UCHAMBUZI: Wahujumu wa elimu washughulikiwe

Rais John Magufuli

Muktasari:

Jambo hili halikutokea kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na ukweli kuwa bila elimu bora taifa lolote haliwezi kufika popote.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, moja ya ajenda kubwa ya wagombea karibu wa vyama vyote ilikuwa na suala la elimu.

Jambo hili halikutokea kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na ukweli kuwa bila elimu bora taifa lolote haliwezi kufika popote.

Wagombea wote walieleza wakichaguliwa watahakikisha wanaboresha elimu kuanzia msingi ya msingi hadi elimu ya juu.

Wagombea wa vyama vikubwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walikuja na sera ya elimu bure.

Baada ya matokeo kutangazwa CCM ilipewa ridhaa ya kuliongoza na Taifa na kama mgombea wake, Dk John Magufuli alivyoahidi, mpango wa elimu bure ulianza kutekelezwa.

Serikali imekuwa ikitenga zaidi ya bilioni 18 kila mwezi kugharimia mpango huo wenye mafanikio makubwa.

Hata hivyo, jitihada hizi, zinaanza kuhujumiwa na watu wachache na katika siku za karibuni, tunashuhudia matukio ya shule kuungua moto na kuwapo kwa wanafunzi hewa.

Naomba nizungumzie suala la shule kuungua moto, tatizo ambalo limekumba mikoa mingi ukiwamo Arusha.

Matukio haya, hadi sasa yamesababisha hasara zaidi ya milioni 300 baada ya moto kuunguza shule tano kwa kuteketeza majengo, vifaa vya shule na vifaa mbali mbali vya wanafunzi. Matukio haya yalisahaulika, lakini yameanza kuibuka kidogokidogo.

Kuna mengi yanaelezwa kuwa nyuma ya matukio haya, wapo wanaohusisha na uadui baina ya shule na wananchi, migogoro baina ya walimu na wanafunzi na mengine yanahusisha na hitilafu za umeme. Sababu zote hizi, zinaweza kudhibitiwa.

Haiwezekani ndani ya mwezi mmoja tu, shule tano za sekondari zimeungua moto mkoani Arusha bila wahusika wakuu kutambulika .

Matukio haya yalianza wilaya ya Monduli, shule tatu ziliungua moto, yakahamia Longido shule moja ikaungua na sasa yameingia Arumeru.

Shule zilizoungua monduli ni shule ya sekondari,Lowassa, shule ya Nanja na shule ya Sokoine na kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Monduli Idd Kimanta hasara ya zaidi ya milioni 215 zimepatikana.

Katika wilaya ya Longido, Shule ya Longido Sekondari, wanafunzi 169 wamekosa mahala ya kulala kutokana na bweni lao kuungua moto.

Mkuu wa wilaya hii, Daniel Chongolo anasema hasara iliyosababishwa na moto huo ni kubwa na akaahidi Serikali kuhakikisha inatambua wahusika.

Katika wilaya ya Arumeru, mabweni ya shule ya Mlangarini hivi karibuni yameungua moto na kusababisha hasara kubwa, huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Felix Ntibenda akiagiza kukamatwa kwa mkuu wa shule na walinzi kwa tuhuma za uzembe

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na maagizo ya awali ya kamati ya ulinzi na usalama kutaka ulinzi katika shule zote kuimarishwa kwa kuhakikisha wanakuwepo walinzi wenye sifa na kushirikisha vyombo vya dola.

Kwa jumla matukio haya hayawezi kuvumilika, kwani mabweni yanaungua wakati wanafunzi wapo madarasani wanajisomea, itakuwaje mabweni yakiungua wakati wanafunzi wamelala.

Naamini Serikali ina vyombo vingi vinavyoweza kulimaliza tatizo hili na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Inawezekana pia ikawa ni hitilafu ya umeme na kama ni kweli, ni lazima sasa mifumo ya umeme katika shule zote za bweni ikapitiwa upya ili kuhakikisha matatizo ya shule kuungua moto yanakwisha.

Musa Juma ni mwandishi wa Mwananchi 0754296503