siku nzima.

Ulijifunza vipi kuandika muswada wa filamu na mbinu ulizotumia kupata nafasi uliyonayo?

Nimejifunza nyumbani, nilikuwa sijui muswada unaandikwaje nikajifunza kupitia nyumbani. Nilianza kuingia katika mitandao kuangaliwa waandishi wa Nollywood, Hollywood wanafanyaje, nikadonoa donoa kila sehemu mpaka baadaye nikapata wazo na hilo wazo likanifanya niandike muswada ambao ndiyo niliyotuma kwenye mashindano haya, nikachaguliwa kushiriki mafunzo.

Kwanini uliamua kuingia katika uandishi wa muswada wa filamu?

Filamu zina uwezo wa kugusa maisha yetu ya wakati wote ya jana ya leo yaliyopita na yajayo, kipindi naumwa nilikuwa naangalia filamu muda wote, kipindi hicho nilijua kwamba kupitia filamu unaweza kuhamasisha kubadilisha maisha yako na ukajua huzuni za watu.

Nikatamani niwe mmoja wa watu ambao wanawapa wengine faraja na wale waliopo katika wakati mgumu wanapata faraja, unamhamasisha mtu unampa mwangaza mpya unamwonyesha maisha mazuri zaidi maana unaweza kusema una maisha magumu kumbe mwenzako ana wakati mgumu zaidi.

Unakutana na changamoto zipi?

Changamoto zipo nyingi ila kwa kazi yangu kwa sasa hivi nikitaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine lazima awepo mtu, lakini pia kuandika kwa kuwa natakiwa kuwa nimekaa, hivyo nikiwa kitandani ninashindwa kufanya chochote, pia kifaa cha kuandikia nahitaji kupata simu nzuri zaidi itakayoniwezesha kufanya kazi zangu kwa urahisi.

Wadau wa filamu wamekupokea vipi?

Nimejulikana kipindi kifupi sana, nimekutana na watu wa bodi ya filamu wakanipokea na nikazungumza nao, wameniambia Tanzania kuna uhaba wa waandishi wa miswada, hivyo wamenipokea kwa mikono miwili, wakanichangia kiasi cha Sh5 milioni. Pia Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff) wameniahidi kwamba nikitoka kwenye mafunzo watanipa kazi za kufanya, wataniingiza rasmi kwenye taasisi yao.

Ukikutana na Rais Magufuli utamwambia nini?

Ni siku ninayoitamani, nikikutana na Rais John Magufuli nitamwambia filamu zina nguvu, Tanzania yetu itasonga mbele kupitia sanaa. Sisi waandishi, waigizaji na watayarishaji filamu tuna uwezo wa kuitangaza nchi masafa marefu.