Wadau: shule za kata zinaweza zikiwezeshwa

Muktasari:

Sekondari hizo zilianzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, zikiwa na lengo la kukuza wigo wa wanafunzi wanaoingia elimu ya sekondari baada ya kumaliza ngazi ya msingi.

Ni zaidi ya muongo mmoja sasa tangu kuanzishwa kwa mpango wa shule za sekondari za kata nchini.

Sekondari hizo zilianzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, zikiwa na lengo la kukuza wigo wa wanafunzi wanaoingia elimu ya sekondari baada ya kumaliza ngazi ya msingi.

Agosti 25 mwaka 2014, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alisema wakati anaingia madarakani mwaka 2005 ni asilimia 10 pekee ya wanafunzi waliokuwa wakichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika shule za Serikali, hali iliyosababishwa na uchache wa shule.

“Kwa miaka mingi hatukujenga shule mpya za sekondari, na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndiyo kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na sera ya shule za kata,” alisema.

Hata hivyo, sera hii haikupokelewa kwa mikono miwili na walio wengi kwa kuwa pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi katika ngazi ya sekondari, hapakuwapo mazingira bora ya kuwapokea wanafunzi hao

Shule nyingi zilijengwa kwa nguvu ya utashi wa kisiasa pasipo kuwa na miundombinu muhimu na hata walimu. Matokeo yake, shule nyingi za kata zikawa taabani kitaaluma huku zikizalisha idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli mitihani ya mwisho ya kidato cha nne. Hiki kikawa kilio cha wadau wengi wa elimu na hata sasa hali ya mambo katika baadhi ya shule haijatengemaa.


Mabadiliko

Hata hivyo, hali ya mambo imeanza kubadilika kwa baadhi ya shule hizo kufanya vizuri kwenye mitihani ya taifa, kiasi cha kuwapa matumaini baadhi ya watu kuwa kama zitaangaliwa kwa jicho la karibu, zinaweza kuwa mkombozi kwa walio wengi.

Mwaka 2011 wanafunzi 20 walitunukiwa zawadi baada ya kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita, huku kati yao saba wakiwa waliosoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za sekondari za kata. Huo ukawa mwanzo wa dalili njema kuwa shule za kata zinaweza kutoa wahitimu bora kama ilivyo shule nyingine za Serikali na za binafsi.

Hata mwaka huu katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karbuni, mwanafunzi ambaye ni zao la sekondari ya kata, Zuhura Sakaya aliibuka mwanafunzi bora katika masomo ya sanaa kwa kushika nafasi ya pili kitaifa.

Sakaya alipata matokeo hayo akitokea Shule ya Wasichana ya Feza, alikopata ufadhili baada ya kufanya vyema katika matokeo yake ya kidato cha nne akitokea katika shule ya sekondari ya kata ya Turiani iliyopo Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Sakaya anasema hakupata nafasi hiyo kama muujiza alijituma tangu akiwa kidato cha nne na kuweka nia kuwa atafaulu kwenda chuo kikuu akitokea katika shule za kata zinazobezwa.

Anasema hakufahamu kama siku moja atakuja kusoma katika shule kama Feza, ilipotokea hakustuka sana kwa sababu aliamini alianzisha mwendo na wengine wamempokea kijiti kuziendeleza.

“Nilijipanga kuungana na wanaoitwa wanafunzi wanaojisikia fahari kutaja majina ya shule zao, tofauti na wao waliosoma kata katika wanaozunguka kutaja majina ya shule zao, kwa kusoma kwa bidii kwa sababu elimu ya juu huwakutanisha wote pamoja.

“Nilijua huko tutapimwa kwa uwezo na siyo kwa shule, aliyesoma kata na ya gharama inayothaminika wote watajadiliwa, kujadili, kudahiliwa pamoja, nimefanikiwa, ” anasema Sakaya.

Sakaya anafafanua juhudi hizo zilimfanya awe miongoni mwa wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2013 kwa shule za Serikali za mkoani Dar es Salaam na kushika namba 10.

Aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati Zuhura akisoma shule kabla ya kuhamishwa, Asha Juma anasema anajivunia matokeo ya mwanafunzi wao huyo.

Anasema tangu akiwa hapo anamfahamu kuwa ni mwanafunzi anayejituma akitaka kujua zaidi na zaidi katika masomo yake.

“Nakumbuka hata katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2013 alitutoa kimasomaso kwa kufanya vizuri Kinondoni, ninafurahia matokeo yake na nilitegemea atafika mbali, ” anasema Juma.

 

Nini kifanyike kuboresha shule za kata?

Mkuu wa shule ya Turiani, Beatrice Mhina Ramadhani anasema jambo muhimu ni kuboresha miundombinu.

Anasema licha ya juhudi za walimu, bado mindombinu hasa ya kujifunzia imekuwa ikikwamisha juhudi hizo.

Anafafanua kuwa kuna wanafunzi wanao uwezo, lakini wanashindwa kuendelea au kufanya vema katika masomo kutokana na kukosa vitu muhimu.

“Shule za kata zinaongoza kuwana wanafunzi kutoka katika familia zenye kipato cha chini, hivyo Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wenye mahitaji maalumu, ikiwamo wale wanaoshindwa kulipa ada, kukosa vifaa na wenye maradhi, ” anasema Ramadhani.

Anasema chakula cha mchana nacho ni muhimu ili kuwapa nguvu wanafunzi ya kusoma kwa sababu imeonekana wazi wengi wao wanachoka kwa sababu ya njaa.

“Tunajituma sana, lakini matokeo yetu yanakuwa chini kutokana na kuchangiwa na vitu vingi ikiwamo mazingira magumu ya kusomea, uduni wa maisha kwa baadhi ya wazazi unaosababisha wanafunzi washindwe kuweka mkazo katika masomo, ”anasema Ramadhani.

Mratibu wa mtandao wa elimu Tanzania (Tanmet), Catherine Sekwao anasema ili shule hizo zifanye vizuri zaidi, lazima kuwe na vifaa vya kusomea na kufundishia.

“Imeonekana zinaweza, ili zifanye vizuri zaidi mikakati zaidi inahitajika kutoka hapa zilipo kusonga mbele, ” anasema Sekwao.

Jovita George, mkazi wa Tabata Bima anasema: “Waanzishe utaratibu wa kuwapa chakula cha mchana, waboreshe miundombinu kama maabara, vitabu vya kusomea, malipo mazuri na ya wakati kwa walimu, semina za mara kwa mara kwa walimu ili kukuza uelewa wao.

“Kama watafanya vitu kwa mazoea, wakaenda puta kufundisha kwa sababu rais aliyepo sasa hataki mchezo, akiondoka nchi na shule za kata zitarudi kule kule zilikotoka, mzazi unamsomesha mtoto miaka minne bila kuwa na uhakika anachokifanya shuleni, ” anasema George.