Wadau: Kiswahili hazina ya Afrika na dunia

Muktasari:

  • Pia, ni lugha ya kwanza ya kibantu inayozungumzwa na watu wengi katika bara hili.
  • Lugha hii imeanza kutanua mawanda yake katika nchi nyingine duniani.

Kiswahili ni lugha adhimu na fahari ya bara la Afrika. Ni lugha ya pili inayozungumzwa na watu wengi Afrika baada ya Kiarabu.

Pia, ni lugha ya kwanza ya kibantu inayozungumzwa na watu wengi katika bara hili.

Lugha hii imeanza kutanua mawanda yake katika nchi nyingine duniani.

Inapendwa kwa sababu ya urahisi wake wa kujifunza na pia kama lugha ya kurahisisha mawasiliano na watu wengi zaidi hasa katika bara la Afrika.

Katika kongamano la kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu) lililofanyika Disemba mwaka jana, wadau mbalimbali kutoka nchi 13 duniani walikutana jijini Dar es Salaam kujadili mafanikio na mikakati ya kukuza lugha ya Kiswahili duniani.

Rais wa Chaukidu, Mahiri Mwita Anasema lugha hiyo ni rasilimali ambayo inaweza kuuzwa katika soko la utandawazi na kujipatia fedha za kigeni na kwamba ufundishaji wa lugha hiyo siyo suala la kitaaluma pekee bali inaweza kuwa fursa ya kibiashara.

Anasema kuna haja ya kukiweka Kiswahili katika namna mpya kwa ajili ya kupelekwa sokoni na kuuzwa kwa wageni.

Kufanya hivyo, anasema Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki zitapata fedha za kigeni kutokana na lugha hiyo.

“Taaluma ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ni taaluma mpya ambayo lazima tujiandae kwa ajili ya kuuza sokoni,” anasema.

Mwita ambaye anaishi Marekani, amewataka Watanzania na Afrika kwa ujumla kujivunia lugha ya kiswahili na kuitumia kama rasilimali ambayo ni kivutio cha utalii kwa wageni kutoka mataifa mengine hasa Ulaya na Marekani.

“Sisi ndiyo tunaofundisha Kiswahili, miaka ijayo watakuwa wanazungumza wengi. Lazima tujiulize tumejipangaje kukabiliana na wale ambao tunawafundisha, wasije wakatupiku siku zijazo,” anasema.

Kiswahili zawadi ya Afrika

Akizungumza katika kongamano hilo, Balozi wa Kiswahili Afrika, Salma Kikwete aliwataka Waafrika kukumbatia utamaduni wao, badala ya kutukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi kwa kutumia lugha zao na kuiacha lugha ya Kiswahili.

Anasema Waafrika wamepewa zawadi ya lugha ya Kiswahili na Mwenyezi Mungu, hivyo wasione haya kuitumia popote watakapokwenda.

“Tunapopata nafasi kwenye majukwaa ya kimataifa tusisite kukitumia Kiswahili, hiyo ndiyo njia moja wapo ya kukuza lugha yetu,” anasema balozi huyo na kusisitiza kwamba siku moja bara zima la Afrika litazungumza Kiswahili.

Anasema Kiswahili kinazidi kukua siku hadi siku na mataifa mengine yanaona umuhimu wa lugha hiyo.

Vyuo vya kimataifa vimeanza kufundisha Kiswahili, jambo linalosaidia kuongeza idadi ya wataalamu na watumiaji wa lugha hiyo.

Wamarekani wakichagua Kiswahili

Ilivyo ni kuwa Kiswahili kimeambatana na utamaduni wa watu na uchumi wao.

Watumiaji wa lugha ya hii wana utamaduni unaofanana na kupitia lugha hii watu wa mataifa mengine wanajifunza utamaduni wa watu wa pwani ya Afrika Mashariki ambako ndiyo asili yake.

Sababu hizo ndizo zilizoifanya Marekani kukichagua Kiswahili kuwa moja ya lugha 12 za kimkakati ambazo Taifa hilo kubwa duniani litazitumia kurahisisha mawasiliano yake na mataifa mengine duniani.

Mwita anasema Kiswahili kimechaguliwa kwa kuwa ni miongoni mwa lugha nyeti kwa ajili ya usalama na ustawi wa kiuchumi wan chi hiyo.

Anaeleza kuwa Wamarekani wamechagua lugha hizo ili waweze kuchangamana na watu wa mataifa mengine, hivyo wameona Kiswahili ndiyo lugha pekee itakayowawezesha kuchangamana na bara la Afrika.

Kiswahili kufundishwa kwa mabalozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Susan Kolimba, anasema Serikali imeandaa mpango wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mabalozi na wanadiplomasia waliopo hapa nchini.

Anasema mafunzo hayo ambayo yataanza kutolewa Februari mwaka huu ni hatua ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa kwa wizara yake, ili kuhakikisha Kiswahili kinakua na kuenea katika nchi zao.

Anasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kimechaguliwa kuratibu mafunzo hayo na sasa kinakamilisha taratibu kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo.

Dk Kolimba anasema Serikali inahimiza matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi, kwa sababu lugha hiyo ndiyo kielelezo cha Taifa hili na utamaduni wake.

“Zaidi ya watu milioni 200 duniani kote wanazungumza lugha ya Kiswahili; ni lugha ya pili baada ya Kiarabu kuzungumzwa na watu wengi Afrika, lakini ni lugha pekee ya Kibantu inayozungumzwa na watu wengi Afrika,” anaeleza.

Anasema Kiswahili ni lugha ya Taifa kwa nchi za Tanzania, Kenya na DRC; anatoa wito kwa nchi nyingine za Afrika kukifanya Kiswahili kuwa lugha yao ya Taifa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye anasema wanaendelea vizuri na mpango wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mabalozi na kwamba watatumia mfumo maalumu wa kuwafundisha.

Ili kukuza Kiswahili, anasema tayari chuo chake kimeanza kuitumia lugha hiyo katika vikao vyake vyote pamoja na utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali. Anasema hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

“Chuo chetu kina mchango mkubwa katika kukua kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu tunafundisha lugha hiyo kwa watu wa mataifa mbalimbali ambao nao wanakwenda kuitumia katika nchi zao,” anasema Profesa Anangisye ambaye amesimikwa rasmi kuongoza chuo hicho baada ya kustaafu kwa mtangulizi wake, Profesa Rwekaza Mukandala.