Wadau: Barabara zisafirishe korosho

Muktasari:

Bei ya korosho ghafi iliongezeka kutoka Sh1,200 iliyokuwapo msimu wa mwaka jana hadi kufikia Sh3,500 kwa kilo mwaka huu.

Katika msimu wa mauzo ya korosho mwaka huu, wakulima wameonyesha kufurahia matunda ya kazi za mikono yao kutokana na bei nzuri.

Bei ya korosho ghafi iliongezeka kutoka Sh1,200 iliyokuwapo msimu wa mwaka jana hadi kufikia Sh3,500 kwa kilo mwaka huu.

Mafanikio haya yanaelezwa kuchangiwa na ushindani wa sokoni uliochangamshwa na wafanyabiashara kutoka Vietnam, usimamizi mzuri wa Bodi ya Korosho pamoja na kuondolewa kwa baadhi ya tozo ambazo siku za nyuma zilikuwa zinapunguza mapato ya mkulima na mfanyabiashara.

Baadhi ya wadau wanasema minada ya korosho imekuwa na mizengwe ambayo ilitengenezwa makusudi ili kuwanufaisha wanunuzi na baadhi ya wasimamizi lakini safari hii Bodi ya Korosho ilitoa miongozo mizuri likiwamo sharti la kumtaka mnunuzi alipe angalau asilimia 25 wakati wa zabuni.

Hata hivyo, mafanikio hayo yameelezwa kujengewa mazingira ya kuwa endelevu hatimaye kuifanya sekta hii ndogo ya kilimo kukua zaidi na kusaidia juhudi za kupambana na umaskini na kukuza Pato la Taifa.

Katibu Mkuu wa Jukwaa la Asasi za Kiraia zinazoshulika na kilimo (Ansaf), Audax Rukonge anasema kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kuboreshwa ili kurahisisha ufanyaji biashara wa korosho na kuendeleza mafanikio yanayopatikana kwa wakulima na Serikali.

“Kwa dhati, naipongeza Serikali pamoja na wadau wengine kwa kuchukua hatua zilizochangia kuimarika kwa bei ya korosho msimu huu. Ni ongezeko kubwa na litawanufaisha wakulima ila kuna mambo kadhaa ambayo yakifanyika, nafikiri, tutadumisha ongezeko la bei na kupanua wigo wa manufaa kwa wakulima, Serikali na Watanzania wengine,” anasema Rukonge.

Anakumbusha, tunapaswa kukumbuka kwamba bei nzuri tunayoifurahia sasa ni ya korosho ghafi. Anasema uuzaji wa korosho ghafi tunatakiwa kuupinga kwa asilimia 100 na njia nzuri ya kuupinga ni kuwa na viwanda vya kuzibangua ili kuongeza mnyororo wa thamani ambao utatengeneza ajira na vipato kwa watu wengi zaidi.

“Tanzania inatakiwa ibangue korosho yake yenyewe,” anaongeza.

Anaeleza, korosho za Tanzania ni miongoni mwa zenye ubora zaidi duniani ambazo zingekuwa na thamani kubwa zaidi kama kungekuwa na viwanda vya kubangua na kusindika nchini.

Anasema kusafirisha na kuuza korosho ghafi nje ya nchi ni sawa na kupeleka nafasi za ajira pamoja na teknolojia kwa wenzetu ilhali wananchi wanazihitaji kujikwamua kiuchumi.

Ili kukabiliana na changamoto ya kusafirisha korosho ghafi, Tanzania ina mpango wa kujenga viwanda vitatu vya kubangua na kusindika korosho Mtwara, Tunduru na Mkuranga.

Viwanda hivi vitajengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Wakfu wa Korosho (CIDTF), taasisi ilichoanzishwa kwa Sheria ya Udhamini ya mwaka 2002 kwa malengo ya kukuza maendeleo ya sekta ya korosho na kilimo kwa ujumla kwa kugharamia utafiti, pembejeo za kilimo, usindikaji, masoko ya ndani na nje na matangazo.

Hata hivyo, Rukonge anasema huenda viwanda hivi visiwe na manufaa makubwa sana kwani vitaajiri watu wachache tu. Anasema viwanda vilivyopangwa ni vile vinavyotumia mitambo mikubwa, nadhani havitasaidia sana kwa mikoa mitatu.

Anapendekeza kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati ili kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa wakulima na wadau wengine wa korosho na kwamba siyo lazima viwanda hivyo vijengwe na mfuko wa wakfu.

“Jambo muhimu ni watu wengi wajiajiri kwa kulima na kubangua kisha mazao hayo yaende kwenye viwanda vikubwa. Serikali inaweza kuhusisha sekta binafsi na wadau wengine ili kujadili namna ya kulitekeleza hili na hatimaye kilimo cha korosho kikawa na tija zaidi,” anasema Rukonge.

Jambo jingine muhimu, kwa mujibu wa Rukonge, Serikali inapaswa kuruhusu usafirishaji wa korosho kwa njia ya barabara kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kuepuka ucheleweshaji wa bidhaa hiyo kwa wanunuzi wanaosafirisha nje ya nchi.

Hivi karibuni, Serikali ilielekeza wanunuzi wa korosho kusafirisha mizigo yao kwa kutumia Bandari ya Mtwara ili taasisi zingine zinazofanya shughuli zake huko waweze kukusanya kodi na tozo tofauti zilizopo lakini kuna uhaba. Inaripotiwa, vyombo vya baharini katika bandari ya Mtwara umesababisha shehena kusubiri kwa muda mrefu katika maghala, hali ambayo inaathiri majukumu ya wanunuzi kwa wateja wao na wafadhili na hatimaye kuhatarisha uimara wa bei uliopo.

“Tukumbuke kwamba meli nyingi za mizigo zinasimama katika Bandari ya Dar es Salaam ambako ndiko mzigo mwingi unaishia,” anasema.

Kutokana na hali hiyo kampuni ya Vietnam, Starnuts, ilishindwa kusafirisha zaidi ya tani 3,800 za korosho kwa sababu meli ilivyotarajiwa kusafirishia bidhaa mzigo wake mpaka Dar es Salaam ilikuwa imejaa kwa muda usiojulikana.

Kadhalika, iliripotiwa kuwa kampuni 107 zimejitokeza kununua korosho na takwimu zinaonyesha takribani tani 141,000 zimenunuliwa lakini ni kati ya tani 54,000 na 57,000 pekee zilizopata kibali cha kusafirishwa. Hiyo inamaanisha zaidi ya tani 90,000 bado hazijasafirishwa nje ya Mtwara.

Ukosefu wa fedha kutokana na kuchelewa huko uliwaondoa wanunuzi wengi na kubakisha wanunuzi wachache wa ndani kwenye vituo vya minada, hali iliyoashiria kwamba huenda bei ikaanza kushuka.

Kusafirisha korosho kwenda Bandari ya Dar es Salaam kupitia barabara kunatarajiwa kufanya biashara ya korosho kuwa endelevu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba itaharakisha mzunguko wa biashara kwani wauzaji wangepeleka bidhaa zao nje ya nchi kwa haraka na kurejesha mikopo yao na kurudi kununua mazao zaidi.

Bandari ya Mtwara pia inasemekana kuwa haiwezi kuhudumia mavuno makubwa ya korosho mwaka huu kutokana na changamoto za miundombinu yake duni na kutoweza kupokea meli kubwa.

Korosho ni zao la pili (baada ya tumbaku) kwa kuliingizai taifa fedha za kigeni. Kwa mujibu wa Benki Kuu (BoT), kwa mwaka ulioishia Septemba, korosho ziliingizia Tanzania Dola 182.3 milioni (zaidi ya Sh364.6 bilioni). Mazao mengine yanayouzwa nje na kuchangia fedha za kigeni ni chai, katani, karafuu, tumbaku na kahawa.

Wakati korosho zikichangia kiasi hicho ndani ya muda huo, thamani ya mauzo ya bidhaa asilia nje ya nchi ilikuwa Dola 822.6 milioni (zaidi ya Sh1.65 bilioni). Tanzania inatarajia kuzalisha zaidi ya tani 200,000 katika msimu wa mavuno mwaka huu ikilinganishwa na tani 125,000 zilizozalishwa mwaka jana kadiri Serikali inavyosambaza mbolea na kuboresha mfumo wa kununua mazao hayo.

 

Ukurasa wa mazingira bora ya kufanya biashara umerudi kwenye gazeti la Mwananchi kila Alhamisi ukiwa na lengo la kuunga mkono jitihada za wajasiriamali nchini. Kwa maoni tuma ujumbe mfupi kwenda namba 0786240172 ukianza na neno RB kwa gharama za kawaida za ujumbe au baruapepe: [email protected]