Wadau: Malipo ya madeni ya walimu yatawaongezea ari ya kufundisha

Tuesday February 13 2018

 

By Tumaini Msowoya, Mwaanchi [email protected]

Moja ya kilio kikubwa cha watumishi wa umma nchini hususani walimu, ilikuwa malimbikizo ya madeni yao.

Wachambuzi wanasema matumaini ya muda mrefu ya kutolipwa yalisababisha kupungua kwa ari ya kufundisha na hivyo kushusha kiwango cha elimu.

Hata hivyo, Serikali imetegua kitendawili cha madai yao. Inasema malimbikizo ya madai ya watumishi wa umma 27,389 yenye thamani ya Sh 43.39 bilioni yatalipwa pamoja na mshahara wa Februari, 2018 kwa mkupuo mmoja.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, anasema fedha hizo zinajumuisha madai ya watumishi ya zaidi ya miaka 10 iliyopita, kwamba majina ya watakaolipwa yatatangazwa kwenye magazeti.

Kati ya watumishi 82,111, walimu ni 53,925 waliokuwa wakidai Sh 53.9 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 42.27 ya madai yote.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Yahaya Msigwa, anasema malipo hayo kwa walimu yatasaidia kuinua kiwango cha elimu.

“Ni hatua nzuri kwa Serikali kulipa madai ya wafanyakazi na kwa sekta ya elimu, suala hili litawaongezea ari ya kufanya kazi zaidi na hivyo, kiwango cha elimu nchini kitaongezeka,” anasema.

Anasema walimu walikuwa wakidai madeni mengi yakiwamo ya uhamisho, kupandishwa vyeo, kupandishwa madaraja na mishahara jambo ambalo lilipigiwa kelele kwa muda mferu.

“Huenda malimbikizo haya ya madeni yalisababisha walimu kukosa mori na matokeo yake kuzifanya shule za Serikali kushindwa kuingia hata kwenye orodha ya shule 20 bora kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, tena hata huu wa kidato cha nne wa juzi. Kwa hiyo hatua hii nzuri,”anaeleza.

Dk Msigwa anasema kimsingi elimu ni sekta muhimu zaidi kwa maendeleo ya nchi.

Anasema nchi yoyote inayotaka kupiga hatua kimaendeleo lazima ikubali kutumia gharama kubwa kuwekeza kwenye elimu ikiwamo, malipo mazuri kwa walimu.

“Ukitaka taifa liwe maskini na lisipige hatua basi usiwekeze kwenye elimu, ujue walimu wanaweza kufanya mgomo na hata usijue kama wapo kwenye mgomo. Mambo ya kimya kimya mabaya, unaweza kuja kushtukia kwenye matokeo,”anasema.

Walimu na motisha

Wachambuzi wa masuala ya elimu wanasema walimu wanapopewa haki yao kwa wakati, wanaongeza ari ya kufanya kazi zaidi.

Hivi karibuni, utafiti wa KiuFunza, uliofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza, ulionyesha kwamba kutoa motisha ya fedha kwa walimu kunaweza kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Dk Jimson Sanga anasema ikiwa malipo yaliyoahidiwa na Serikali yatatolewa, kiwango cha elimu kitaongezeka.

“Shule binafsi zinafanya vizuri na zinaongoza kwenye mitihani ya kitaifa kwa sababu zimewekeza kwa walimu kwa hiyo, Serikali inayo kazi kubwa ya kuhakikisha walimu hawakati tamaa ya kazi yao,” anasema.

Dk Sanga anasema walimu wanapaswa kuwa na mishahara ya kutosha, marupurupu, uhakika wa makazi hasa kwa wale walio shule za vijijini pamoja na mikopo ya masharti nafuu kwa wale watakaoweza kumudu.

Anasema kulipa madeni ni mwanzo mzuri pia lazima kuwe na mpango endelevu wa kuhakikisha kuwa kundi hilo linaangaliwa kwa ukaribu ili kushughulikiwa pale linapokuwa na malalamiko.

Malipo ya wafanyakazi

Kwa mujibu wa Dk Mpango, watumishi wasiokuwa walimu 28,186 waliokuwa wakidai jumla ya Sh73.6 bilioni sawa na asilimia 57.7

Anasema Serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara hadi kufikia Julai Mosi mwaka jana ilikuwa na madai ya mishahara yenye jumla ya Sh 127.6 bilioni kwa watumishi 82,111.

Anaeleza kuwa kati yao walimu walikuwa 53,925 huku wakidai Sh 53.9 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 42.27 ya madai yote na wasiokuwa walimu 28,186 walikuwa wakidai jumla ya Sh73.6 bilioni sawa na asilimia 57.7 ya madai yote.

“Madai haya yalikuwa ya muda mrefu mengine yakiwa ya kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2017,” anasema Dk mpango.

Anasema madai hayo yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa na kuchelewa kurekebishiwa mishahara.

Dk Mpango alisema madai ya watumishi 27,389 kati ya 82111 yenye jumla ya Sh 43.39 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 34 ya madai yote ya Sh 127.6 bilioni yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na kulipwa bila marekebisho.


Advertisement