MAONI YA MHARIRI: Wahusika shambulio la CUF wanasakwa wapi?

Muktasari:

Wabunge wanaomuunga mkono katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad walifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza mpango wao wa kwenda ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni kusafisha kila kitu ambacho hakistahili kuwepo.

Jana, pande mbili zinazosigana ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) zilitoa matamko ambayo yanaashiria hali isiyo nzuri, si tu katika siasa za chama hicho, bali za nchi kwa ujumla.

Wabunge wanaomuunga mkono katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad walifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza mpango wao wa kwenda ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni kusafisha kila kitu ambacho hakistahili kuwepo.

Kauli yao inamaanisha-na ndivyo ilivyoelezwa na wabunge hao- kuwa shughuli hiyo itahusisha hata kumuondoa Profesa Ibrahim Lipumba ambaye wanaamini kuwa si mwenyekiti wa chama hicho baada ya kumkubalia barua yake ya kujiuzulu.

Profesa Lipumba, ambaye aliandika barua ya kujiuzulu mwaka juzi kabla ya kubatilisha uamuzi huo mwaka jana, naye amejibu kuwa ameshajiandaa kwa ujio huo ambao ameuelezea kuwa unaweza kutumiwa na waovu kufanya vurugu na hivyo amelitaarifu Jeshi la Polisi. Hatua zilizofikia pande hizo mbili ni matokeo ya mlolongo wa matukio ya kisiasa yaliyotokea ndani ya chama hicho kuanzia mwaka jana wakati Profesa Lipumba alipoamua kurejea madarakani, lakini akakataliwa na Mkutano Mkuu.

Kati ya matukio hayo, yamo ambayo vyombo vya usalama vilitakiwa kuingilia kati kuhakikisha inazuia uwezekano wa vitendo viovu kuendelea kutawala katika siasa. Lakini tukio la hivi karibuni ndilo limeshangaza wengi kuhusu ushiriki wa polisi katika kuhakikisha inazuia vurugu zozote na kuchukulia hatua vitendo ambavyo vinaashiria kutokea kwa vurugu.

Mwenyekiti wa CUF wilayani Kinondoni aliandaa mkutano na waandishi wa habari kupinga tuhuma zilizotolewa na kundi linalomuunga mkono Profesa Lipumba kuwa kuna njama dhidi ya mchumi huyo.

Wakati mkutano huo ukikaribia mwisho, kikundi cha watu wanne, mmoja wao akiwa ameficha sura kwa kofia mithili ya soksi, maarufu kama Ninja, na ambaye alikuwa na bastola, kilivamia ukumbini na kuanza kuwapiga waandaaji na waandishi wa habari waliokuwepo.

Watu hao walienda kwenye hoteli ulikofanyika mkutano huo wakitumia gari lenye nembo ya CUF. Mmoja wa watu hao, hakufanikiwa kuondoka na wenzake eneo la tukio baada ya kudhibitiwa na wananchi na hivyo kushambuliwa hadi kukatwa sehemu ya kisigino.

Hadi sasa habari hizo zimezungumzwa na waandishi wa habari waliokuwa eneo la tukio na baadhi ya watu, lakini Jeshi la Polisi halijatoa tamko lolote kuhusu shambulio hilo, kuhusu wahusika na hatua ilizochukua, zaidi ya kusema inaendelea kuwasaka wahusika.

Cha ajabu, mkurugenzi wa CUF wa mawasiliano ya umma ambaye anamuunga mkono Profesa Lipumba, alitoa tamko mbele ya waandishi wa habari akisema mtu aliyedhibitiwa na wananchi ni mmoja wa askari wa upande wao na alienda hotelini hapo na wenzake kwa ajili ya kulinda doria.

Tunadhani kiongozi huyo ndiye alitakiwa kuwa mtu wa kwanza kuhojiwa na polisi kwa kuwa na ufahamu wa watu walioenda kushambulia mkutano wa waandishi wa habari, kujua mtu aliyetumia vibaya bastola kuvamia na kutishia watu na mtu ambaye anafahamu kikundi kilichojitwalia jukumu la kufanya doria bila ya ruhusa ya polisi.

Matukio kama haya yanapoachiwa yaishe bila ya wahusika kuchukuliwa hatua, yanachochea kuendelea kwa vitendo vya watu kutumia vibaya silaha za moto, lakini pia kuanza kuondoa amani katika vyama vya siasa. Wito wetu kwa Jeshi la Polisi waliangalie shambulio hilo kama tukio hatari na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu waliohusika kupanga mipango ya kushambulia na walioshiriki ili kukomesha vitendo hivyo.