Wagombea 106 wawekewa ngumu uchaguzi wa Kenya

Mmoja wa wanaharakati wa Kenya akionyesha bango kupinga baadhi ya wagombea wenye tuhuma mbalimbali za ufisadi kupitishwa katika uchaguzi wa nchi hiyo. Picha na Mtandao

Muktasari:

Yakiongozwa na Kenya National Integrity Alliance, mashirika hayo yanataka wagombea 106 wazuiwe kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi na mambo mengine yanayokiuka maadili ya kijamii.

Mashirika ya haki za kijamii yamewaweka katika wakati mgumu wagombea wasio na rekodi nzuri na yanataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kuwazuia kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 8.

Yakiongozwa na Kenya National Integrity Alliance, mashirika hayo yanataka wagombea 106 wazuiwe kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi na mambo mengine yanayokiuka maadili ya kijamii.

Hatua hii imezua tumbojoto miongoni mwa waliotajwa, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mipango ya Kitaifa, Ann Waiguru na aliyekuwa Msajili Mkuu wa Mahakama, Gladys Shollei.

Waiguru alilazimishwa kujiuzulu 2015 baada ya wizara yake kupoteza zaidi ya Sh1 bilioni kwa ufisadi.

Waiguru sasa anagombea ugavana wa Jimbo la Kirinyaga na ana nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kwa sababu ya umaarufu wake.

Bunge pia linataka mwanasiasa huyo kuzuiwa kugombea kiti hicho kwa sababu ya sakata la wizi wa fedha lililosababisha miradi inayolenga vijana, kufilisika.

Waiguru ni mwandani mkuu wa Rais Uhuru Kenyatta na amefanya kazi naye katika nyadhifa mbalimbali kuanzia 2008 wakati Kenyatta akiwa naibu waziri mkuu katika Serikali ya Muungano.

Mgombea huyo wa ugavana anaapa kuwa hakuiba pesa. Anawalaumu waliokuwa chini yake kwa kupora fedha za umma. Wafuasi wake wamekwenda mahakamani wakitaka majaji waamuru mwanasiasa huyo akubaliwe kugombea kiti hicho. Waiguru anasema badala ya kutuhumiwa na kulaumiwa kwa kupora fedha hizo, anafaa kupewa hongera kwa sababu ni yeye alijitwika jukumu la kupiga kipenga kilichozuia fdha faidi kuibwa na hatimaye kunaswa na kushtakiwa kwa wizi huo.

Kwa upande wake, Shollei amejitenga na madai kuwa alihusika kwenye mipango ya kupora fedha za Idara ya Mahakama kwa kuongeza bei ya nyumba ya Jaji Mkuu iliyokuwa inanunuliwa miaka minne iliyopita.

Shollei anawania kiti kuwakilisha wanawake katika jimbo la Uasin Gishu baada ya kufutwa kazi na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) miaka mitatu iliyopita.

Wakili huyu ambaye sasa ni mwanasiasa ana hamaki si haba kwa kutuhumiwa kwa kosa ambalo mahakama haikumpata na hatia baada ya kesi kuamuliwa.

Anahoji ni kwa nini watu fulani wanafanya bidii usiku na mchana wakilenga awekewe vizingiti ili asiwanie kiti hicho.

Isitoshe, Shollei anasema kuwa mashirika hayo hayana haki kisheria kuzuia yeyote kuwania kiti chochote, akiongeza kuwa aliye na uwezo huo ni mahakama.

Mashirika hayo yamepeleka maombi hayo kwa IEBC yakisisitiza wanasiasa wenye kesi za ufisadi wasiruhusiwe kushuka kwenye mirekebu ya siasa za 2017.

Majina hayo ya wanasiasa 106 yako kwenye orodha ya tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC).Yanasema wanasiasa hao hawana maadili na kwa hiyo hawawezi kuongoza vyema.

Yanaongeza kuwa IEBC ina jukumu la kimaadili kutoorodhesha majina hayo kwenye gazeti rasmi ya Serikali.

Itakuwa vigumu kwa EACC kukosa kuorodhesha kwa kuwa wanasiasa hao wote wameshakabidhiwa vyeti vyao vya kugombea viti mbalimbali kote nchini.

Wakizuiwa, itabidi kura nyingine ya mchujo ipangwe na kufanywa, jambo ambalo halitakuwa bora ikizingatiwa kuwa zoezi hilo lahitaji pesa. Swali ni je, pesa za kufanya zoezi lingine la mchujo zitapatikana wapi?

Msingi wa mashirika hayo kutaka hatua zichukuliwe kwa washukiwa wa ufisadi na uhalifu mwingine, unajikita kwenye Katiba. Ibara ya Sita wa Katiba ya Kenya inasema Mkenya yeyote ambaye ana dosari hata kidogo ya uadilifu na mienendo hana budi kuzuiwa kugombea kiti cha kisiasa na kamwe hawezi kukubaliwa kupewa wadhifa wowote serikalini.

Haki ya kikatiba inakubali watu wenye doa kuhujumiwa lakini sheria inaonekana kutumiwa vibaya. Shollei na wengine waliojikuta pabaya wanalalama kwamba kuna watu fulani ambao wana dhambi nyingi za kiufisadi na mambo mengine ambao hawako kwenye orodha hii ya watu 106.

Wanataka haki iwe ngao na mlinzi wa wote. Shirika Transparency International (IT) linalojihusisha na masuala ya uwazi katika ngazi zote za kijamii inasema ingawa IEBC imewakabidhi washukiwa hao vyeti vya kugombea katika uchaguzi, ni wazi kuwa orodha ya mwisho na iliyokamilika ya wagombea watakaowania viti mbalimbali bado haijachapishwa kwenye gazeti rasmi la Serikali.

Mkurugenzi mtendaji wa IT, Samuel Kimeu anasisitiza kuwa wagombea wasio na dosari wala doa ndio wanafaa kuteuliwa.

IEBC ilipokea karatasi za uteuzi kutoka kwa wawaniaji mbalimbali kote nchini kaunzia Mei 28 na itaendelea hadi Julai 28.

EACC ilitoa majina ya watu hao 106 kwa EIBC ikitaka wachukuliwe hatua na kuadhibiwa mara moja kwa kujihusisha na ufisadi na mambo mengine mabaya.

Miongoni mwa viongozi hao 106 wanaochunguzwa na EACC, 11 wanawania ugavana, mmoja analenga useneta; wawili wanawania viti vya mjumbe mwakilishi wa Wanawake, 13 wanagombea ubunge wa kitaifa huku 14 wanawania uwakilishi wa wadi.

Orodha ya EACC yaonyesha kuwa wawaniaji wenye kesi kortini ni wanaowania ugavana ni sita, wawili wanawania useneta na mmoja anagombea kiti cha Mwakilishi wa Wanawake bungeni. Tisa wanawania ubunge wa kitaifa na 23 wanawania uwakilishi wa wadi.

Kimeu analenga ya kurejesha heshima na na uaminifu kwa nyadhifa mbalimbali za umma kulingana na ibara ya wa Sita ya Katiba.

Sehemu hii ya katiba ni msingi wa uongozi bora na haina budi kutekelezwa kwa vyovyote vile.

Viongozi wetu wamezoea kufanya uhalifu na kukwepa mkono refu wa sheria lakini sasa wajihadhari kwa sababu wanaweza kufungiwa nje. Hii itasaidia kutoa onyo kwa wengine wanaojaribu kuiba mali ya umma na kujitajirisha, kisha wanatumia mali hiyo kuwania viti na kupata nafasi nyingine ya kupora na kufilisi miradi balimbali.

Hii imeleta ufukara na magonjwa kwa wananchi kwa sababu pesa zinazotengewa miradi na maendeleo ya kijamii haziwafikii wanaolengwa.

Miongoni mwa wale wamejipata kwa orodha hii, ni wale waliotuhumiwa kwa kutoa matamshi yanayotisha maisha ya Wakenya. Wengine walitumia ujanja kujipatia shahada ya chuo kikuu ili waweze kukukubaliwa kupigania viti vya kisiasa ama kupata ajira za vyeo vya juu serikalini.

TI imeomba makundi mengine yanayolenga kustaawishwa kwa ibara ya 6 wa katiba unaosisitiza maadili miongoni mwa Wakenya wote, watoe ripoti zao haraka iwezekanavyo ili hatua inayofaa ichukuliwe kwa waliotajwa.

Makundi hayo ni tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu, Mwanasheria Mkuu na ofisi ya mkurugenzi wa kesi za umma.

Irungu Houghton ambaye anaongoza moja ya mashirika hayo anasema azma yao ni kuhakikisha Kenya inaongozwa na watu wenye maadili bora.

Anasisitiza kuwa kamwe hawatalegeza Kamba hadi azma yao itimie kwa vyovyote vile.

Huku mashirika hayo yakindelea kuwasha moto chini ya viti vya wagombea hao 106, wengi wanasubiri kama kweli watafanikiwa kuwazuia baada ya wao kupokea vyeti vya kura ya mchujo.

Hakuna mwaniaji wa urais aliyelengwa na mashirika hayo. Wengine waliolengwa ni magavana Evans Kidero (Nairobi), Alfred Mutua (Machakos), Hassan Joho (Mombasa), Kenneth Lusaka (Bungoma), Okoth Obado (Migori), Mwangi Wa Iria (Murang’a) na Cyprian Awiti (Homa Bay).

Pia walio mashakani ni Seneta wa Nairobi, Mike Sonko, Seneta mteule Elizabeth Ongoro, mgombea wa ugavana wa Homa Bay, George Ochilo Ayacko na Mbunge Mathew Lempurkel.