Wadau wanahitaji zaidi ya taarifa za fedha za kampuni kujiridhisha

Muktasari:

  • Wakaguzi wa hesabu za fedha huandaa taarifa hizi kwa ajili ya wadau mbalimbali kama vile wateja, mamlaka za fedha na nyinginezo, wawekezaji na wanahisa.

Ni jambo la kawaida kwa kampuni kutoa taarifa zake kwa kipindi fulani. Mara nyingi hutoa taarifa za robo, nusu au mwaka mzima zinazoonyesha mambo mbalimbali ya fedha hasa faida na hasara.

Wakaguzi wa hesabu za fedha huandaa taarifa hizi kwa ajili ya wadau mbalimbali kama vile wateja, mamlaka za fedha na nyinginezo, wawekezaji na wanahisa.

Kimsingi, kampuni hizi hutoa taarifa za fedha. Kwa miaka ya karibuni wadau wanaohitaji taarifa za kampuni wameongezeka vivyo hivyo taarifa zinazohitajika hivyo haja ya kuandaa taarifa pana zenye ufafanuzi wa zaidi ya zile za fedha pekee.

Katika taarifa za fedha, kampuni huonyesha afya yake kifedha kwa maana ya kupata faida au hasara ndani ya kipindi husika. Huonyesha mtiririko wa fedha zilizoingia na kutoka.

Pamoja na mambo mengine taarifa hizi huonyesha gharama za uzalishaji, mapato hatimaye faida au hasara. Kwa baadhi ya wadau kinachojalisha ni faida tu. Hata hivyo kwa wengine taarifa za faida tu hazitoshi. Wanahitaji kujua faida husika imetengenezwa vipi na hata pengine imetumikaje.

Hii ni pamoja na kujua athari za mchakato mrefu wa utengenezaji faida kwa mazingira, jamii na uchumi kwa jumla. Hali hii huhitaji kampuni kuandaa taarifa nyingi zaidi.

Mazingira

Katika mchakato wa kuzalisha faida athari mbalimbali hutokea kwenye mazingira. Hii ni kwa sababu ya matumizi ya malighafi. Pia uzalishaji, usambazaji, matumizi na ubakizaji wa kilichozalishwa hufanyika katika mazingira kwa maana pana ya ardhi, maji na hewa.

Haya yote huweza kuathiri mazingira. Huweza kuharibu uoto wa asili, kuchafua ardhi, hewa na maji hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi. Hii huathiri maendeleo endelevu.

Hivyo ni muhimu kampuni zikatoa taarifa za namna shughuli zao zinavyoaathiri mazingira na zinazofanya kurekebisha uharibifu unaotokea katika mazingira na jamii inayozunguka miradi yao. Hii ni muhimu katika muktadha wa maendeleo endelevu.

Tukumbuke hatukuirithi dunia kutoka kwa mababu zetu bali tumeikopa kutoka kwa watoto na watoto wa watoto wetu. Tukiiharibu katika harakati zetu za kuzalisha mali ni wao watakaobeba mzigo mzito wa kuisafisha au kuishi katika dunia chafu.

Kimaadili na haki si sahihi mababu kula zabibu mbichi halafu wajukuu wabebe mzigo wa kupigwa ganzi la meno.

Athari kwa jamii

Uzalishaji wa bidhaa na huduma hufanyika katika jamii inayozunguka mradi. Kampuni za aina zote huweza kuathiri mazingira, utamaduni na mpangilio wa maisha kwa ujumla.

Ni muhimu kampuni zikatoa taarifa za athari zilizojitokeza au zinazoweza kujitokeza kwenye jamii inayoizunguka. Uzalishaji unaweza kuvuruga mfumo wa jamii na familia, huweza kuleta watu wapya na, mila na desturi mpya katika jamii. Pia, huweza kuongeza msongamano katika huduma za jamii kama maji, afya, elimu, barabara hata makazi kwa ujumla. Ni lazima kampuni zieleze athari hizi kwa jamii husika.

Leseni za kijamii

Pamoja na leseni za biashara zilizopo kisheria, kampuni hazina budi kutafuta na kupata leseni ya kijamii. Hii si kipande cha karatasi kama leseni za biashara bali ni kukubalika katika jamii husika.

Kukubalika huku hutokana na mambo mengi kama vile namna kampuni inavyorejesha katika jamii inakochuma faida zake. Hii hutokea katika mfumo wa wajibu wa kampuni kwa jamii.

Wajibu huu huchukua sura nyingi kama vile ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii katika jamii husika. Hivyo, pamoja na kutoa taarifa za fedha zinazojikita katika faida ni muhimu taarifa za kijamii nazo zitolewe.

Haki za binadamu

Operesheni za kampuni huweza kuathiri haki za binadamu. Wadau hutaka uzalishaji unaojali haki za binadamu kwa mapana yake. Kampuni zinategemewa kuweka wazi namna zinavyojali haki za binadamu.

Kwa mfano hazipaswi kuwatumia watumwa au watoto katika uzalishaji. Hazitakiwi kuwa na mazingira ya kazi yasiyo na staha kwani kazi zenye staha hufanyika katika mazingira mazuri kwa maana ya mwanga, hewa na nafasi ya kutosha, usafi, ujira unaoendana na kazi, mapumziko na fidia stahiki.

Utawala bora

Kuna mtizamo potofu kuwa utawala bora unapaswa kudaiwa kutoka serikalini tu. Katika mapana yake, utawala bora unajumuisha uwazi, uwajibikaji, kutokuwa na rushwa na manyanyaso na kuwa na bodi za wakurugenzi.

Katika uzalishaji mali na taarifa za kampuni taarifa za utawala bora wa kampuni husika zinahitajika. Hairidhishi kuelezwa faida tu. Wapo wawekezaji katika kampuni ambao hawatanunua hisa bila kuona taarifa za uwazi, uwajibikaji na tathmini ya vitendo vya rushwa.

Taasisi za fedha hasa zinazotoa mikopo huweza kudai taarifa hizi kabla ya kukubali kutoa fedha hata kama ukokotoaji unaonyesha faida.

Ushauri

Kwa kuzingatia ukweli kwamba wadau wanataka taarifa za hesabu za fedha na zisizo za fedha kama ilivyoainishwa, ni muhimu mambo kadhaa kufanywa. Pale ambapo kampuni hazitoi taarifa hizi ni vizuri na muhimu zikafanya hivyo.