MAONI YA MHARIRI: Wabunge jiandaeni vizuri kujadili Sheria ya Fedha

Muktasari:

Tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango awasilishe bajeti hiyo bungeni Alhamisi Juni 8, mwaka huu, wabunge wamekuwa wakiijadili kwa kutoa hoja mbalimbali za kuiboresha licha ya kwamba kwa sehemu kubwa suala lililochukua nguvu ya mjadala ni suala la madini kutokana na hatua ambazo Rais John Magufuli anachukua katika sekta hiyo.

Wakati mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ukielekea ukingoni, Muswada wa Sheria ya Fedha ambao ni kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Bajeti hiyo umewasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza.

Tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango awasilishe bajeti hiyo bungeni Alhamisi Juni 8, mwaka huu, wabunge wamekuwa wakiijadili kwa kutoa hoja mbalimbali za kuiboresha licha ya kwamba kwa sehemu kubwa suala lililochukua nguvu ya mjadala ni suala la madini kutokana na hatua ambazo Rais John Magufuli anachukua katika sekta hiyo.

Baada ya mjadala huo unaotarajiwa kuhitimishwa Jumanne ijayo, Muswada wa Sheria ya Fedha utasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa na wabunge, kisha kupitishwa na kuwa sheria.

Lengo la sheria hiyo ni kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na mapato ya Serikali ili ziendane na Mpango wa Bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha.

Ni kupitia sheria hiyo, Bajeti ya Serikali ambayo wiki iliyopita ilishangiliwa na baadhi ya wabunge na kuelezwa na Spika wa Bunge kuwa haijapata kutokea, pia ikakosolewa na wabunge wengine katika maeneo mbalimbali, itasimamiwa na kutekelezwa kwa kuwa sheria hiyo ndicho chombo cha kuitafsiri katika vitendo.

Kutokana na umuhimu wa sheria hiyo, ndiyo maana tunawataka wabunge wajiandae kwa kuisoma kwa umakini na kuijadili kwa kina na weledi ili kuhakikisha sheria inatungwa bila ushabiki kama ambavyo baadhi ya wabunge wameonekana wakati wa mjadala wa bajeti husika.

Mathalani, wakati Bajeti ikiwasilishwa Dk Mpango alisema wafanyabiashara wadogo kwenye maeneo yasiyo rasmi watatambuliwa na kupewa vitambulisho, suala ambalo wabunge na wananchi kwa ujumla waliliunga mkono, wakati katika muswada huo limeunganishwa na adhabu kali ambayo bila shaka hawataipigia makofi.

Katika muswada huo wa sheria ya fedha, suala hilo limeongezewa kifungu cha adhabu, kuwa watakaoshindwa kujiandikisha walipe faini isiyopungua Sh200,000 na isiyozidi Sh1 milioni au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka miwili gerezani.

Si lengo letu kusema kwamba suala hilo lisiwe na adhabu au lipingwe, bali tunataka kuonyesha kwamba katika baadhi ya maeneo kilichosomwa katika Bajeti, ni tofauti na kilichomo kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha, ama kuna kitu kimeongezewa au kupungua, hivyo wabunge wasipokuwa makini masuala mengine yanaweza kuwapita na kuleta athari kubwa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa pale wabunge wanapoondoa siasa na kuwa makini na kuonyesha mapengo yaliyomo kwenye muswada wa sheria, mambo hubadilika na kuleta unafuu kwa wananchi walio wengi bila kuathiri wigo wa kodi uliopangwa na Serikali.

Mfano katika Bajeti ya mwaka 2016/17 wabunge, tena wakiwa wa CCM peke yao, walipinga kamati za fedha na mipango kuondolewa katika kusimamia mchakato wa zabuni kwenye halmashauri.

Katika muswada huo, Serikali ilikusudia kuondoa jukumu la kamati ya fedha na mipango katika usimamizi wa masuala ya ununuzi ya halmashauri lakini wabunge walisimama na kipengele hicho kikaondolewa.

Suala jingine ambalo lilijitokea katika mapendekezo ya Sheria ya Fedha mwaka jana, ilikuwa adhabu kubwa ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua Sh3 milioni kwa watu ambao wangepatikana na makosa ya kutokudai risiti za elektroniki, lakini baada ya majadiliano faini ilipunguzwa na kuwa Sh30,000.