Wachezaji Kili Stars na kiu ya ubingwa wa Chalenji

Muktasari:

  • Mashindano ya Chalenji yanachezwa kwa mfumo wa makundi mawili kisha timu mbili zitakazofanya vizuri kwenye kila kundi zitapata nafasi ya kutinga nusu fainali kisha fainali ambayo itatoa bingwa.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘ Kilimanjaro Stars’ tayari kimetua nchini Kenya kwa ajili ya kushindania taji la mashindano ya Chalenji yaliyoanza jana hadi Desemba 17.

Mashindano ya Chalenji yanachezwa kwa mfumo wa makundi mawili kisha timu mbili zitakazofanya vizuri kwenye kila kundi zitapata nafasi ya kutinga nusu fainali kisha fainali ambayo itatoa bingwa.

Kundi A lina timu tano ambazo ni Tanzania Bara, Libya, Rwanda, Zanzibar na Kenya. Kundi B ni Uganda,Zimbabwe,Burundi,Ethiopia na Sudan Kusini. Huenda timu moja ikahamishiwa Kundi B baada ya Zimbabwe kujitoa.

Spoti Mikiki ilibonga na wachezaji wa Kilimanjaro Stars wakielezea wamejiandaaje na nini Watanzania tutarajie kutoka kwao.

Erasto Nyoni, fulubeki

Niko na timu ya Simba...Kikosi cha Kilimanjaro Stars tuko sawasawa, tunaweza kufanya vizuri kwenye mashindano ya Chalenji kutokana na wachezaji wengi kuwa na viwango vya juu.

“Wachezaji wengi hii itakuwa mara yao ya kwanza hivyo watakuwa na shauku ya kutaka kuonyesha vipaji vyao, tumekuwa pamoja kwa muda nadhani hapatakuwa na tatizo la muunganiko.

Kwa mimi, haya yatakuwa mashindano yangu ya zaidi ya mara tano kuitumikia Kili na mara yangu ya kwanza ilikuwa 2006 nchini Ethiopia.

Abdul Hilal, Winga

Ninachezea Tusker ya Kenya, nimepanga kuitumia vizuri hii nafasi ambayo nimeipata kwa kuaminiwa na kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara.

“Ninachokiamini ni kuwa safari moja huzaa nyingine hili nimekuwa nikipenda sana kulisema, kuitwa kwangu kwa mara ya kwanza na Mayanga kulianzisha hatua nyingine ya kuendelea kuaminiwa.

“Sitaki kumwangusha Ammy ambaye ameona ninafaa kwenye kikosi chake pamoja na kuona ninafaa kuwa mwakilishi wa wachezaji wengine ili nikalipiganie Taifa, nitacheza kwa kujitolea ili kuisaidia timu.

Hamis Abdallah, kiungo

Mimi ni kiungo mkabaji wa Sony Sugar ya Kenya, nimefurahi kurejea kwenye nchi ambayo ninacheza ligi...ushirikiano na kujituma kutatupa mafanikio na kutwaa Kombe la Chalenji.

“Wachezaji tumekuwa na ushirikiano wa uchezaji, kuna muda anaweza asiwepo mchezaji fulani kwenye nafasi yake lakini kutokana na ushirikiano wetu huwa kuna mtu ambaye anaweza kwenda kuziba lile pengo.

“Ushirikiano huo nadhani watu waliuona kwenye mchezo wetu wa kirafiki uliopita dhidi ya Benin, japo hii sio Taifa Stars ila ina wachezaji wengi ambao walikuwa kwenye kikosi kile.”

Gadiel Michael, fulubeki wa kushoto

Niko na Yanga, lakini ni wazi huu ni wakati wetu wa kufanya kitu kwa ajili ya Taifa kwa kuzingatia hiki ni kipindi ambacho Tanzania imekosa kombe hilo kwa muda mrefu.

Mara ya mwisho kwa Tanzania Bara kuchukua ubingwa wa Chalenji ni 2010...Binafsi ninaona kuwa hiki ni kizazi chenye wachezaji ambao wanaweza kuliletea heshima Taifa, tunaweza kufanya kweli kwenye hayo mashindano, naomba wapenda soka watuunge mkono.”

Peter Manyika JR, kipa

Ninachezea Singida United. Sisi kama wachezaji, tunakwenda Kenya tukiwa na njaa ya kupata matokeo ya ushindi katika kila mchezo ambao tutakuwa tunacheza.

“Njaa ya kupata matokeo inaweza kuifanya timu yoyote kucheza kwa moyo na kutokata tama hata kama tutakuwa nyuma, mpira ni dakika tisini.”

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, fulubeki

Mimi ni nahodha msaidizi wa Simba, nasema kucheza ugenini hakuwezi kutufanya tushindwe kupata matokeo kwa sababu hali ya hewa ya Kenya na kila kitu vinafanana na nyumbani.

Hatutakuwa na kisingizio, kuwa kwetu Kenya ni kama tuko nyumbani sioni kama kutakuwa na tatizo, kila mmoja wetu naona yupo kwenye hali nzuri.

Juma Kennedy, sentahafu

Ninakipiga Singida United, na hii ni mara yangu ya kwanza kuwa kwenye timu ya Taifa na ni fursa kwangu kuendelea kuonyesha uwezo wake zaidi. “Watanzania wengi wananifahamu kupitia Singida ambayo nimekuwa nikiichezea, kupitia timu ya Taifa itakuwa ni kama daraja la kunifanya nitambulike zaidi kimataifa, pamoja na kuwa nawaza hilo lakini pia jukumu langu la kwanza litakuwa kuisaidia timu.

Boniphace Maganga, fulubeki wa kulia

Ninachezea Mbao FC ya Mwanza, ukweli itakuwa aibu kama tutarudi mikono mitupu, ni bora tukikosa sana tuambulie hata nafasi ya pili na sio kuishia hatua ya makundi.

“Binafsi sipendi kushindwa, nachukia sana kuona timu yangu inapoteza hivyo hata kama nikiwa mchezaji wa akiba nitajitahidi kuwahamasisha wenzangu ili tufanye vizuri.

Shiza Kichuya, kiungo/winga

Ninachezea Simba. Ninachokiona, hatuna sababu ya kupoteza kwenye mashindano hayo kutokana na uchu tulio nao wa kutwaa ubingwa.

“Kinachotakiwa,ili kutwaa ubingwa inatakiwa tuwe makini kwenye uchezaji wetu, kama tukiwa tunashinda michezo yetu ya makundi itatufanya kuingia na morali ya ushindi kwenye nusu fainali ambayo inaweza kutusaidia kutinga fainali. “Sioni kama inashindikana kurudi na taji nchini, tumejitolea kupigania Taifa letu.”

Raphael Daud, Kiungo

Niko na klabu ya Yanga, kikubwa ninawataka Watanzania kutuunga mkono kwa sababu hata sisi hatupendi kufanya vibaya kwenye mashindano.

“Hakuna mchezaji hata mmoja ambaye anatamani kuona timu yetu ikifanya vibaya, kwa pamoja tunaweza kuifanya Kili kufanya vizuri kikubwa kila mtu afanye majuku yake.”

Elias Maguli, straika

Nilikuwa ninachezea Dhofar lakini mkataba wangu umekamilika, ukweli nimepania kufunga mabao mengi kila nitakapokuwa napata nafasi ili kuisaidia Kili kupata matokeo ya ushindi.

Katika eneo langu la ushambuliaji natakiwa zaidi kufunga mabao, kila nitakapokuwa nafunga nitakuwa natengeneza mazingira kwa timu yangu kupata matokeo ya ushindi.

“Siwezi kabisa suala la wapi nitatua maana ni kweli makataba wangu umemalizika na timu yangu Oman, nawaza zaidi kwa sasa kulisaidia Taifa langu alafu hayo mengine yatafuata maana kama ofa ninazo za kutosha ni uchaguzi wangu, wapi patanifaa.

Yohana Mkomola, straika

Mkomola nilikuwa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana cha Serengeti Boys kilichoshiriki mashindano ya Afrika kwa Vijana, nitatumia nafasi hii kujifunza.

“Bado ninakuwa kiuchezaji, nahitaji kujifunza mengi kupitia ushindani, kama nitapata nafasi ya kucheza itakuwa ni faida kwenye ukuaji wa soka langu na kama sintopata basi itakuwa faida nyingine.

“Hata ile hatua ya kuitwa timu ya Taifa halafu ninafanya mazoezi ninajifunza baadhi ya vitu vya uchezaji kutoka kwa kaka zangu ambao wamenitangulia.

Kelvin Yondani, beki wa kati

Niko Yanga kama beki wa kati, tutajituma na hapatakuwa na mtihani wa maelewano kwa sababu wachezaji wamekuwa pamoja kwa muda sasa tofauti na vipindi kadhaa nyuma na kulikuwa na panga pangua ya kikosi.

“Wachezaji wanapokuwa pamoja kuna namna nzuri inajengeka maelewano ya kucheza, kuliko ile ya leo wengine kesho wengine hufanya wachezaji kuwa na wakati mgumu wa kuelewana, kwa maandalizi ambayo tumefanya tutafanya vizuri.”