Wadau na macho tofauti kwa maofisa elimu wilaya, mkoa

Muktasari:

Maofisa elimu ni miongoni mwa viongozi wanaosimamia masuala yanayohusu elimu kwenye maeneo husika.

Maofisa elimu ni miongoni mwa viongozi wanaosimamia masuala yanayohusu elimu kwenye maeneo husika.

Kuna ofisa elimu wa ngazi ya wilaya, mkoa pia wapo waratibu elimu kata wenye jukumu la kuratibu na kusimamia elimu ngazi ya kata.

Pamoja na majukumu ya maofisa hawa, wapo baadhi ya wadau wanaokosoa kuwapo kwa nafasi hiyo, wakisema haina tija katika maendeleo ya elimu nchini.

Hata hivyo, kuna wengine wanaosema kutokana na unyeti wa sekta ya elimu, nafasi hizo hazina budi kuendelea.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga anasema viongozi hao ndio kiungo muhimu cha mawasiliano yanayohusu elimu.

“Ni watu muhimu na bila hao elimu inaweza kuyumba, kama ilivyo kwa waganga wakuu wa wilaya na mikoa, ndivyo ilivyo kwa maafisa elimu,”anasema.

Anasema sio rahisi wakurugenzi kusimamia elimu moja kwa moja kutokana na kutokuwa na maadili ya kiualimu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Christopher Magomba anasema utitiri wa maofisa elimu uliopo haupaswi kuwapo.

“Ufanisi ungeweza kufanywa kwa kuwa na kiongozi mmoja tu, sasa kuna ofisa elimu taaluma, watu wazima, takwimu, vifaa, msingi, sekondari na wengine wengi. Hii ni gharama hata kwa uendeshaji,”anasema.

Anasisitiza kuwa lazima wizara iwe na mfumo mzuri wa kuwapata maofisa elimu watakaosaidia kuifanya taaluma ikue na siyo kuizorotesha.

Mchambuzi wa elimu, Dk Frank John anasema siyo maofisa elimu ndiyo ambao wanajukumu la kusimamia ubora wa elimu kwenye maeneo husika, kuratibu na kuendesha shughuli zote muhimu kwenye sekta hiyo. “Tunaweza kuwa bora kielimu kwa kuwa na viongozi bora wenye taaluma na weledi wa kusimamia elimu, hatuwezi kuendeshwa kisiasa kwenye suala la elimu hapo tutakuwa tunapotea,” anasema.

Anabainisha kuwa kinachotakiwa kufanywa ni kutengeneza namna nzuri ya kuwapata maofisa elimu.

Tofauti na ilivyo kwenye taaluma nyingine, ofisa elimu lazima awe mtu mwenye taaluma ya elimu, uzoefu wa kazi na asiye mbabaishaji.

“Tukisema ofisa elimu aombe kazi tutashindwa kuwapata maofisa elimu wazuri, watapatikana wasomi wasio na maadili ya kiualimu, hawa hawatafaa kuongoza elimu,”anasema.

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Patrick Myovela anasema utaratibu wa zamani uliokuwa ukitumika kuwapata maofisa elimu bila upendeleo, ndio unapaswa kuendelea kutumika.

Anasema zamani viongozi hao walipatikana kwa uzoefu wa kazi, weledi na sifa ya elimu jambo lililosaidia kuboresha kiwango cha elimu.

“Akipatikana ofisa elimu asiye na uzoefu haitakuwa rahisi kuifahamu kazi yake kwa sababu hajui chochote kuhusu ualimu. Tunataka yule aliyeanza chini akapanda vyeo hadi kufikia nafasi ya kuwa ofisa elimu,” anasema.

 

Majukumu ya ofisa elimu wa mkoa

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uboreshaji wa Elimu, majukumu ya ofisa elimu ngazi ya mkoa ni kuwakilisha Wizara katika ngazi zote za kielimu katika eneo lake la kazi.

Kiongozi huyo anapaswa kufafanua na kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo katika elimu ya awali na msingi, sekondari, mafunzo ya ualimu, elimu ya watu wazima na vituo vya ufundi stadi.

Majukumu mengine ni kuwa mshauri mkuu wa Katibu Tawala wa Mkoa husika kuhusu masuala yote yahusuyo elimu.

Mwongozo huo pia unataja majukumu mengine kuwa ni kushughulikia upanuzi wa elimu ngazi ya elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya ufundi, elimu ya watu wazima, elimu ya sekondari na elimu ya ualimu.

Ofisa elimu ndiye kiongozi anayepaswa kusimamia maslahi ya walimu kwenye eneo mkoa wake.

Pia ndiye anayeratibu, kusimamia, kuendesha na kutathmini mitihani ya darasa la nne na la saba, kidato cha nne na cha sita, mafunzo ya ualimu pamoja na mitihani ya ufundi katika mkoa wake akishirikiana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) na wizara.

Majukumu mengine ni kufuatilia utekelezaji wa taarifa za ukaguzi wa shule na vyuo.

Pia kuchambua takwimu za elimu katika mkoa kwa ajili ya mipango ya maendeleo katika ngazi za wilaya, mkoa na Taifa.

Anapaswa kusimamia na kuendesha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza katika mkoa wake.

Mwongozo huo unamtaja ofisa elimu wa mkoa kuwa ni kiongozi anayepaswa kuratibu na kusimamia uhamisho wa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari ndani na nje ya mkoa wake.

Majukumu mengine ni kuruhusu kukariri kwa wanafunzi shule za msingi hadi darasa la 6 kulingana na taratibu zilizopo.

Mwongozo huo unataja majukumu mengine kuwa mwakilishi wa ofisa elimu kiongozi wa elimu katika mikutano ya bodi inayohusu uendeshaji, mipango ya maendeleo, nidhamu, mapato na matumizi ya fedha za shule za sekondari na vyuo vya ualimu katika mkoa wake

 

Majukumu ya ofisa elimu wa wilaya

Anapaswa kutoa ushauri wa kitalaamu kwa Halmashauri ya Wilaya, Mji au Manispaa kuhusu masuala yote ya kielimu.

Ndiye anayedhibiti matumizi ya fedha za elimu kwa mujibu wa miongozo ya fedha za Serikali.

Mwongozo huo wa uboreshaji wa elimu unamtaja kiongozi huyo kuwa anapaswa kushughulikia upanuzi wa elimu katika ngazi ya elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, mafunzo ya ualimu, elimu ya watu wazima na vituo vya ufundi stadi.

Pia, kufuatilia kwa madhumuni ya kutathmini maendeleo ya elimu katika wilaya.

Mwongozo huo unamtaja ofisa elimu kwamba anapawa kutayarisha na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya elimu kila mwaka.

Kuhakikisha kwamba shule zote zinaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Majukumu mengine ni kuhimiza udhibiti wa nidhamu ya walimu na wanafunzi wilayani sambamba na kusimamia maslahi ya walimu.

Anatakiwa kufuatilia utekelezaji wa taarifa za ukaguzi wa shule na vyuo, kusimamia maendeleo ya taaluma katika wilaya, kukusanya, kuratibu na kuchambua takwimu za elimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo katika ngazi ya shule, wilaya, mkoa na Taifa.

 

Ofisa taaluma wilaya

Anatakiwa kufundisha kila inapolazimika kufanya hivyo kwa lengo la kuonyesha mfano wa ufundishaji bora kwa walimu pamoja na kudumisha ualimu wake.

Anatakiwa kufuatilia na kuhimiza uanzishaji na matumizi bora ya vituo vya walimu.

Pia, kushirikiana na wilaya katika kupanga na kuendesha semina, warsha na mikutano ya elimu ya ualimu.

Kiongozi huyo atatakiwa kuandaa mipango ya mafunzo ya walimu kazini na kushiriki katika kuwafundisha.

Mwongozo huo unasema, ofisa elimu taaluma wa wilaya ndiye anayepaswa kuhimiza na kushiriki katika kuendesha mashindano ya taaluma kwa wanafunzi wa shule za msingi.