Wageni Dar wanavyoongeza idadi ya wagonjwa wa TB

Kifua Kikuu maarufu TB, ni ugonjwa sugu unaoambukizwa na vimelea aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho ila kwa hadubini na kipo kifua kikuu cha ndani ya mapafu na cha nje ya mapafu.

Inaelezwa kuwa zaidi ya watu bilioni mbili duniani wanaugua TB. Huu ni ugonjwa unaoshika nafasi ya tisa kwa kuua kati ya maradhi yote yasababishwayo na vimelea.

Kifua Kikuu kimekuwa chanzo cha vifo milioni 1.3 kwa wale wasio na virusi vya ukimwi (VVU) na 374,000 kwa waliokuwa na VVU, ambao ndiyo hushambuliwa zaidi.

Wastani wa watu milioni 10.4 waliugua kifua kikuu huku kati yao asilimia 90 ni watu wazima ambapo asilimia 65 walikuwa wanaume na asilimia 10 walikuwa ni wenye virusi vya Ukimwi.

Hali ya TB Tanzania

Wakati takwimu hizi zikitajwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi mengi ya TB duniani.

Mkoa wa Dar es Salaam pekee, umegundua wagonjwa wengi wa TB kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mikoa mingine kutokana na takwimu za mwaka 2017 za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu (NTLP).

Unafuatiwa na mikoa ya Mwanza kwa asilimia 6, Mbeya (5), Arusha (5), Dodoma (5), Morogoro (5) na iliyosalia ilijumuishwa katika asilimia 54 zilizosalia.

Mfuatiliaji wa tathmini kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti TB, Dk Zuweina Kondo anasema idadi kubwa ya wagonjwa wanaopatikana Mkoani Dar es Salaam huchangiwa na uwapo wa vituo vingi vya maabara vinavyopima vimelea vya ugonjwa huo tofauti na mikoa mingine.

Pia, mkoa huo unapokea wagonjwa wengi kutoka mikoa mingine wanaofuata matibabu na mara wapimwapo, hubaini kuwa na maradhi ya TB na kufanya idadi hiyo ihesabike kama wao pia ni wakazi wa Dar es Salaam wakati sivyo hivyo.

“Mkoa huu una idadi kubwa ya wagonjwa tuliowagundua na kuwaweka katika matibabu, hii haimaanishi kuwa ndiyo unaoongoza Tanzania hapana, ila ni mkoa wenye maabara nyingi ambazo zinaweza kuhudumia jamii kwa upana wake,” anasema.

Dk Kondo anasema takwimu hizo zinaonyesha kati ya watu 100,000, watu 287 wana maambukizi ya vimelea vya TB, hivyo kulingana na ripoti ya NBS ya mwaka 2018 ya idadi ya watu milioni 54, takwimu zinaonyesha kati yao 160,000 wanaugua ugonjwa huo kati ya Watanzania wote.

Anasema baada ya vipimo vya maabara kote nchini, wameweza kuwabaini Watanzania 64,000 na kuwaingiza kwenye dawa sawa na asilimia 40 ya waliotarajiwa kufikiwa huku asilimia 60 wakishindwa kuwapata.

Kifua kikuu sugu

Akizungumzia kifua kikuu sugu, Dk Kondo anasema mwaka 2016, wagonjwa 158 kati ya 730 sawa na asilimia 22 walianza matibabu. Anasema asilimia 5.6 walikuwa watoto na asilimia 44 walikuwa na maambukizi shirikishi ya virusi vya Ukimwi na vifo vilikuwa kwa asilimia 17.

Mikakati ya kupambana na TB

Anasema katika mikakati ya kupambana na kifua kikuu, nchi imejiwekea mipango ya taifa ya Sera ya Afya, Mpango mkakati wa afya, Mkakati wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti TB na Ukoma na Mpango mkakati wa mwaka 2015-16 hadi 2019-2020.

“Tumejipanga katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la ugunduzi wa wagonjwa, dawa na uchunguzi,” anasema.

Dk Kondo anafafanua kuwa katika maeneo waliyolenga ni pamoja na kifua kikuu kwa watoto, kifua kikuu sugu, maambukizi shirikishi ya Kifua kikuu na Ukimwi, ukoma, shughuli za jamii, uraghabishi mawasiliano na uhamasishaji jamii.

Anasema mafanikio katika kutibu kifua kikuu yameonekana miaka ya hivi karibuni kutoka asilimia 50 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 34 mwaka 2016 kwa mujibu wa ripoti ya NTLP ya mwaka 2016.

“Asilimia 90 wanapatiwa dawa nyumbani kwani vituo vinavyotoa huduma za maabara vimeongezeka kwa sasa kutoka 945 mwaka 2014 mpaka 1199 mwaka 2016,” anasema.

Anasema kumekuwa na wigo katika matumizi wa teknologia mpya ya GenXpert 160 na ugatuzi wa huduma za kifua kikuu sugu kufikia mikoa 27.

Naye Naibu meneja wa mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma, Dk Liberate Mleoh anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa duniani.

Anasema changamoto inayowakumba zaidi ni kuwakosa asilimia 60 ya wagonjwa ambapo hadi sasa wamefanikiwa kuwafikia asilimia 40 pekee.

“Bado hatujaweza kuwafikia makundi yanayoathirika zaidi wakiwemo wajidunga na migodini lakini ushiriki wa vituo vya tiba binafsi ni mdogo,” anasema.

Dk Mleoh anasema idadi ndogo wa asasi za kijamii na NGO kujihusisha na masuala ya TB ni changamoto kubwa kwao ikiwemo wagonjwa wa ukoma kuchelewa kugunduliwa.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Mohammed Bakari Kambi alisema matibabu ya kifua kikuu ni ya muda mrefu, lakini pia ni muhimu kwa mgonjwa akianza matibabu hayo ahakikishe anamalizia ule muda wote ambao anatakiwa awe kwenye matibabu na hiyo ndiyo inaihakikishia Serikali kwamba inatibu ipasavyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu anakiri kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zinazoongoza kwa maambukizi ya virusi vya Kifua Kikuu.

Anatoa wito kwa wauzaji wa dawa za binadamu kuacha mara moja kutoa dawa pasipo cheti cha daktari.

“Nitoe wito kwa watu wote wenye maduka ya dawa, huruhusiwi kuuza dawa bila cheti cha daktari, tutaweka tangazo iwapo unakohoa zaidi ya wiki mbili hutaruhusiwa kuuziwa dawa bila cheti cah daktari.”

Pamoja na kwamba matibabu hayo hutolewa bure, Serikali imesema imeamua kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa matibabu hayo kwa pamoja.

“Tumeshirikiana na wenzetu wa sekta binafsi takribani vituo vya afya 1200 na vimeweza kutoa huduma za uchunguzi kwa asilimia 5.5 ya wagonjwa na baada ya kushirikiana nao wamefikia asilimia 10.4.”